7:21 AM
MWANAMKE mmoja mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru
mkoani Arusha, Melisiana Kabunde (29) amekamatwa na maguni 26 ya dawa za
kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 1300.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Liberartus
Sabas alisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye
ni mkulima alikamatwa juzi majira ya saa 4 asubuhi nyumbani kwake Ngaramtoni
alikohifadhi bangi hiyo.
Sabas katika taarifa yake alisema kuwa kukamatwa kwa Kabunde ni kufuatia
taarifa njema kutoka kwa raia wema kuwa mtuhumiwa amekuwa na tabia ya kuhifadhi
bangi nyumbani kwake na ndipo polisi ilipokwenda kufanya upekuzi na kufanikiwa
kukamata kiasi hicho cha bangi ambacho thamani yake haijajulikana.
Kamanda alisema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani
Arusha na bado upelelezi wa tuhuma za kupatikana na bangi bado unaendelea.
Wakati huohuo Polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na raia wema Desemba
13 mwaka huu majira ya saa 10 jioni eneo la stendi kuu walifanikiwa kukamata
noti bandia za Shilingi elfu kumi kumi za milioni 6 .
Taarifa ya Kamanda Sabas ilisema kuwa noti hizo zilikamatwa mara baada
ya Imelda Juma kumtuma Jamal Abdul ambaye ni dereva wa usafiri wa pikipiki
maarufu kama Toyo kwenda kuchukua mzigo huko Sakina Darajani na alipofika
alielekezwa mzigo ulipo bila ya kuwepo mtu wa kumkabidhi mzigo huo ambao
ulichukuliwa na kuondoka chini ya pikipiki iliyokuwa imepaki hapo.
Kamanda alisema dereva wa Toyo alichukua mzigo huo na kuondoka nao hadi
katika kituo cha mabasi ya Dar –Express kwa maelekezo aliyopewa kuwa atume
mzigo huo Dar es Salaam kwa mtu aitwaye Emmanuel ambaye ndiye mwenye mzigo huo.
Alisema hata hivyo uongozi wa basi la Dar –Express uligoma kusafirisha
mzigo huo bila ya kupekuliwa hatua iliyopingwa na Emmanuel na ndipo mbeba mzigo
aliambiwa achukua Sh 50,000 akate tiketi na ada ya mzigo huo.
Kamanda alisema dereva wa Toyo alifanya hivyo na alikuwa tayari kusafiri
na mzigo huo lakini alichukua Sh 10,000 ili akanunue juisi lakini aliiangalia
noti hiyo na kugundua kuwa ni bandia na alitoa taarifa Polisi na Imerda Juma
alikamatwa.
Polisi inaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini mtandao wa
utengenezaji wa noti bandia na Imerda Juma anaendelea kuhojiwa na Polisi na
upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
0 comments:
Post a Comment