MBUNGE
wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), ameitaka Serikali itolee
tamko juu ya kauli ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ya
kuwataka Watanzania wasioweza kumudu bei mpya ya umeme watumie vibatari.
Katika
swali lake la nyongeza alilouliza kwa niaba ya Mbunge wa Maswa Mashariki
Sylvester Kasulumbayi (Chadema), Msigwa alitaka kujua Serikali inaichukuliaje
kauli hiyo ya kuwataka wananchi kutumia vibatari iwapo watashindwa kulipia bei
mpya ya umeme.
Akijibu
swali hilo, Simbachawene alikanusha kutoa matamshi hayo ya kuwataka wananchi
kutumia vibatari na kufafanua kuwa kamwe hawezi kudharau matumizi ya taa hiyo
ya asili, kwa kuwa ndio iliyomkuza.
Alikiri
kuhojiwa na Redio One Novemba 25, mwaka huu, kuhusu suala la kupanda kwa bei ya
umeme, ambapo akiwa kama mmoja wa watoa maamuzi, hakutaka kuzungumzia ukweli
kuwa bei hiyo inapanda au la.
“Nasikitika
nilinukuliwa vibaya na baadhi ya vyombo vya habari, niliposikia taarifa hii
niliomba mkanda wa mahojiano yangu kwa uongozi wa Redio One na kuyasikiliza
ukweli ni kwamba maneno haya hayamo, naomba Watanzania watambue kuwa
walipotoshwa,” alisisitiza Simbachawene.
Alisema
alichoulizwa katika mahojiano hayo, ni kama mwananchi wa kawaida ataweza
kulipia gharama za umeme za bei hiyo mpya kutokana na maisha magumu yaliyopo
sasa.
Alisema
katika majibu yake, alikwepa kukiri kuwa bei ya umeme inapanda au la, ila
alitumia neno kibatari wakati akilinganisha gharama halisi za matumizi ya umeme
wa kawaida na gharama za anayetumia nishati ya kibatari.
“Nilifafanua
kuwa mtumiaji wa kibatari ndiye mwenye gharama kubwa kutokana na mafuta ya taa
anayonunua kila siku, wakati yule wa umeme hutumia gharama nafuu kwa kulipia
mara moja kwa mwezi gharama ya Sh 1,500 kwa uniti, hii ndio dhana yangu ya
kutumia neno kibatari, siwezi kukashifu matumizi yake hata kidogo,” alisema.
Katika
swali la msingi la Kasulumbayi, alitaka kujua asilimia 35 ya pato la Watanzania
wa kipato cha chini inayotumika kwenye nishati imepanda au kushuka na iwapo
uvumbuzi wa visima vipya vya gesi asilia vimesaidia matumizi ya nishati kwa
Watanzania wenye kipato kidogo.
Akijibu
swali hilo, tangu kutolewa kwa takwimu hiyo mpya ya pato la mwananchi mwenye
kipato cha chini ni muda mrefu na sasa inahitajika takwimu mpya ambapo wizara
hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu itafanya utafiti kwa nchi nzima ili kupata kiwango kipya cha takwimu
hizo.
Kuhusu
uvumbuzi wa gesi asilia, Simbachawene, alisema kutokana na taarifa ya upembuzi
yakinifu, mradi wa kusambaza gesi asilia jijini Dar es Salaam utahusisha kaya
30,000, magari 8,000 ambayo yatajaza gesi kupitia vituo 15 vya gesi pamoja na
hoteli 10.
Alisema
gharama za mradi kwa sasa ni dola za Marekani milioni 65.1 na Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC) limemwajiri mwekezaji wa kudurusu upembuzi
uliofanyika awali ili kupata gharama halisi pamoja na kusanifu michoro ili
mradi ujengwe.








0 comments:
Post a Comment