Wednesday, February 12, 2014

Soma kauli ya Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara Kuhusu Mashine za TRA (EFD)



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAULI YA WAZIRI KIVULI WA VIWANDA NA BIASHARA KUHUSU EFD
Tangu mwishoni mwa mwaka jana, mwezi Novemba na mapema mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali hususan kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekuwa kwenye mgogoro mkubwa na wafanyabiashara kuhusu matumizi ya vifaa vya kielektroniki kwa ajili ya kutoza na kukusanyia kodi (EFD).
Mgogoro huo umekuwa mkubwa kiasi kwamba wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali ya nchi, kupitia katika jumuiya zao, waliamua kufanya maandamano na kufunga maduka yao kama moja ya njia za kuwasilisha madai yao serikalini ili yaweze kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa madai ya wafanyabiashara hao dhidi ya serikali ni pamoja na;
·        Elimu juu ya matumizi ya EFD, hali ambayo inaonesha hakukuwa na maandalizi wala ushirikishwaji wa wadau wote katika suala hilo muhimu.
·        Kuwepo kwa hali ya kulazimishwa kwa watu wasiohusika kwa maana ya wafanyabiashara wenye mitaji midogo ukilinganisha na gharama za kununua na kuendesha mashine hizo.
·        Bei kubwa ya kununulia na kuendesha mashine hizo, ambayo inasababishwa na upatikanaji wake ikidaiwa kuwa kuna msambazaji mmoja tu.
Ndugu wanahabari
Kama mnavyojua, suala hili ni mtambuka. Linahusisha sekta nyingi na zaidi ya wizara moja. Wizara mama ya wafanyabiashara nchini ni Wizara ya Viwanda na Biashara huku suala la matumizi ya EFD likiwa chini ya Mamlaka ya Mapato (TRA) iliyoko chini ya Wizara ya Fedha na Uchumi.
Wizara zote hizo mbili hadi sasa zimeshindwa kutoa suluhisho katika mgogoro huu ambao sasa unaanza kutishia mzunguko wa uchumi na bila shaka kama utaendele namna hii unaweza kusababisha mfumuko wa bei ambapo hatimaye mwathirika atakuwa ni mwananchi wa kawaida au mtumiaji wa mwisho wa bidhaa na huduma za wahusika wote katika sakata hili.
Kutokana na ukweli kwamba wizara zote hizo mbili zimeshindwa kutoa majawabu ya kumaliza kabisa kadhia hiyo inayoendelea kati ya wafanyabiashara na TRA, tunataka mambo kadhaa yafanyike.
·        Kwa hatua ambayo mgogoro huu umefikia na namna unavyochukua sura mpya kila siku, sasa serikali itambue kwamba hili tayari ni tatizo ambalo linahitaji suluhisho na majawabu sahihi.
·        Serikali iache kutumia mabavu, vitisho vya kutumia polisi na kauli za kejeli katika kushughulikia tatizo hilo, hasa kupitia kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.
·        Serikali iweke wazi mchakato uliotumika kumpata muuzaji na msambazaji wa hizo mashine za EFD.
·        Serikali iweke wazi mkataba uliopo kati yake na muuzaji/ msambazaji wa mashine za EFD.
·        Serikali, kupitia Ofisi ya Rais (Ikulu), itoe ufafanuzi wa namna ambavyo madai hayo ya wafanyabiashara yatafanyiwa kazi ili shughuli za uuzaji, uzalishaji na utoaji huduma ambayo ni sehemu ya mzunguko wa uchumi, ziendelee huku kila mtu akitimiza wajibu wake, kwa maana ya mtoa kodi, mkusanya kodi na mtoza kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Tunaitaka ikulu ijitokeze kumaliza mgogoro huu kwa sababu tayari suala hilo limefika huko baada ya wafanyabiashara wenyewe kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete aingilie kati kusaidia kuondoa utata.
Kuna umuhimu wa Rais Kikwete kuwaambia Watanzania hatima ya tatizo hilo kwa sababu kimantiki, wafanyabiashara wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya wizara zote mbili kuishia kutoa ahadi na matumaini hewa ya kushughulikia lakini hakuna kitu chochote kinachoendelea.
Tunatambua umuhimu wa kuwepo na mfumo mzuri utakaohakikisha kuwa kila mtu anayestahili kulipa kodi anafanya hivyo kadri ya kanuni za ulipaji kodi zilivyo, hivyo hatuwezi kukubali kuwepo mianya yoyote yoyote ile ya watu kukwepa kodi. Tumelisema hili mara kadhaa na tutaendelea kusisitiza.
Pamoja na kusisitiza umuhimu wa ulipaji kodi, tutaendelea pia kuhoji busara inayotumika kuweka ‘vihunzi’ vingi sana kwa makundi fulani ya walipa kodi, huku serikali hiyo hiyo ikiendelea kutoa mianya ya kukwepa kodi au kutoa misamaha mikubwa ya kodi kwa wafanyabiashara au wawekezaji wakubwa kiasi hata cha kuathiri ukuaji wa pato la taifa na ustawi wa uchumi wetu.
Mbali ya kuitaka Serikali, kupitia Ikulu kuingilia kati mzozo huu wa sasa, pia kupitia taarifa hii tunaitaka ifanyie kazi madai yote ya wadau mbalimbali katika sekta ya biashara ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu sasa na CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani, kupitia Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiyasema mara kwa mara, kupitia kwenye hotuba za Waziri Kivuli au hoja za wabunge wake.
Tunasema hivyo kwa sababu mgogoro huu wa mashine za EFD ni dalili tu ya tatizo au matatizo ya msingi ambayo hayatafutiwi majawabu ya kudumu. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa nchi hii inatoa fursa nzuri kwa ajili ya watu wake kuzalisha na kufanya biashara yenye tija kwa wauzaji na wanunuzi kwa ajili ya uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.
Imetolewa leo Februari 12, Dar es Salaam na;
Hyness Kiwia (MB)
Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara


0 comments:

Post a Comment