Friday, November 15, 2013

WATAKA NGOMA ZA ASILI ZIFUNDISHWE SHULENI

WANAFUNZI wa shule za msingi Mvumi Misheni na Chalula Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma,  wameiomba Serikali kurudisha vipindi vya ngoma za asili shuleni ili kudumisha utamaduni wa Mtanzania.

Wanafunzi hao walitoa kauli hiyo juzi wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike ambao ni viongozi wa mabaraza.

Walisema sasa hakuna vipindi vya michezo ya ngoma za asili kutokana na Serikali kutoona umuhimu wa kuwepo, hali inayowafanya kutofahamu mila na desturi za utamaduni wa Mtanzania.

Asha Hassani (13) wa Shule ya Msingi Chalula, alisema inasikitisha kuona Serikali imekuwa ikisisitiza michezo mingine, lakini kwa upande wa ngoma za asili halipo kabisa.

Alisema michezo kama mipira na kukimbia imekuwa ikitengewa muda, lakini jambo kama hilo halipo kwenye ngoma za asili.

Hata hivyo, Ofisa Utamaduni Wilaya ya Chamwino, Nicholaus Achipota alisema tatizo lililopo ni baadhi ya walimu kubadilisha vipindi vya ngoma za asili na kuweka masomo mengine.

Awali, wakizungumza kwenye kujadili suala hilo la utamaduni, walimu wa shule ya msingi za Mvumi Misheni walisema kukosekana kwa vipindi hivyo vya ngoma za asili, kunatokana na kutowekwa kwenye mtaala wa kufundishia masomo.

Walimu Flora Kulwa na Shukrani Msambili walisema mfumo mzima wa serikali katika michezo mashuleni umelenga zaidi kwenye masomo ya darasani. Walisema kwenye ngoma za asili huwa na umuhimu pale ambapo kuna ugeni shuleni, lakini si vinginevyo.

0 comments:

Post a Comment