Saturday, November 23, 2013

HUU NDIYO MPASUKO WA CHADEMA

SASA ni dhahiri kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinameguka na kubaki vipande, kutokana na uamuzi uliochukuliwa jana na Kamati Kuu yake kuwavua rasmi madaraka vigogo wake watatu. Mkutano wa siku mbili wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika Dar es Salaam hatimaye jana ulimalizika kwa kuchukua hatua dhidi ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Baada ya hatua hiyo ambayo ni ngumu kuaminika ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani, zilipatikana taarifa zingine za Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Said Arfi kujiuzulu wadhifa huo. Kwa hatua hiyo, viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya chama kutokana na tuhuma za kuunda mtandao wa kukivuruga chama hicho na kuiagiza Kamati ya Chama ya Wabunge kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa madaraka yake yote ya Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hayo yalibainishwa jana na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu alipokuwa akitoa uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Alisema uamuzi mwingine ni pamoja na viongozi hao kuandikiwa hati zenye tuhuma dhidi yao haraka na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe chama kwa vitendo vyao, ikiwa ni pamoja na kupewa fursa ya kujitetea kama inavyoelekezwa kwenye Katiba ya chama.
Lissu alisema Kamati pia imetaka baada ya utekelezaji wa azimio, ikutane kwa kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua zingine zitakazofuata.
Mtandao wa ushindi Akizungumza kilichojiri katika mkutano huo hata kufikia uamuzi huo, alisema ilibaini kuwapo mkakati wa kukiharibu chama kupitia waraka uitwao “Mkakati wa Mabadiliko 2013” ulioandaliwa na kikundi kinachojiita “Mtandao wa Ushindi”.
Alisema kikundi hicho vinara wake wakuu ni wanne ambao ni Zitto anayejulikana kama ‘MM’ au Mhusika Mkuu, Dk Mkumbo anayejulikana kama M1, Mwigamba anayejulikana kama M3 na mtu mwingine ambaye jina lake halijajulikana anayejulikana kama M2.
Alisema M2 anatajwa kwenye waraka huo kuwa yuko ukingoni kuondolewa katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika Sekretarieti ya Chama Makao Makuu. “Kwa mujibu wa waraka wenyewe, mkakati huu umeandaliwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza utekelezaji,” alisema.
Lissu alisema mbele ya Kamati Kuu, Dk Mkumbo alikiri kuwa MM ni Zitto, M1 ni yeye na M3 ni Mwigamba na kukataa kumfahamu M2 na kukiri yote yaliyoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni ya kwao.
Alisema lakini Zitto alikana kuuona waraka huo na kumhusu kwa kuwa ametaja tu jambo ambalo Kamati Kuu ilikataa kutokana na kuwa Juni 30 waraka huo ndio ulihaririwa mara ya mwisho na kupelekwa kwa Zitto kwa ushauri na utekelezaji.
Lissu alisema mkakati huo ni wa kuipasuapasua Chadema na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za nchi na si wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama kwa njia ya...
SOMA ZAIDI: HABARILEO ONLINE

0 comments:

Post a Comment