Thursday, February 28, 2013

WATANZANIA WANAKULA KILO 12 TU YA NYAMA KWA MWAKA BADALA YA KILO 50

Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi , Wizara hiyo, Benedict Ole Nangoro, amesema utafiti umebaini ulaji wa nyama kwa mtanzania ni wastani wa kilo 12 kwa mwaka tofauti na kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa wa ulaji wa Kilo 50 kwa mtu kwa mwaka. 
Akifungua mkutano wa tano wa Baraza la Mwaka la wadau wa tansia ya nyama nchini jana, Naibu Waziri alisema alisema pia  uzalishaji wa nyama katika machinjio na sehemu ya kuuzia ni duni na hivyo kusababisha kupoteza soko maalumu la ndani na kulazimu Serikali kuagiza nyama kutoka nje ya nchi.
Akielezea kiwango cha ulaji nyama nchini, Nangoro alisema utafiti umebaini  licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo , ulaji  nyama kwa wananchi  wake ni wa kiwango cha chini.
Kwa mujibu wa naibu waziri, katika    kipindi cha Januari na Februari mwaka huu , nyama iliyoingizwa nchini ni tani 192 za ng’ombe , 8.2  Kondoo na tani 48.5 za nyama ya nguruwe; thamani ya tani hizo ni takribani sh bilioni 1.3.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kinachosikitishwa zaidi ni ukweli kwamba sehemu kubwa ya nyama hiyo inatokana na mifugo inayozalishwa hapa nchini.
 “ Mifugo hii inasafirishwa kwenda nchi jirani kwa njia zisizo halali na baadaye kusindikwa na kurudishwa nchini kama nyama iliyoangizwa toka nje ya nchi na kuuzwa kwa bei kubwa,” alisema.

0 comments:

Post a Comment