Thursday, February 28, 2013

WAKAMATWA WAKIUZA NYAMA YA FISI

WATU wawili akiwemo Mwenyekiti wa kitongoji cha Ihumwa Kata ya Mtumba katika Manispaa ya Dodoma wamekutwa wakiuza nyama ya fisi kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.
Wanaotuhumiwa kuuza nyama hiyo ya fisi ni Gabriel Mwaluko ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji na Dickson Mafutaa aliyekuwa akishirikiana na mwenyekiti huyo kuuza ‘kitoweo’ hicho.
Kukamatwa kwa watu hao kunatokana na  taarifa za wananchi zaidi ya 10 walionunua  na kula nyama hiyo na kuwa na wasiwasi kutokana na kuuzwa kwa bei rahisi hali ambayo ilifanya wafikishe taarifa hiyo kwa Ofisa Afya.
Akizungumzia tukio hilo  la  Jumatatu mchana, Ofisa Afya wa Kata ya Mtumba,  Michael Dong’o alisema mwenyekiti huyo alikutwa akiwa ameweka nyama hiyo kwenye mifuko ya rambo na kuiuza kati ya Sh 500 hadi Sh 1,000 kwa kipande kimoja.
Dong’o alisema baada ya kumuhoji Mwenyekiti  huyo, alisema nyama waliyokuwa wakiuza ilitokana na fisi waliyemuua kutoka kwenye pori la Ihumwa.
Alisema waliamua kumchuna na kisha kukata vipande vya nyama hiyo na kisha kupeleka kwenye kilabu cha pombe za kienyeji kwa ajili ya kuuza.
Kwa mujibu wa ofisa afya, watuhumiwa hao walikiri kuuza nyama ya fisi na wakati huo huo inadaiwa walikutwa na ngozi ya mnyama huyo ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa plastiki.
Ofisa Afya anadai mwenyekiti huyo wa kitongoji alisema kuwa licha ya kuuza nyama hiyo kilabuni, pia familia yake ilipata.
 Afisa afya aliwataka wakazi wa maeneo ya kuwa makini kwa kujihadhari  na kula nyma zilizothibitishwa na wataalamu wa afya.
Alisema ni vizuri kwa wananchi kuacha uchu wa kula nyama hasa  zinazouzwa kwenye vilabu vya pombe vya kienyeji kuepuka magonjwa hatari yanayoweza kusababishwa na nyama.
Kulingana na maelezo ya ofisa afya, wanakusudia kuwafungulia watuhumiwa hao mashitaka polisi  kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hata uhalali wa kuwa na nyama na ngozi ya fisi.


0 comments:

Post a Comment