
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki akitoa taarifa ya kikao cha
kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO,Dar es salaam.
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Jumla
ya kata 22 katika manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke zitaingizwa
katika mpango wa utengaji wa maeneo maalum (smart area) kwa ajili ya
kuboresha usafi wa mazingira jijini Dar es salaam.
Akitoa
taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es salaam (RCC)
leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck
Sadiki amesema uanzishaji wa maeneo maalum ya usafi wa mazingira
unalenga kuondoa shughuli zote zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya
jiji kinyume cha sheria na kulifanya jiji la Dar es salaam kuendelea
kuwa katika hali isiyoridhisha ya usafi wa mazingira.
Amesema
utekelezaji wa mpango huo wa utengaji wa maeneo maalum unazingatia
sheria ya mipango miji Na. 8 ya mwaka 2007 na sheria ya mazingira Na. 20
ya mwaka 2004 na kuzitaja kata zitakazohusika katika mpango huo kuwa
ni pamoja Keko, Chang’ombe, Kurasini, Mibulani , Sandali na kata ya
Gerezani zote za manispaa ya Temeke.
Kata
nyingine ni Mchafukoge, Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, Kisutu,
Kivukoni,Upanga Mashariki na Upanga Magharibi ambazo ziko manispaa ya
Ilala na kata za Hananasif, Kinondoni, Kigogo, Mzimuni na Magomeni zote
za manispaa ya Kinondoni.
Amesema
kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo hatua mbalimbali
zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa shughuli zote zinazosababisha
kero katika eneo husika, biashara zisizo rasmi, biashara za vyakula,
uchomaji nyama na mahindi kando kando ya barabara na maeneo ya watembea
kwa miguu, uondoaji wa gereji bubu, maguta, mikokoteni bajaji na
bodaboda katikati ya jiji.
Shughuli
nyingine zitakazofanyika ni zile za uondoaji wa malori makubwa yenye
zaidi ya tani 10 katika maeneo yasiyoruhusiwa na kubainisha halmashauri
zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hizo.
“Halmashauri
zetu zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli zote
tulizoziainisha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi japo kuna
maeneo tuliyoyatenga kwa wananchi hayatumiki na baadhi ya wahusika
hawako tayari kwenda kwenye maeneo hayo” amesema.
Kuhusu
waendesha bodaboda na bajaji kuendelea kuingia katika maeneo
yasiyoruhusiwa hususani katikati ya jiji la Dar es salaam amesema kuwa
serikali haitalifumbia macho suala hilo kwa kuwa liko kisheria.
Amesema
watekelezaji wa sheria ya SUMATRA ya kuhifadhi maeneo yaliyotengwa
wanaendelea na zoezi la kuwaondoa wote wanaovunja sheria hiyo na kutoa
wito kwa wahusika wa zoezi hilo kuliendesha kwa kufuata sheria, taratibu
na kuzingatia utu na haki za binadamu.
“Nimeshatoa
maagizo kwa watendaji na viongozi wanaosimamia zoezi hili wahakikishe
wanaheshimu utu na haki za binadamu, kama ni kampuni ikigundulika
tutaifungia isipate tenda zozote za serikali, nachosema wahusika wawe
makini serikali hatutawavumilia wanaoendesha vitendo vya hujuma, uonevu,
wizi, uporaji na ukiukaji wa haki za binadamu” Amesisitiza.
Aidha
ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaa licha ya kukabiliwa na changamoto ya
ufinyu wa bajeti unaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zenye tija
kwa maendeleo ya wananchi zikiwemo Elimu, Afya, ujenzi na ukarabati wa
barabara, madaraja na miundombinu mingine ya jiji ambayo imeharibiwa na
mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema
katika kuimarisha huduma za afya mkoa kupitia kamati ya ushauri ya mkoa
(RCC) imepitisha maombi maalum ya zaidi ya shilingi bilioni 45 nje ya
bajeti ili kukabiliana na tatizo la msongamano mkubwa wa wagonjwa wa nje
na wale wanaolazwa katika hospitali za mkoa wa Dar es salaam.
Amesema
kuwa mkoa wake unapata wagonjwa wengi wa nje kutoka maeneo mbalimbali
yakiwemo ya Kisarawe, Mkuranga, Mafia, wilaya ya Bagamoyo,Kibaha na
Chalinze jambo linaloongeza mzigo kwa hospitali za mkoa huo.
“Mkoa
wa wetu wa Dar es salaa una idadi kubwa ya watu kuliko mikoa mingine
nchini pia unahudumia watu wengine wengi kutoka maeneo mbalimbali, jambo
hili linaongeza mzigo kwa hospitali zetu kutokana na kuwahudumia
wananchi kutoka nje ya mkoa” Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa wagonjwa wa nje sasa wanafikia 1500 hadi 2000 kwa siku jambo
linalowafanya kuomba fedha zaidi kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa
hospitali za rufaa za mkoa na ujenzi wa hospitali maalum kwa ajili ya
mama na motto itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 600 kwa wakati
mmoja.
Katika
hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki
ameeleza kuwa mkoa wake una dhamira ya kuongeza maeneo mapya ya utawala
kwa kuongeza kata 113 na mitaa 570 pamoja na kupitia mapendekezo
yaliyowasilishwa kwenye kikao Maalum cha kamati ya ushauri ya mkoa
na mabaraza ya madiwani ya halmashauri husika kuhusu kuugawa mkoa wa
Dar es salaam katika muundo wa wilaya 5.
Amesema kuwa wilaya zilizopendekezwa ni pamoja na Ilala, Kinondoni, Temeke, wilaya ya Kigamboni na wilaya ya Ubungo.
0 comments:
Post a Comment