Monday, December 24, 2012

Coaster Ruksa Kusafirisha Abiria Dar - Moshi

SERIKALI imeruhusu mabasi aina ya Toyota Double Coaster kusafirisha abiria mpaka Moshi, ili kupunguza tatizo la usafiri wakati huu wa msimu wa sikukuu.
Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Conrad Shio alisema lengo la uamuzi huo ni kuondokana na tatizo la usafiri.
Alisema kuwa mabasi ambayo yalikuwa tayari kufanya shughuli hiyo, yalitakiwa kupakia abiria wake kwenye Kituo cha Mabasi  ya Mikoani cha Ubungo chini ya usimamizi wa Sumatra na Polisi kwa kutumia bei halali iliyopangwa na Serikali.
“Kabla ya kuanza safari, mabasi haya yalitakiwa kuja ubungo na kupakia abiria hapo chini ya usimamizi wa Polisi na Sumatra na baada ya hapo tunawaandikia kibali na wanaanza safari yao,” alisema.
Aidha alisema katika operasheni waliyoianza ya kukagua mabasi yanedayo mkoani na kudhibiti upandaji wa nauli kiholela kuanzia Novemba mpaka Jumamosi iliyopita, mabasi 87 yalikamatwa kwa kosa la kupandisha nauli na asilimia kubwa yalikuwa aina ya Toyota Double Coaster.
“ Katika mabasi tuliyokamata ni yale yanayofanya safari zake Dar es Salaam-Moshi-Arusha, Dar es Salaam-Mwanza na Dar es Salaam-Bukoba.
“Lakini kwa asilimia kubwa ni mabasi ya Toyota Double Coaster   badala ya kufuata utaratibu tuliouweka na kuwa na vibali, waliweka vituo vyao Ubungo Maziwa, Mwenge na maeneo mengi na hao ndio tuliowakuta na kosa la kupandisha nauli hadi Sh 45,000,” alisema.
Alisema kuwa pia mabasi manne yanayofanya safari zake kutoka ya Dar es Saalm kwenda Mwanza yamekamatwa kutokana na ubovu wa magari yao na mengine zaidi yako katika orodha hasa baada ya kufuatiliwa mwenendo wao.
“Utakuta mabasi ya kampuni fulani, leo limeharibika hili, kesho lingine na siku inayofuata lile la kwanza linaharibika, hii inaonesha kuwa kampuni hiyo hayafanyi matengenezo. Majina ya kampuni hizo tutayataja baada ya kuyafikisha makao makuu,” alisema.
Noah hapana
Shio alikana kuruhusu magari madogo aina ya Noah kusafirisha abiria na kuonya kuwa magari hayo yatakuwa yakifanya hivyo kinyume cha sheria na kwa kificho.
Kutokana na watu wengi kutaka kusafiri wakati huu wa msimu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka, bei za nauli za kwenda mikoani zimepanda zaidi huku baadhi ya abiria wakishindwa kusafiri kutokana na ongezeko la nauli na mabasi kujaa.
Uchunguzi ulifanywa na gazeti hili, ulibaini kuwa bei ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ilipanda hadi kufikia Sh 50,000 kwa abiria mmoja ikiwa ni tofauti na bei ya Serikali ya Sh 16,400 kwa mabasi ya kawaida; semi-Luxury Sh 25,100 na luxury Sh 28,600.
Gazeti hili lilibaini pia kuwa magari binafsi aina ya Noah juzi yalisafirisha abiria kwenda Moshi na Arusha kutoka Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment