Na Benedict
Liwenga-MAELEZO-Dar es Salaam.
KAMPUNI inayojishughulisha na
utoaji wa mikopo kwa watumishi wa Serikali na kampuni zilizothibitishwa
ijulikanayo kama Platinum Credit Ltd
leo imekabidhi vifaa vya michezo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Jeshi la Magereza na TAMISEMI kwa ajili ya maandalizi ya michezo ya
Shimiwi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni mjini Dodoma.
Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Fedha
wa Kampuni hiyo Bw. Elias Samwel amesema kuwa kampuni yake inajihusisha na
utoaji wa mikopo ya fedha kwa watumishi wa serikali na kampuni
zilizothibitishwa na kiasi cha ziada wanachokipata wanakitumia katika kusaidia
jamii katika shughuli mbalimbali ikiwemo michezo.
Aidha, kampuni hiyo imekabidhi jezi,
tisheti na kofia zenye thamani ya shilingi milioni 10 ili ziweze kusaidia
katika michezo ya Shimiwi itakayofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
“Thamani ya vifaa hivi ni ndogo
lakini ninaamini kuwa vitasaidia katika kuleta chachu ya maendeleo katika
michezo ya shimiwi”. Alisema Samwel. Kwa upande wake Katibu wa Klabu ya
Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Saidi Marusu
ameishukuru kampuni ya Platinum Credit Ltd kwa mchango wao mkubwa waliojitolea
katika kusaidia kutoa vifaa vya michezo.
“Kwa niaba ya Wizara Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo napenda kutoa shukurani kwa kupokea vifaa hivi kwani ninaamini
kuwa vitaleta chachu katika mashindano haya ya Shimiwi”. Alisema Bw. Marusu.
Naye Kamishna Msaidizi wa Jeshi la
Magereza Mkwanda Hassid Mkwanda ameishukuru kampuni hiyo kwa kupata vifaa hivyo
na amesema kuwa vitasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo yao katika
michezo ya Shimiwi. “Vifaa hivi vitatumika kwa lengo
lililokusudiwa na sio vinginevyo”. Alisema Mkwanda.
Naye mwakilishi wa TAMISEMI ambaye ni
Katibu Mkuu wa Shimiwi Bw. Ramadhani Sululu ameishukuru kampuni hiyo kwa
mchango wake mkubwa wa kutoa vifaa hivyo vya michezo na ameongeza kuwa vifaa
hivyo vitasaidia kuleta hamasa katika michezo.
“Katika mashindano ya Shimiwi tumejiandaa
vizuri na tunaamini kuwa tutashiriki vema katika michezo hiyo”. Alisema Sululu. Mashindano ya Shimiwi yanahusisha
Wizara zote za Serikali na Taasisi zake ambapo itajumuisha michezo ya kuvuta
kamba, mpira wa miguu, pete, riadha, drafti, bao, karata na kurusha tufe.








0 comments:
Post a Comment