Saturday, February 8, 2014

Jumba la Maajabu linavyochochea utalii Zanzibar

KATIKA kipindi cha sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya watalii wa nje na wa ndani wanaongezeka katika visiwa vya Zanzibar kutembelea vivutio vya utalii na hasa Jumba la Maajabu ambalo limesheheni historia kuhusu Zanzibar na ubunifu mkubwa juu ya usanifu wa majengo kwa kutumia teknolojia ya kipekee.
Jumba hilo maarufu kama Beit-al- Ajaib kwa lugha ya Kiarabu ni miongoni mwa vitu vya kipekee vinavyopatikana katika visiwa vya Zanzibar na limehifadhi kumbukumbu na historia ndefu kuhusu ubunifu na maendeleo ya Zanzibar.
Jumba hilo lipo barabara ya Mizingani katika ufukwe wa bahari na linaonekana kwa urahisi unapoingia Zanzibar kwa njia ya bahari.
Jumba hilo lenye zaidi ya miaka 125 ni sehemu ya kivutio muhimu kwa watalii ambao wanafika Zanzibar kila siku kwa ajili ya kujifunza tamaduni, mambo ya kale na hatua za maendeleo katika jamii ya Waafrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Utamaduni Zanzibar, jumba hilo huonekana la ajabu kutokana na ujenzi wake pia ni la kwanza kutumia maji ya bomba. Lina nguzo zaidi ya 40 zilizojengwa kwa ustadi mkubwa.
Wajenzi wa jumba hilo walitumia mchanganyiko wa utaalamu kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Asia na Ulaya ingawa lilisimamiwa na utawala wa Sultani kutoka jamii ya Waarabu.
Jengo la kwanza kutumia umeme
Jumba hilo limepata umaarufu mkubwa kwa kuwa lilikuwa jengo la kwanza Afrika Mashariki kutumia umeme. Wakati huo watu walikuwa wakitumia kandili, vibatari na mishumaa kwa ajili ya kupata mwanga nyakati za usiku.
Pia wapo ambao walikoka moto mkubwa ili kupata mwanga wa kukamilisha shughuli zao kabla ya kulala.
Lakini jumba hilo lilikuwa likiwaka taa ambazo zilibandikwa ukutani na nyingine zilining’inia kutoka uzi mrefu uliotundikwa kwenye dari.
Kwa kuwa mwanga wa taa hizo ulionekana kwa mbali ulisababisha watu wengi kupigwa na butwaa.
Taarifa za kuwepo kwa jumba lenye taa za ajabu zilisambaa katika ukanda wote wa Afrika Mashariki hivyo watu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania hasa wavuvi walisafiri hadi Zanzibar kushuhudia maajabu ya jumba hilo.
Kuwa na lifti.
Jumba hilo la ghorofa lilikuwa jengo la kwanza kuwa na lifti katika ukanda wa Afrika Mashariki. Tofauti na majengo mengine ambayo ilikuwa ni lazima kupanda ngazi ili ufike ghorofani wageni waliofika kwenye jengo hilo hawakupanda ngazi bali walitumia lifti.
Lift ni mashine maalum inayokaa katika chumba kidogo ambapo watu huponyeza kitufe na kisha mashine hiyo huwapandisha hadi ghorofa ya juu na kumshusha tena ghorofa ya chini pasipo pasipo kutumia ngazi.
Habari za kuwepo kwa lifti katika jengo hilo zilizua gumzo na maswali mengi katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Wavuvi na wasafiri waliofika Zanzibar walikwenda kwenye jumba hilo kwa lengo la kuingia ndani ili waweze kushuhudia maajabu wanayoyasikia.
Mfumo wa maji.
Mfumo wa maji taka na maji safi ya bomba ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha jumba hilo kuonekana la maajabu. Wakati majengo mengine ya kifahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki yalikuwa na vyombo mbalimbali kuhifadhia maji, Jumba la maajabu lilikuwa la kwanza kuwa na bomba zinazotiririsha maji ndani ya nyumba.
Jumba hilo lilipata umaarufu zaidi baada ya kuwekwa mfumo wa maji safi na salama pia mfumo wa maji taka. Pia mfumo huo ulisababisha baadhi ya watu kujawa wa maswali mengi juu ya uwepo wa maji safi katika jumba lililopo kwenye kisiwa kilichozungukwa na bahari yenye maji ya chumvi.
Hata wataalamu waliofika katika jengo hilo walishangazwa na ubora na uzuri wa jengo hilo lililojengwa kwa mtindo wa kipekee. Kwa mujibu wa historia ya Zanzibar, ubunifu wa jumba hilo ulifanywa na askari wa meli toka Scottland na lilijengwa na Sultan Barghash bin Said katika mwaka wa 1883, kwa ajili ya ofisi yake.
Matumizi ya jengo.
Hata hivyo matumizi ya jumba hilo yalikuwa yakibadilika kadiri miaka ilivyokuwa ikienda na jinsi tawala zilivyokuwa zikibadilika visiwani humo. Kati ya mwaka 1870 na 1888 jumba hilo lilitumika kwa ajili ya sherehe za kitaifa chini ya utawala  wa kisultani.
Mwaka 1913 utawala wa kikoloni wa Waingereza ulibadilisha matumizi ya jumba hilo na kulifanya ofisi za Serikali za Mitaa. Inaaminika kuwa hadi sasa hakuna jengo lolote la ofisi ya Serikali za Mitaa Tanzania bara na visiwani ambalo linakaribia kuwa na hadhi ya jumba hilo la maajabu.
Baada ya Zanzibar kupata uhuru matumizi ya jengo hilo yalibadilishwa na kuwa jumba la kumbukumbu za kihistoria kuhusu harakati za ukombozi wa Zanzibar. Kati ya mwaka 1964 na 1977 Jumba hilo maarufu lilitumika kama jumba la kuhifadhi kumbukumbu za chama cha Afro Shiraz Party (ASP) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) .
Baada ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 1977 jumba hilo kumbukumbu nyingine muhimu pia kama ofisi ya CCM, hali ya jumba haikuwa ya kuridhisha sana pamoja na kuwa na historia ndefu.
Kwa mfano ndio ilikuwa sehemu pekee ya kuweza kuona magari ya Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amaan Karume.
Jumba hilo lilibadilishwa matumizi na kuwa sehemu ya hifadhi ya Taifa kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za kale hasa zile zinazohusiana na jumba hilo na maajabu yake.
Uzuri wa jumba hilo umekuwa moja ya hazina ya historia iliyouwezesha Mji Mkongwe kuwa katika orodha ya urithi wa Dunia uliyohifadhiwa na Shirika la Kimataifa ya Maendeleo ya Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Katika jumba hilo kuna makumbusho ya utamaduni wa Jahazi ambapo kuna picha za majahazi ya msimu yaliunganisha Mwambao wa Mswahili na sehemu nyinginezo za Bahari ya Hindi. Lina michoro na zana za kale zinazoelezwa shughuli mbalimbali za wenyeji na wageni ambao wameifanya Zanzibar kuwa kisiwa cha watu wenye asili tofauti.
Katika jumba hilo kuna chombo cha usafiri maarufu kama Mtepe ambacho kiliundwa bila kutumia misumari.
Pia ukitembelea jumba hilo utaona kumbukumbu za utaarabu wa Waswahili ambao unawakilishwa na tamaduni mbalimbali kama vile majengo, mavazi, uchongaji, imani, lugha, nyimbo na ngoma.
Kumbukumbu ya vita.
Jengo hilo limehifadhi kumbukumbu ya vita vilivyodumu kwa muda mfupi katika historia ya vita duniani.
Vita hii ilitokea Agosti mwaka 1896 na inadaiwa kuwa vilidumu kwa takribani dakika 32 tu.
Kwa mujibu wa historia, vita hiyo ilitokea mara baada ya kifo cha ghafla cha Sultani Sayyid Hamid Thuwain bin Said ambaye alifariki tarehe Agosti 25, 1896. Baada ya kifo hicho kijana machachari Khalid bin Barghash alijitangaza kuwa mrithi wa Sultani Sultani Sayyid Hamid jambo ambapo lilipingwa na Waingereza.
Ingawa Barghash alikuwa kipenzi cha wenyeji wa Zanzibar hakuwa chaguo la Waingereza ambao ndio waliokuwa na jukumu la kulinda usalama wa Zanzibar kutokana na urafiki wa muda mrefu kati ya utawala wa Uingereza na utawala wa Kisultan ambao ulianzia Oman.
Waingereza walichukizwa na kitendo cha Barghash kujitwalia madaraka kwa kuwa walitaka Hamoud bin Mohamed awe mrithi kwa kuzingatia utaratibu uliokuwepo kwamba mkubwa ndio mwenye dhamana ya kurithi kiti cha mfalme endapo mfalme atafariki dunia.
Waingereza walimpendelea Hamoud bin Mohamed ambaye alikuwa mpwa wa aliyekuwa Sultan wa Oman na mtu aliyependelea zaidi maisha ya kisasa. Waingereza walimuamini angeweza kuwa rahisi zaidi kufanya naye kazi kuliko Khalid ambaye alikuwa mwerevu na mwenye uwezo wa kujitegemea. Waingereza walibaini kuwa maslahi yao yatapotea na hivyo walitoa onyo na kumtaka aachie madaraka vinginevyo wangetumia nguvu za kijeshi kumtoa.
Hata hivyo Barghash hakutishika na aliendelea kushika ngome zote muhimu kwa ajili ya kuimarisha himaya na utawalawake. Kuona hivyo Waingereza walijiandaa kwa ajili ya vita.
Serikali ya Uingereza ilimuagiza Mkuu wa Jeshi katika Bahari ya Hindi kuleta kwa haraka meli za kivita Zanzibar ili zikaungane na meli mbili za kivita za Kifalme ambazo zilikuwa zimetia nanga katika bandari wakati Sultan alipofariki.
Amri hiyo iliendelea hadi jioni ya Agosti tarehe 25, wanaume wa Kizanzibari katika uwa wa Kasri walikuwa na saa 40 kutafakari hatima yao. Ilikuwa kupigana au kukimbia.
Wangekaa? Wangeweza kweli kuendelea kusubiri tu na kukodoa macho kwa Simba wa Ubereru ambaye alikuwa anakaribia kuachiliwa dhidi yao?
Mnamo Agosti 26 1896 majeshi yalijiandaa kwa ajili ya vita ambayo ilifanyika kesho yake na kati ya dakika 37 hadi 45 ambapo Barghash alifanikiwa kuwaponyoka Waingereza na kukimbilia kusikojulikana.
Vita hiyo iliharibu baadhi ya jengo la maajabu hasa mnara wa saa hivyo kulifanya umbo la jengo hilo kubadilika kidogo hasa sehemu ya mbele.
Baadhi ya majengo ya Kisultani yaliharibika ikiwa ni pamoja na mnara wa saa uliokuwa katika jumba la maajabu.
Baada ya vita hiyo mnara huo ulifanyiwa matengenezo na hadi leo unatumika kama alama ya kumbukumbu ya vita hiyo inayoshikilia historia ya dunia ya vita iliyochukua muda mfupi kuliko vita zote.

0 comments:

Post a Comment