Friday, October 5, 2012

SERENGETI FIESTA 2012 HAPATOSHI LEO LEADERS CLUB



Tamasha la Serengeti fiesta 2012 leo linafikia tamati kwa mwaka huu baada ya kutimua vumbi kwa takribani miezi miwili tangu kuanza kwake na kufanikiwa kuangusha burudani yake katika mikoa 11 ya Tanzania bara zikiwemo Kilimanjaro, Tanga, Musoma ,Shinyanga , Mwanza, Tabora, Singida,Mbeya , Iringa, Dodoma na Morogoro.
Sura tofautitofauti za wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya na baadhi ya wasanii maarufu  wa filamu za kibongo (bongo movie) zimekuwa zikionekana kwa nyakati tofauti   katika majukwaa mbalimbali ya tamasha hilo katika mikoa mbalimbali hali iliowafanya mashabiki wa tamasha hilo kushuhudia ukweli juu ya kauli mbiu ya mwaka huu unaosema ‘ Serengeti fiesta 2012 muonekano tofauti, burudani ileile’
 Maadhimisho ya kilele cha tamasha hilo yanatamatishwa usiku wa leo katika viwanja vya leaders club maeneo ya kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo msanii mmoja kati ya wasanii wenye  miraba minne kutoka nchini Marekani Leonard Roberts maarufu kama Rick Ross atasababisha muonekano tofauti wa Serengeti fiesta kuendelea kushika hatamu pale atakapopanda katika jukwaa lililoandaliwa kwa namna ya tofauti na ya kipekee kulioko miaka iliyopita.
Rick Ross ambaye ni mmoja kati ya wasanii wakali wanaotamba katika ulimwengu wa muziki wa rap (Hiphop) nchini Marekani amewasili usiku wa kuamkia leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere na kupokelewa na  waandaaji wa tamasha hilo kampuni ya Prime Time Promotions wakiongozwa na Mkurugenzi wa Clouds Media Group Bw. Joseph Kussaga na Mkurugenzi wa Utafiti wa Clouds Media Group Bw. Ruge Mutahaba pamoja nao mkurugenzi wa masoko wa Kampuni ya bia ya Serengeti Bw. Ephraim Mafuru akiwa ameongozana na  meneja wa bia ya Serengeti  Bw. Allan Chonjo kutoka kampuni ya bia ya Serengeti ambayo ndio mdhamini mkuu wa tamasha hilo kwa mwaka wa tatu sasa.
Akizungumza kuhusu ujio wa mwanamziki huyo na mstakabali mzima kuhusu tamasha la Serengeti fiesta mwaka huu,mkuruganzi wa utafiti wa clouds media group Bw. Ruge Muatahaba amesema taratibu zote zimekamilika na kwamba maandalizi yote kuhusiana na tamasha hilo yako katika hatua nzuri “ maandalizi yako vizuri kabisa na mambo yanakwenda kama yalivyotarajiwa, watanzania watarajie kuona burudani ya aina yake tofauti kabisa na miaka iliyopita” alisema Mutahaba huku akitoa shukrani zake za dhati kwa kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar esSalaam Sulleimani Kova kwa kumhakikishia ulinzi wa kutosha katika eneo la tukio na maeneo ya jirani na kusema kuwa mbali na askari polisi pia watakuwepo askari mgambo kutoka katika makampuni ya ulinzi kama Altimate Security na mengineyo hali itakayowafanya watanzania wote watakaofika na kupita katika maeneo yanayozunguka eneo la tukio kuwa katika hali ya usalama.
Kwa niaba ya wadhamini wa tamasha hilo kampuni ya bia ya Serengeti, meneja wa bia ya Serengeti Bw. Allan Chonjo amesema kilele cha tamasha hilo mwaka huu itakuwa na sura mpya kabisa hali itakayoonesha kwa vitendo muonekano mpya burudani ileile ya Serengeti fiesta 2012 “ watanzania wengi wamekuwa wakishuhudia muonekano mpya wa tamasha hili katika mikoa yote ambayo tumeweza kupita na kwamba muonekano huo tunatamatisha hapa jijini kwa kufanya kila kitu kilichozoeleka miaka iliyopita kuwa katika hali nzuri na ya kuvutia zaidi” alisema Chonjo na kuongeza kuwa wasanii watakaotoa burudani ukumbini hapo watajitikeza jukwaani kwa staili tofauti na kufanya tamasha hilo kuwa kivutio kwa mashabiki wake.
Aidha Bw. Chonjo amewataka watanzania wote kuwa wastaarabu katika tamasha hilo kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuepusha madhara na matatizo yanayoweza kepukika “tumeweka utaratibu mzuri wa kununua tiketi za kuingilia kwa kuweka vituo karibu kona zote za jiji ili kuepuka vurugu na msongamano getini wakati wa kuingia” aliongeza Chonjo na kumalizia kwa kuwataka mashabiki wanywe kistaarabu.
Tamasha la Serengeti fiesta leo lina fikia kilele chake kwa mwaka huu 2012 tayari kabisa kuanzania kwa maandalizi ya tamasha hilo kwa mwaka ujao 2013.

0 comments:

Post a Comment