

Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar
(JUWASEZA) Maalim Fadhil Hamada Mshamba akisoma risala kwenye mkutano
Mkuu wa Jumuiya hiyo uliofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hapo Skuli ya Sekondari ya Lumumba.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
**************************************

Walimu
Wakuu wa Skuli za Sekondari Nchini wanawajibu wa kuendelea
kushirikiana zaidi na wazazi katika kuhakikisha ufaulu mkubwa wa
wanafunzi unaongezeka zaidi kwa kuzingatia na kutumia akili zao.
Ushirikiano
huo unaweza kufikia lengo kubwa iwapo utakwenda sambamba na upatikanaji
wa uongozi ulio makini wa Kamati za maskuli katika maeneo mbali mbali
hapa nchini.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiufungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Jumuiya ya Walimu wakuu wa Skuli
za Sekondari Zanzibar unaofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya
Lumumba Mjini Zanzibar.
Balozi
Seif alisema jambo kubwa liliopo hivi sasa katika kuona wanafunzi wengi
wanafanikiwa katika muelekeo wa kitaaluma ni kujaribu kutumiwa mbinu za
pamoja baina ya pande hizo mbili na namna ya udhibiti wa matumizi
mabovu ya mitandao ya mawasiliano ya Kompyuta ambayo hufanywa na
wanafunzi walio wengi Nchini.
Alifahamisha
kwamba wanafunzi wa karne hii wamebahatika kupata nafasi nzuri ya
kusoma kupitia mitandao hiyo ya Kompyuta lakini wengi kati yao hutumia
fursa hiyo kwa kuangalia michezo na filam zilizo nje ya Maadili jambo
ambalo huzorotesha kiwango chao cha ufaulu kwenye mitihani yao.

Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba walimu Wakuu hao kusimamia vyema
majukumu ya kazi zao za kila siku kwa walimu na wanafunzi wao kwa lengo
la kunyanyua kiwango cha elimu kitakachokidhi mahitaji ya sasa ya
sayansi na Teknolojia Duniani.
Alifahamisha
kwamba Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 50 yanakwenda
sambamba na miaka 50 tokea kutangazwa kwa elimu bila ya malipo hapa
Zanzibar.
Alisema
katika kuthamini uzito wa Mapinduzi hayo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ipo katika
utekelezaji wa sera mpya ya elimu ya mwaka 2006.
Balozi
Seif alieleza kwamba lengo la sera hiyo ni kuweza kukabiliana na kasi
ya maendeleo iliyopo ulimwenguni hivi sasa, mabadiliko ya Teknolojia
kimazingira na kiakili katika kumuandaa vyema mtoto.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibart aliwapongeza Walimu Wakuu wa Skuli za
Sekondari Zanzibar kwa uamuzi wao wa kuanzisha jumuiya hiyo na kutoa
wito kwa skuli binafsi ambazo bado hazijajiunga kushirikiana na jumuiya
hiyo ili kusaidiana kupata nguvu za pamoja zitakazosaidia kutatua baadhi
ya changamoto zinazowakabili.
“
Skuli binafsi pia zinapaswa kupongezwa kwa mchango unazotoa wa kuiunga
mkono Serikali kutoa elimu bora bila ya ubaguzi. Skuli hizi zimeisaidia
sana Serikali kuwapatia ajira Raia wa Nchi hii pamoja na kuipunguzia
mzigo mkubwa Serikali wa mrundikano wa wanafunzi katika skuli nyingi
Nchini “ Alisema Balozi Seif.

Katika
kuunga mkono jitihada za Walimu Wakuu hao wa Skuli za Sekondari
Zanzibar za Kuunda Jumuiya yao Balozi Seif alichangia shilingi Laki
500,000/- kusaidia mkutano huo pamoja na kuahidi kusaidia Kompyuta moja
na Mashine moja ya Foko Kopi kwa ajili ya Ofisi ya Jumuiya hiyo.
Aidha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wana jumuiya hiyo kwamba
atawasiliana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini katika
kuangalia uwezekano wa kuipatia Jumuiya hiyo eneo la kujenga Ofisi yake
pamoja na kupatiwa hati miliki za maeneo yote ya Skuli za Serikali.
Akisoma
Risala ya Wanajumiya hiyo ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari
Zanzibar Katibu wa Jumuiya Hiyo Maalim Fadhil Hamada Mshamba alisema
lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwaunganisha walimu wa Serikali
na Binafsi ili kuwa na sauti moja katika kuwafinyaga vyema watoto
kielimu.
Maalim
Fadhil alisema wanajumiya hiyo hivi sasa wanajivunia mafanikio makubwa
waliyoyapata tokea kuanzishwa kwake mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na
kurejea kwa nidhamu katika maskuli mengi nchini, utunzaji wa mazingira
pamoja na taaluma ya kuepuka taathira mbaya za ajira kwa watoto.
Katibu
Mkuu huyo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar
alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kuwa ni
pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo ya Skuli, upungufu wa samani,
ukosefu wa vyombo vya usafiri kwa walimu Wakuu pamoja na uvamizi wa
maeneo ya Maskuli kwa kujengwa nyumba za kudumu za watu binafsi.
Mapema
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Mwanaid
Saleh alisema Wizara hiyo inaendelea na tathmini ya kupanga vigezo
mbali mbali vitakavyotoa fursa kwa walimu kupanda daraja kwa mujibu wa
Taaluma wanazozipata.
Mada
mbali mbali zinajadiliwa katika Mkutano huo wa Siku Tatu wa Jumuiya ya
Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar ukihitimishwa na uchaguzi
Mkuu wa kuwachaguwa Viongozi wake wapya.
Miongoni
mwa mada zitakazojadiliwa katika Mkutano huo kuwa ni pamoja Maendeleo
na mafanikio ya elimu katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2006 pamoja na changamoto zake,
pamoja na Utawala wa Mwalimu Mkuu na utekelezaji wa majukumu .
Nyengine
ni Mchango wa Skuli Binafsi katika kuleta maendeleo ya Elimu Zanzibar,
usimamizi wa Mwalimu Mkuu katika somo la Hesabu pamoja na muelekeo Mpya
wa tathmini ya mwanafunzi ndani ya Zanzibar.
Mkutano
Mkuu huo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar
umepata baraka ya kuhudhuriwa pia na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya
Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Tanzania Bara (TAHOSSA)
Ujumbe
wa mwaka huu wa Mkutano huo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za
Sekondari Zanzibar { JUWASEZA } ni Muelekeo mpya wa Tathmini ya
Mwanafunzi Zanzibar.








0 comments:
Post a Comment