Monday, December 9, 2013

Picha ya mwisho ya Mandela yaoneshwa

PICHA ya mwisho ya Kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela akiwa hai imetolewa akionekana mwenye tabasamu huku ameshika mkono wa kitukuu chake.

Picha hiyo ilipigwa Mei nyumbani kwake Houghton jijini Johannesburg akiwa amekaa kwenye kiti alichokipenda sana –mwezi mmoja kabla hajalazwa hospitalini jijini humo.

Kwa familia ya Mandela picha hiyo inabaki kuwa kumbukumbu nzuri za nyakati za furaha. Na kwa mtoto wa miaka mitatu, Lewanika, ambaye anaonekana kwenye picha hiyo, itakuwa ni kumbukumbu ya aina yake, anasema baba yake, aliyeipiga, akiongeza kuwa kitakuwa ni kitu ambacho ni hazina kwake atakapokuwa amekua kiasi cha kuweza kuelewa mambo.
Ni taswira ya mwisho ya mtu wa kihistoria ambaye Waafrika Kusini na walimwengu duniani wanamwomboleza-huku pia wakisherehekea urithi aliowaachia wa amani, mtu mashuhuri ambaye karama zake zitahisiwa na kila mtu duniani hata katika miaka ijayo.
Picha hiyo inamwonesha Lewanika akiwa amekaa kwenye mkono wa kiti, huku akimwangalia kwa udadisi mkubwa babu yake, mtu ambaye amekuja kuwa alama ya nchi yake, katika mapambano dhidi ya maovu, lakini ambaye pia mtoto huyo alizoea kumwita ‘baba’.
Akihojiwa jana na The Mail on Sunday la Uingereza, baba yake Lewanika, Ndaba Mandela-ambaye ni mjukuu wa Mandela-alisema alipiga picha hiyo akiamini kuwa huenda ikawa ni fursa yake ya mwisho kuwapiga picha wawili hao wakiwa pamoja.
“Ilikuwa Mei, Jumamosi moja mchana. Tulikuwa tumekuja kumjulia hali mzee huyo na tukamkuta akiangalia kipindi cha National Geographic kwenye televisheni, “Ndaba (30) alisema.
“Alimwangalia Lewanika na kumwita, “njoo, njoo.” Uso wa mzee ulijawa nuru alipomwona-kama ujuavyo alipenda sana watoto. Walikumbatiana na mwanangu akamwita “baba”. Ilinigusa sana kuwaona wawili hao wakiwa pamoja.”
Ndaba ambaye ni Mwenyekiti wa Wakfu wa Africa Rising ambayo inashughulikia maendeleo ya uchumi wa vijana wa Afrika Kusini, anaishi katika nyumba ya Mandela ya Houghton, ambako ndiko mzee huyo alifia Alhamisi.
Ndaba alisema: “Tunajivuna kwamba tumeweza kutunza kumbukumbu hii maalumu na kupata heshima ya kuionesha dunia.”
Alipenda watoto
Binti wa Mandela, Zindzi (53) naye aliiambia The Mail on Sunday mapema mwaka huu jinsi baba yake alivyopenda kuwa na watoto na vijana karibu naye. Anakumbuka simulizi ya jinsi alivyotoka gerezani, alipomwomba aache kumnyonyesha mwanawe wa kiume ili akae na mtoto huyo chumbani kwake, amlishe na kumlea kila usiku.
Zindzi alisema wakati fulani:”Baba hufurahi sana anapoona watoto wamemzunguka. Anawapenda na hufurahi wakimpandapanda.”
Picha hii ilitoka wakati Mandela akisumbuliwa na maambukizi sugu ya mapafu yaliyogundulika akiwa gerezani alipotengwa na kuwekwa kwa miezi kadhaa akiwa ndani ya rumande yenye giza.
Hali yake ilibadilika ghafla mapema wiki jana, wakati binti yake mkubwa Makaziwe, aliyezaliwa katika ndoa yake ya kwanza, aliposimulia uchungu wake alipomwona baba yake akiwa “katika kitanda chake cha mauti.”
Jana Ndaba, akiwa mwana familia wa kwanza kuzungumza tangu Mandela afariki dunia, alielezea masikitiko yake makubwa, lakini akaongeza:”Kuna hisia za faraja pia, kwamba hatimaye yuko mahali pema zaidi. Ni faraja kutambua kuwa mamilioni kwa mamilioni ya watu duniani wako nasi katika majonzi haya. Nimeona maua yote nje ya nyumba, haiaminiki.”
Kuhusu picha hiyo, Ndaba aliongeza: “Siku moja nitamwambia mwanangu Lewanika juu ya babu yake huyu alivyokuwa maarufu na picha hii itakuwa maalumu kwake.”
Alikumbuka, kwamba Mandela alikuwa amekaa kwenye kiti chake katika chumba cha kupumzika nyumbani kwake, huku amezingirwa na vitabu na picha alizopewa kama zawadi, alipompeleka mwanawe huyo. 
Kuna wakati madaktari walikuwa na wasiwasi na afya yake hasa kutokana na moyo wake kuzidi kudhoofu; mikono yake iliyovimba kutokana na tatizo hilo, vyote vinaonekana kwenye picha hiyo.
Baada ya wiki kadhaa alizidiwa usiku wa manane na kukimbizwa katika hospitali ya moyo jijini Pretoria ambako alilazwa kwa miezi mitatu. Katika picha hiyo Mandela anaonekana mwenye furaha kwa kuwa na kitukuu chake.
“Alipozaliwa nilimwuliza mzee tumwite jina gani,” Ndaba anakumbuka. “Na babu yangu akapendekeza jina la Ngubencuka ambalo ni la mmoja wa wahenga wetu. Nalazimika kusema nilikuwa tayari nina jina la Lewanika lakini tukampa jina la katikati la Ngubencuka.”
Ndaba alikuwa Brazil akiwakilisha nchi yake katika kura za ratiba ya fainali za soka Kombe la Dunia aliposikia taarifa za kifo cha babu yake. “Ndio nilikuwa nimewasili katika eneo la shughuli mara nikapigiwa simu na shangazi. Tulirudi nyumbani mara moja.”
Alisema takribani asilimia 90 ya familia tulikusanyika nyumbani kwa Mandela katika barabara inayopambwa na miti ya mijakaranda katika kitongoji cha watu matajiri.
“Ni majonzi lakini kila mmoja alikuwa akijishughulisha kulisha ndugu na kuandaa mambo mbalimbali. Tulikuwa na chakula cha pamoja leo (jana) jambo ambalo ni jema.”
Miongoni mwa watu walioshinda nyumbani hapo ni mke wa pili wa Mandela, Winnie. Mke wa tatu Graca Machel alikuwa pembeni mwa kitanda wakati anakata roho Alhamisi, pamoja na wajukuu wake kadhaa na wazee wa kimila wa jamii ya Waxhosa. Walijumuika pia na Mchungaji ambaye alifanya maombi ya mwisho kwa mzee.
Mandela alikuwa na watoto sita, watatu walishatangulia mbele za haki. Mmoja alikuwa ni wa kiume Makgatho Lewanika Mandela, ambaye alifariki dunia kwa Ukimwi mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 55. Mjukuu wa Makgatho-aliye na Mandela kwenye picha hiyo- alipewa jina la kati la babu yake huyo.
Kwa jumla kuna wajukuu 17 na vitukuu 13. Zenani ambaye ni binti wa mjukuu wa Mandela, Zoleka, alifariki dunia katika ajali ya gari siku ya mkesha wa uzinduzi wa sherehe za fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini. Alikuwa na umri wa miaka 13.
Ndaba alisema: “Sisi ni familia kubwa na tutakuwa hapa kwa siku chache zijazo. Tukio kubwa litakuwa ni sherehe za kumbukumbu ya Mandela Jumanne. Kwa maziko ya Jumapili, nina uhakika kutakuwa na wakuu kadhaa wa serikali za dunia.
“Najua Obama (Barack-Rais wa Marekani) alisema anataka kuja na Rais wa Ufaransa anataka kuja pia, na viongozi mbalimbali wa Afrika. Sijasikia ni nani anakuja kutoka Uingereza”.
Hata hivyo, habari kutoka Uingereza zilisema Malkia Elizabeth II hatahudhuria maziko ya Mandela kutokana na ushauri wa madaktari apunguze safari ndefu kutokana na afya yake. Mwanawe, Prince Charles atamwakilisha.
Malkia badala yake anatarajiwa kutoa heshima zake katika Misa maalumu itakayofanyika kwenye Kanisa la Westminster Abbey, London, Uingereza.

0 comments:

Post a Comment