MAHAKAMA ya Kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu
wa kivita, ICC imetengua uamuzi wake wa awali uliomruhusu Rais wa Kenya Uhuru
Kenyatta kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi ya uhalifu wa kivita
inayomkabili.
Mahakama
hiyo sasa imesema kuwa ni lazima Rais Kenyatta afike mbele ya mahakama hiyo
kusikiliza kesi yake na ushahidi unaotolewa dhidi yake.
Mahakama
hiyo imesema kama sheria inavyotaka, Rais Kenyatta lazima binafsi ahudhurie
vikao vya kesi inayomkabili. Imesema maombi yoyote ya baadaye ya kutaka
asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo, yatafikiriwa kutokana na msingi wa
suala linaloombewa ruhusa hiyo.
Mahakama
hiyo imefikia uamuzi kwamba hukumu iliyotolewa katika rufaa ya tarehe 25 Oktoba
2013 ya Mwendesha mashitaka dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang,
imetoa taarifa mpya muhimu ambayo inahalalisha kuangaliwa upya kwa suala la
kesi hiyo.
Mahakama ya
Rufaa ya ICC imehitimisha kuwa Mahakama ina hiyari kwa mujibu wa kifungu namba
63(1), kinachosema kuwa "mtuhumiwa ni lazima awepo mahakamani wakati kesi
inayomkabili ikiendeshwa", lakini hiyari hiyo imewekewa kikomo.
Mahakama
ya Rufaa imetoa uamuzi kwamba mtuhumiwa kutofika mahakamani, inaruhusiwa pale
tu panapokuwa na sababu maalum na za kipekee, na lazima sababu hizo ziwe
zinakidhi hoja kwa mtuhumiwa kutofika mahakamani hapo.
Imeendelea kusema kwamba
uamuzi wa kama mtuhumiwa aruhusiwe kutohudhuria sehemu ya vikao vya kesi yake
lazima uzingatie hali halisi ya ombi la mtuhumiwa.
Awali
mahakama hiyo ya ICC katika uamuzi wake wa tarehe18 October 2013, ilitoa
masharti kwa upande wa utetezi wa Bwana Uhuru Muigai Kenyatta kuwepo mahakamani
hapo wakati wa ufunguzi na kufunga kesi inayomkabili badala ya kuwepo wakati
wote. Wakati huo angeweza kusikiliza maelezo kutoka pande zote na kusikiliza
maoni ya waathirika wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 nchini Kenya.
Pia angetakiwa kuwepo siku ya kufunga kesi hiyo kwa kusikiliza hukumu yake.
SOMA ZAIDI: BBC SWAHILI







0 comments:
Post a Comment