Tuesday, November 19, 2013

Utatu wa Kenya, Rwanda na Uganda watinga kortini

WATU watatu wamewasilisha ombi kutaka Mahakama ya Afrika Mashariki  isitishe uamuzi uliopitishwa katika vikao vitatu vilivyofanyika Uganda, Rwanda na Kenya wakidai vimekiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Vikao hivyo viliofanyika Entebe,  Uganda, Kigali , Rwanda na Mombasa , Kenya . Walalamikaji wameomba mahakama ionye nchi  husika ambazo ni Rwanda, Uganda na Kenya zisirudie kosa.
Waliofungua kesi ni Ally Msangi, David Mataka na John Bwenda, ambao wamewasilisha maombi hayo kupitia Wakili Mwandamizi, Jimmy Obed wa Kampuni ya Uwakili ya Jimmy Obed ya Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuwasilisha maombi hayo kwenye ofisi ya Masijala ya
Mahakama ya Afrika Mashariki Jijini Arusha na kupokewa na Ofisa Masijala, Boniface Ogotu, Jimmy alidai wanataka mahakama itamke kuhusu kuheshimu mkataba uliopo .
Alidai Rwanda, Uganda na Kenya wamekiuka mkataba wa Jumuiya hiyo kupitia vikao walivyofanya Juni 24 na 25 mwaka huu Entebe, Uganda.
Wanadai vikao vingine vilivyofanyika kinyume na mkataba ni vya Agosti 28 mwaka huu Mombasa,  Kenya na Oktoba 28 mwaka huu Kigali, Rwanda.
Alidai katika vikao hivyo walitoa uamuzi ambao unatakiwa kutekelezwa, na kwamba wamevunja Ibara ya 71(F), 71(D) na Ibara ya 12 kifungu cha 3 (3)c, Ibara ya 6 (a), (b), (d) na (f) na ibara ya 8 (1) c na 8 (3)c.
"Wadai wanataka Mahakama hii ifanyie kazi vizuri maombi haya na kutoa amri ya kuzuia kufanyika kwa utekelezaji wa uamuzi uliopitishwa kwenye vikao hivyo na kuwaamuru wasirudie kukiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki''.
Alidai wajibu maombi katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Uganda na Rwanda. 

0 comments:

Post a Comment