Monday, December 16, 2013

Mandela alikuwa shabiki wa Man U, Liverpool au Arsenal?

Enzi za uhai wake hakuwahi kutamka wazi timu anayoishabikia zaidi ya kusema kuwa yeye ni mtu anayependa michezo, lakini hiyo haijaifanya dunia iache kuamini kuwa ipo timu moja anayoipenda kuliko nyingine.
Mashabiki wa timu mbalimbali duniani kwa wiki moja sasa wamekuwa wakivutana kila mmoja akitumia picha kama ushahidi kuwa kiongozi huyo alikuwa akishabikia timu fulani.
Katika mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter na instagram, mashabiki wamekuwa wakitumia ushahidi wa picha mbalimbali ambazo kiongozi huyo alipiga na wachezaji kama kielelezo.
Kuishabikia Arsenal

Picha aliyopiga na wachezaji wa Arsenal wakiwa uwanjani nchini Afrika Kusini mwaka 1993 inawafanya waamini kuwa shujaa huyo alikwa akiishabikia Arsenal.
Shabiki mkubwa wa timu hiyo na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha CNN, Piers Morgan aliandika katika ukurasa wake kuwa wamempoteza mtu muhimu katika klabu yako.
“Wakati dunia inasikitika kwa kumpoteza shujaa, sisi mashabiki wa Arsenal tunasikitika kumpoteza shabiki mwenzetu (Gunner),” aliandika Morgan.
Kuishabikiwa Manchester United


Picha inayomuonyesha Madiba akiwa na wachezaji wa Manchester United aliowaalika ofisini kwake mwaka 2006 imetumiwa na mashabiki wa timu hiyo kama ushahidi wa madai kwamba alikuwa akiiunga mkono timu hiyo.
Mashabiki hao wanasema isingekuwa rahisi kwa Mandela kuacha shughuli zake na kuialika timu hiyo kama asingekuwa anaipenda na kuishabikia.
Picha nyingine ya Mandela aliyopiga na kocha wa timu hiyo, Alex Ferguson alipotembelea nchini Afrika Kusini mwaka imetumika kama ushahidi kuwa kiongozi huyo alikuwa akiiunga mkono timu hiyo.
Kuishabikia Liverpool


Mashabiki wa Liverpool wao ndiyo wamejihakikishia kabisa kuwa Madiba alikuwa shabiki wa timu hiyo kwani katika historia yake hakuna picha inayomuonyesha akiwa amevalia jezi nyingine ya mpira wa miguu zZaidi ya Liverpool.
Wanasema Madiba kuna picha nyingi amevaa jezi ya timu ya mpira wa miguu zaidi ya timu yao huku wakiwataka mashabiki wa timu nyingine watoe ushahidi kama wao.
“Jezi ya timu usiyoipenda ni sawa na tambara chafu la chooni, kamwe huwezi kuivaa , Madiba kuvaa jezi ya Liverpool ni ishara kuwa alikuwa shabiki wa kufa na kuzikana (diehard fan),” aliandika shabiki wa Liverpool katika mtandao wa facebook.

Wanasoka wajitoa mhanga
Wachezaji wa Didier Drogba na Emmanuel Eboue wamenusuriika kupewa adhabu na Shirikisho la Mpira la Uturuki baada ya kuonyesha ujumbe wa kumkumbuka Mandela.
Drogba baada ya mechi kwisha wiki iliyopita alivua jezi na kubaki na singlet iliyokuwa na maneno Rest iIn Peace Madiba.
Hata baada ya kutishiwa adhabu alisema hajutii na iwapo atapata nafasi nyingine atarudia kitendo hicho tena na tena.
Katika sheria za soka mchezaji haruhusiwi kuonyesha maneno yanayohusiana na siasa, hata hivyo shirikisho hilo lilishindwa kuwaadhibu baada ya mashabiki kuwaunga mkono.
Klabu ya soka ya Galatasaray nayo iliweka picha kubwa ya Mandela nje ya uwanja wao ujulikanao kama Turk Telekom Arena.
Mandela kupenda michezo
Mandela alikuwa mpenda mchezo, aliwahi kusema kuwa michezo na siasa haviwezi kuchanganywa, lakini ni marafiki walioungana kwa kiasi kikubwa, wenye urafiki wa karibu.
Kauli hiyo aliitoa Juni 24, 1995 aliitoa Mandela jijini Johannesburg akiwa Rais wa Afrika Kusini alipokuwa akikabidhi Kombe la Dunia la ‘Rugby’ kwa nahodha wa timu ya nchi hiyo, Springboks, Francois Pienaar.
Soma Zaidi

0 comments:

Post a Comment