Monday, November 25, 2013

Bonex mkombozi wa janga la moto nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Simba Logistic and Equipment Fareed Nahdi akirusha kifaa cha Bonex katika moto kwa ajili ya kuzima moto uliowashwa wakati wa uzinduzi wa kifaa hicho.




Mtoto akionesha namna ya kutumia kifaa hicho kuzimia moto.


Kamishna wa kikosi cha zimamoto Rogatius Kipali akizima moto katika kuonesha ubora wa kifaa hicho.
Meneja Mradi wa teknolojia ya Bonex Lura Lyabandi akiwafafanulia wageni.



TEKNOLOJIA ya aina mbalimbali zinazidi kukua na kusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua kero mbalimbali hapa nchini.

Katika jiji la Dar es salaam kama majiji mengine nchini kero kubwa mojawapo ni upatikanaji wa utatuzi wa haraka wa kukabiliana na janga la moto.

Kutokana na miundombinu mibovu ya barabara ya jiji hili kikosi cha zima moto kimekuwa kikikumbana na kero kubwa ya kufika haraka katika maeneo mbalimbali ambapo moto unawaka.

Mbali na barabara kuwa ni kikwazo kikubwa lakini pia kerokubwa ni mkusanyiko wa nyumba nyingi katika eneo moja yaani unakuta kuna maeneo ambapo gari haliwezi kufika kutokana na mkusanyiko wa nyumba.

Hali hiyo inapelekea nyumba nyingi kuungua moto na kupelekea upotevu wa mali nyingi za watu kwa kuwa moto ukizuka kwenye nyumba moja na kushindwa kuzuiliwa mapema basi unaunguza na nyumba za jirani.
Katika kukabiliana na hali hiyo kumekuwa na mikakati mbalimbali ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kupitia kikosi cha usalama barabarani imekuwa ikiendesha mafunzo ya aina mbalimbali ya kuzuia moto.

Mafunzo hayo yamesaidia kikosi hicho katika kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto lakini hata hivyo imekuwa ni shida katika maeneo yasiyofikika kiurahisi na haraka.

Katika kukabiliana na janga kampuni ya Simba Logistic Equipment Co Ltd imezindua kifaa kipya kiitwacho Bonex ambacho kinabebeka kirahisi.

Kifaa hicho inaonekana kuwa  ni teknolojia mpya ambayo inalenga kusaidia kutatua kero ya muda mrefu ya kutabiliana na janga la moto.

Kifaa ni cha kurusha ambapo iwapo moto umezuka ghafla sehemu kinachotakiwa kufanyika ni kuchukua kifaa hicho na kisha kukitupa katike eneo ambalo moto umewaka.

Bonex ni chupa ambayo ni ya plastic ambayo ndani yake ina kimiminika chenye kemikali hiyo ya kuzima moto kwa kiwango kikubwa.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Fareed Nahdi anasema kuwa kifaa hicho kinalenga kusaidia utoaji wa huduma ya uzimaji moto kwa urahisi zaidi.
Anasema kuwa ni rahidi kutumia kwa kuwa ni kifaa cha kurusha tu katika moto na kisha kinazima moto.

"Najua ukilinganisha na teknolojia nyingine inavyofanya kazi hii ni tofauti kwa kuwa vifaa vingine unatakiwa kufuata taratibu ambazo ni ndefu kidogo kwanza ujue namna ya kuvifungua na kisha ndio kuelekeza kwenye  moto tena kwa kuwa umesogelea" alisema Nahdi.

Alisema kuwa pia inatakiwa kufanyiwa kwanza mafunzo ya kuelekezwa namna ya kutumia lakini hiki unarusha tu kwenye moto na kinazima kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Kamishna wa kikosi cha Zimamoto Tanzania, Rogatius Kipali anasema kuwa ofisi yake inatambua juhudi zinazofanywa na wadau wengine mbalimbali katika kukabiliana na janga la moto.

Anasema kwa mfano mzuri  ni kifaa hicho ambacho hata mama wa nyumbani anaweza kukitumia kuzimia moto iwapo imetokea katika mazingira ya nyumba yake.

" Najua ndio kuzima moto ni kazi yetu lakini ikumbukwe kuwa pale unapotokea kunatakiwa kuwe na hatua za awali za kufuatwa katika kuuzima na ndio hivyo hivyo ambavyo hawa watu wa Simba Logistic wamekuja na kifaa hichi muhimu"anasema Kipali.

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mohamed Mpinga anasema kuwa kifaa hicho kinaweza kusaidia kuzuia ajali za moto katika magari kwa kuwa ni rahisi kutumia.

Kwa upande wetu kikosi cha usalama barabarani tunaona kuwa kifaa hiki pia ni mkombozi kwa kuwa kwanza hakihitaji ukarabati kama vifaa vingine vya kuzimia moto"anasema Mpinga.




0 comments:

Post a Comment