QUNU, Afrika
Kusini
SIKU mbili baada
ya maziko ya Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ugomvi kati ya
watoto na wajukuu wa shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani,
umeibuka upya.
Inadaiwa siku
chache kabla ya maziko ya Mandela, mjukuu wake mkubwa, Mandla alifukuzwa katika
nyumba ya babu yake katika kijiji cha Qunu.
Mbali na
kufukuzwa, inadaiwa vitasa vya nyumba hiyo vilibadilishwa na huduma za maji na
umeme zilizokuwa zikitumika katika nyumba ya Mandla kijijini hapo,
zilisitishwa.
Hata usafiri kwa
ajili ya kwenda mazikoni haukutolewa kwa ndugu waliozaliwa pamoja na Mandla na
wanasiasa na viongozi wa dini waliokuwa wakishirikiana na mjukuu huyo,
walitengwa na wengine kukosa mwaliko wa kuhudhuria maziko ya Jumapili.
Inadaiwa kwamba
mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, alimtaka Mandla, ambaye ni Chifu wa
Mvezo, kijiji alichozaliwa Mandela, kutoa mifugo yake iliyokuwa katika eneo la
nyumba hiyo.
Gazeti la The
Times, limebainisha kwamba mjane wa Mandela, Graca Machel na mwanasheria wa
siku nyingi wa kiongozi huyo, George Bizos, walijaribu kuwataka wanafamilia hao
kudhibiti hali hiyo isijioneshe lakini bila mafanikio.
Kiini
Ugomvi huo
ulitokana na mgogoro ulioibuka wakati Mandela akiwa mahututi katika Hospitali
ya Med Clinic, kuhusu wapi alipaswa kuzikwa kati ya kijiji alichozaliwa cha
Mvezo au alichokulia cha Qunu.
Wosia wa Mandela
uliofunguliwa akiwa katika hospitali hiyo ya Pretoria, ulieleza wazi kuwa
alipenda azikwe karibu na wanawe walikozikwa na kwa wakati huo, makaburi yao
yalikuwa Mvezo.
Wanawe hao,
Makgato aliyefariki dunia mwaka 2005; Makaziwe, ambaye ni mwanawe wa kike wa
kwanza aliyefariki dunia akiwa mchanga mwaka 1948; na Madiba Thembekilea,
aliyekufa kwa ajali ya gari mwaka 1969; walizikwa Qunu.
Hata hivyo,
Mandla, ambaye ni mtoto wa Makgato na kiongozi mkuu wa ukoo wa Madiba, anaotoka
Mandela na Mbunge wa ANC, alifukua miili hiyo mwaka 2011 na kuizika upya Mvezo,
alikozaliwa babu yake.
Mahakamani
Uamuzi huo wa
Mandla ambao haukushirikisha familia, ulisababisha watoto wa Mandela,
wakiwakilishwa na Mwanasheria, Sandla Zigadla, kwenda mahakamani kutaka mabaki
ya ndugu zao, yarudishwe Qunu.
Jaji Lusindiso
Pakade, alitoa amri kumtaka Mandla aache kuingilia mchakato wa kuhamisha mabaki
ya miili hiyo kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Mandla alifanya jaribio la
kuzuia mchakato huo, lakini Jaji Pakade, alizuia jaribio hilo na badala yake
akakazia hukumu kutaka miili hiyo ifukuliwe haraka.
Nguvu yatumika
Baada ya hukumu hiyo, huku vyombo vya habari
vya Afrika Kusini na kimataifa vikishuhudia, maofisa wa Serikali walivunja
lango la makazi ya Mandla kwa vifaa maalumu, ili kutoa nafasi kwa gari la
kubeba maiti kuingia ndani yalikokuwa makaburi hayo.
Miili ilifukuliwa na uchunguzi wa kisayansi
kufanyika kwa takribani saa mbili na kuthibitisha kwamba ni mabaki ya watoto
hao, kabla ya kuzikwa upya Qunu.
Juzi, Mandla
alisema: “Kama ilivyo kwa karibu kila mmoja wetu katika familia, kabla ya kifo
cha babu, nilidhamiria kutoomboleza, nilijiandaa kusherehekea mazuri yote
aliyoniachia na aliyoacha kwa ajili ya ulimwengu.
“Hata hivyo,
nilikosea, kwa kuwa maumivu ya kumpoteza tata bila kutarajia, yaliniingia kama
vile niliyekatwa na kitu chenye ncha kali.”
Mjukuu huyo,
alisema alijikuta akiugua upweke siku chache baada ya kifo cha Madiba, pamoja
na kuwa karibu na familia. “Hata hivyo ujumbe wa kututakia faraja ulivyokuwa
ukitufikia, nilianza kupona,” alisema Mandla.
Pia alishukuru
Serikali kwa kuandaa masuala yaliyokuwa yakifanyika katika siku hizo 10 za
maombolezo na kuongeza kuwa kila kitu kilifanyika vizuri.









0 comments:
Post a Comment