Thursday, December 19, 2013

Soma taarifa ya Mamlaka ya usafiri wa Anga kuhusiana na ndege iliyotua Uwanja wa Ndege wa Arusha badala ya KIA


Kutokana na taarifa hiyo hapo juu kutoonekana vizuri nimeandika hapo chini


TUKIO LA NDEGE AINA YA BOEING 767-300 MALI YA ETHIOPIAN AIRLINES ILIYOTUA KWENYE UWANJA WA NDEGE WA ARUSHA BADALA YA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA KILIMANJARO (KIA) TAREHE 18/12/2013
Jana majira ya 12:47 mchana, Ndege ya Shirika la Ethiopia aina ya Boeing 767-300 yenye injini mbili na uwezo wa kubeba abiria 260 ilitua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Arusha badala ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ilipotarajiwa kutua.
Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Addis Ababa, Ethiopia ikielekea Kilimanjaro na Mombasa, ilitegemea kutua Uwanja wa Ndege wa KImataifa wa Kilimanjaro (KIA) saa 6:55 mchana katika safari yake ya kawaida, ilikuwa n ajumla ya watu 213 (Abiria, rubani na wahudumu wa ndege).
Mawasiliano ya kwanza ya ndege na Uwanja wa KImataifa wa Kilimanjaro yalikuwa ni saa 6:29 mchana ambapo rubani alisema ametoka Addis Ababa, Ethiopia kwenda Kilimanjaro aliruka futi 36,000 kutoka usawa wa bahari na alitegemea kutua KIA saa 6:50 mchana.
Muongoza ndege alimwelekeza rubani njia ya kufuata kuelekea KIA hadi atakapouona uwanja na kisha kutua barabara namba 27 (Runway 27). Rubani pia alipewa tahadhari kuwa kuna ndege ndogo imekwama mwanzo mwa barabara namba 09 (Runway 09) kutokana na tatizo la kupata pancha na barabara iliyopo ni namba 27 yenye urefu wa meta 3,200 ambazo zinaweza kutumika.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, rubani alijibu na kusema atamwita tena baada ya kuachiwa na Nairobi. Baada ya muda mfupi, rubani aliita tena KIA na kuripoti kuwa ameachiwa na Nairobi na anaomba kuendelea kuteremka. Muongoza ndege wa KIA alimruhusu kuendelea kushuka hadi hatimaye kufikia futi 7,000.
Baada ya muda rubani akaripoti kwamba, amekiona kiwanja na anaomba aendelee kutua kwa macho (visiual approach) barabara namba 27. Rubani aliruhusiwa kuendelea kutua kwa kuona na aliripoti akiwa upande wa kushoto wa barabara namba 27.
Baadae rubani aliita tena na kuripoti kwamba yuko upande wa kushoto wa barabara namba 27 na anaiona barabara ya ndege namba 27. Wakati wote alikuwa kwenye masafa ya KIA (120.1MHz) na hali ya hewa kwa wakati wote ilikuwa nzuri. Baada ya hapo muongoza ndege wa KIA alimruhusu kutua barabara namba 27. Baada ya kutomuona akitua muongoza ndege wa KIA alianza kuita bila mafanikio. Wakati muongoza ndege wa KIA akiendelea kuita ndege hiyo, alipigiwa simu na muongoza ndege wa Arusha kumtaarifu kuwa anaiona ndege aina ya BOEING inatua barabara namba 27 Arusha.
Hakuna taarifa ya tahadhari iliyotolewa na marubani wa ndege hiyo ya Ethiopia ET 815, kabla ya kutua uwanja wa Arusha. Aidha uwanja wa ndege wa KIA alikuwa unaruhusu ndege hiyo kutua licha ya ndege ndogo kukwama mwanzoni mwa barabara ya 09  (Runway 09) kwa vile bado ilikuwa na barabara yenye urefu wa meta 3,200 ambazo zingeweza kutumika.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inashirikiana na Kitengo cha Usimamizi wa Ajali, Wizara ya Uchukuzi, kubaini chanzo cha tukio hilo. Tayari timu ya wataalamu iko eneo la tukio, hivyo taarifa zaidi zitatolewa uchunguzi utakapokamilika.

0 comments:

Post a Comment