Monday, December 9, 2013

Aliyemuona Mandela dakika 90 kabla ya kifo asimulia

 Nelson Mandela: The  first democratically elected president of South Africa had repeatedly been hospitalised with lung troubles in recent years. Photograph:  Camera Press/ Yousuf Karsh
DAKIKA za mwisho za maisha yake, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, hakuwa akitumia mashine ya kumsaidia kupumua.
Mmoja wa wanafamilia wa Mandela, Bantu Holomisa, aliyemuona kiongozi huyo dakika 90 kabla ya kifo chake, ameripotiwa akisema alikuwa akipumua bila msaada wa mashine hiyo na alikuwa amezungukwa na wanafamilia wa karibu.
 "Wakati anafariki Alhamisi iliyopita usiku, hakuwa akitumia msaada wa mashine kupumua, alikuwa akipumua bila mashine hiyo,” alisisitiza mtoa taarifa aliyenukuliwa na gazeti la kila wiki la Sunday Times.
Mandela aliyekuwa akisumbuliwa na mapafu, amekuwa akilazwa mara kwa mara kutokana na matatizo hayo na ni mara chache alikuwa akilazimika kutumia mashine ya kumsaidia kupumua.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times, Mjukuu wa Mandela, Mandla aliitwa kwa dharura kutoka katika kijiji alikozaliwa Mandela, Mvezo ili awe karibu na babu yake na alibaki hapo mpaka alipovuta pumzi ya mwisho.
Mbali na Mandla, wengine waliokuwepo wakati akikata roho ni viongozi waandamizi wa chama cha ANC na viongozi wa dini waliokuwa wakijitahidi kufariji familia na marafiki wa karibu.
Kwa mujibu wa jarida la kila wiki la City Press, wanafamilia wa karibu waliruhusiwa kuingia katika chumba cha Mandela wawili au watatu kwa ajili ya kuonana naye kwa mara ya mwisho.
 "Waliokuwa nyumbani wamezungumzia huzuni kubwa iliyokuwa katika nyumba hiyo,” City Press liliandika.
Ilielezwa pia kwamba Mandela alikuwa hajaweza kuzungumza neno kwa miezi kadhaa.
Gazeti la Sunday lilimnukuu Bantu Holomisa, ambaye ni mmoja wa watu waliomuona Mandela katika dakika za mwisho, akisema alipokea simu akielezwa kuwa hali ya kiongozi huyo ilikuwa mbaya.
 "Nilikwenda moja kwa moja kumuona katika chumba chake, Nilihuzunika kumuona katika hali ile kwa kuwa alikuwa amebadilika tangu nilipomuona mara ya mwisho,“ alisema.
 Holomisa alisema alikaa kwa zaidi ya saa moja na Mandela na kuondoka nyumbani hapo dakika 90 kabla ya kifo chake kutokea.
"Familia ilikuwa inajitahidi kuvumilia na kulikuwa na utulivu. Hali ilikuwa ngumu pale wanajeshi walipowasili kuchukua mwili wa Madiba karibu saa sita za usiku,” gazeti hilo lilimnukuu mmoja wa wanafamilia aliyekuwepo.

"Wanajeshi walipokuwa wakishuka ghorofani katika chumba cha Mandela na mwili wa Madiba usio na uhai, wakisindikizwa na  Mandla, ndio nilianza kuamini kwamba Madiba hayupo na sisi.”  
CHANZO: HABARILEO

0 comments:

Post a Comment