Showing posts with label Nelson Mandela. Show all posts
Showing posts with label Nelson Mandela. Show all posts

Wednesday, December 18, 2013

Ugomvi familia ya Mandela wafufuka

 
QUNU, Afrika Kusini
SIKU mbili baada ya maziko ya Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ugomvi kati ya watoto na wajukuu wa shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani, umeibuka upya.
Inadaiwa siku chache kabla ya maziko ya Mandela, mjukuu wake mkubwa, Mandla alifukuzwa katika nyumba ya babu yake katika kijiji cha Qunu.
Mbali na kufukuzwa, inadaiwa vitasa vya nyumba hiyo vilibadilishwa na huduma za maji na umeme zilizokuwa zikitumika katika nyumba ya Mandla kijijini hapo, zilisitishwa.
Hata usafiri kwa ajili ya kwenda mazikoni haukutolewa kwa ndugu waliozaliwa pamoja na Mandla na wanasiasa na viongozi wa dini waliokuwa wakishirikiana na mjukuu huyo, walitengwa na wengine kukosa mwaliko wa kuhudhuria maziko ya Jumapili.
Inadaiwa kwamba mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, alimtaka Mandla, ambaye ni Chifu wa Mvezo, kijiji alichozaliwa Mandela, kutoa mifugo yake iliyokuwa katika eneo la nyumba hiyo.
Gazeti la The Times, limebainisha kwamba mjane wa Mandela, Graca Machel na mwanasheria wa siku nyingi wa kiongozi huyo, George Bizos, walijaribu kuwataka wanafamilia hao kudhibiti hali hiyo isijioneshe lakini bila mafanikio.
Kiini
Ugomvi huo ulitokana na mgogoro ulioibuka wakati Mandela akiwa mahututi katika Hospitali ya Med Clinic, kuhusu wapi alipaswa kuzikwa kati ya kijiji alichozaliwa cha Mvezo au alichokulia cha Qunu.
Wosia wa Mandela uliofunguliwa akiwa katika hospitali hiyo ya Pretoria, ulieleza wazi kuwa alipenda azikwe karibu na wanawe walikozikwa na kwa wakati huo, makaburi yao yalikuwa Mvezo.
Wanawe hao, Makgato aliyefariki dunia mwaka 2005; Makaziwe, ambaye ni mwanawe wa kike wa kwanza aliyefariki dunia akiwa mchanga mwaka 1948; na Madiba Thembekilea, aliyekufa kwa ajali ya gari mwaka 1969; walizikwa Qunu.
Hata hivyo, Mandla, ambaye ni mtoto wa Makgato na kiongozi mkuu wa ukoo wa Madiba, anaotoka Mandela na Mbunge wa ANC, alifukua miili hiyo mwaka 2011 na kuizika upya Mvezo, alikozaliwa babu yake.
Mahakamani
Uamuzi huo wa Mandla ambao haukushirikisha familia, ulisababisha watoto wa Mandela, wakiwakilishwa na Mwanasheria, Sandla Zigadla, kwenda mahakamani kutaka mabaki ya ndugu zao, yarudishwe Qunu.
Jaji Lusindiso Pakade, alitoa amri kumtaka Mandla aache kuingilia mchakato wa kuhamisha mabaki ya miili hiyo kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Mandla alifanya jaribio la kuzuia mchakato huo, lakini Jaji Pakade, alizuia jaribio hilo na badala yake akakazia hukumu kutaka miili hiyo ifukuliwe haraka.

Nguvu yatumika
Baada ya hukumu hiyo, huku vyombo vya habari vya Afrika Kusini na kimataifa vikishuhudia, maofisa wa Serikali walivunja lango la makazi ya Mandla kwa vifaa maalumu, ili kutoa nafasi kwa gari la kubeba maiti kuingia ndani yalikokuwa makaburi hayo.  
Miili ilifukuliwa na uchunguzi wa kisayansi kufanyika kwa takribani saa mbili na kuthibitisha kwamba ni mabaki ya watoto hao, kabla ya kuzikwa upya Qunu. 
Juzi, Mandla alisema: “Kama ilivyo kwa karibu kila mmoja wetu katika familia, kabla ya kifo cha babu, nilidhamiria kutoomboleza, nilijiandaa kusherehekea mazuri yote aliyoniachia na aliyoacha kwa ajili ya ulimwengu.
“Hata hivyo, nilikosea, kwa kuwa maumivu ya kumpoteza tata bila kutarajia, yaliniingia kama vile niliyekatwa na kitu chenye ncha kali.”
Mjukuu huyo, alisema alijikuta akiugua upweke siku chache baada ya kifo cha Madiba, pamoja na kuwa karibu na familia. “Hata hivyo ujumbe wa kututakia faraja ulivyokuwa ukitufikia, nilianza kupona,” alisema Mandla.
Pia alishukuru Serikali kwa kuandaa masuala yaliyokuwa yakifanyika katika siku hizo 10 za maombolezo na kuongeza kuwa kila kitu kilifanyika vizuri.

Monday, December 16, 2013

Mandela alikuwa shabiki wa Man U, Liverpool au Arsenal?

Enzi za uhai wake hakuwahi kutamka wazi timu anayoishabikia zaidi ya kusema kuwa yeye ni mtu anayependa michezo, lakini hiyo haijaifanya dunia iache kuamini kuwa ipo timu moja anayoipenda kuliko nyingine.
Mashabiki wa timu mbalimbali duniani kwa wiki moja sasa wamekuwa wakivutana kila mmoja akitumia picha kama ushahidi kuwa kiongozi huyo alikuwa akishabikia timu fulani.
Katika mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter na instagram, mashabiki wamekuwa wakitumia ushahidi wa picha mbalimbali ambazo kiongozi huyo alipiga na wachezaji kama kielelezo.
Kuishabikia Arsenal

Picha aliyopiga na wachezaji wa Arsenal wakiwa uwanjani nchini Afrika Kusini mwaka 1993 inawafanya waamini kuwa shujaa huyo alikwa akiishabikia Arsenal.
Shabiki mkubwa wa timu hiyo na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha CNN, Piers Morgan aliandika katika ukurasa wake kuwa wamempoteza mtu muhimu katika klabu yako.
“Wakati dunia inasikitika kwa kumpoteza shujaa, sisi mashabiki wa Arsenal tunasikitika kumpoteza shabiki mwenzetu (Gunner),” aliandika Morgan.
Kuishabikiwa Manchester United


Picha inayomuonyesha Madiba akiwa na wachezaji wa Manchester United aliowaalika ofisini kwake mwaka 2006 imetumiwa na mashabiki wa timu hiyo kama ushahidi wa madai kwamba alikuwa akiiunga mkono timu hiyo.
Mashabiki hao wanasema isingekuwa rahisi kwa Mandela kuacha shughuli zake na kuialika timu hiyo kama asingekuwa anaipenda na kuishabikia.
Picha nyingine ya Mandela aliyopiga na kocha wa timu hiyo, Alex Ferguson alipotembelea nchini Afrika Kusini mwaka imetumika kama ushahidi kuwa kiongozi huyo alikuwa akiiunga mkono timu hiyo.
Kuishabikia Liverpool


Mashabiki wa Liverpool wao ndiyo wamejihakikishia kabisa kuwa Madiba alikuwa shabiki wa timu hiyo kwani katika historia yake hakuna picha inayomuonyesha akiwa amevalia jezi nyingine ya mpira wa miguu zZaidi ya Liverpool.
Wanasema Madiba kuna picha nyingi amevaa jezi ya timu ya mpira wa miguu zaidi ya timu yao huku wakiwataka mashabiki wa timu nyingine watoe ushahidi kama wao.
“Jezi ya timu usiyoipenda ni sawa na tambara chafu la chooni, kamwe huwezi kuivaa , Madiba kuvaa jezi ya Liverpool ni ishara kuwa alikuwa shabiki wa kufa na kuzikana (diehard fan),” aliandika shabiki wa Liverpool katika mtandao wa facebook.

Wanasoka wajitoa mhanga
Wachezaji wa Didier Drogba na Emmanuel Eboue wamenusuriika kupewa adhabu na Shirikisho la Mpira la Uturuki baada ya kuonyesha ujumbe wa kumkumbuka Mandela.
Drogba baada ya mechi kwisha wiki iliyopita alivua jezi na kubaki na singlet iliyokuwa na maneno Rest iIn Peace Madiba.
Hata baada ya kutishiwa adhabu alisema hajutii na iwapo atapata nafasi nyingine atarudia kitendo hicho tena na tena.
Katika sheria za soka mchezaji haruhusiwi kuonyesha maneno yanayohusiana na siasa, hata hivyo shirikisho hilo lilishindwa kuwaadhibu baada ya mashabiki kuwaunga mkono.
Klabu ya soka ya Galatasaray nayo iliweka picha kubwa ya Mandela nje ya uwanja wao ujulikanao kama Turk Telekom Arena.
Mandela kupenda michezo
Mandela alikuwa mpenda mchezo, aliwahi kusema kuwa michezo na siasa haviwezi kuchanganywa, lakini ni marafiki walioungana kwa kiasi kikubwa, wenye urafiki wa karibu.
Kauli hiyo aliitoa Juni 24, 1995 aliitoa Mandela jijini Johannesburg akiwa Rais wa Afrika Kusini alipokuwa akikabidhi Kombe la Dunia la ‘Rugby’ kwa nahodha wa timu ya nchi hiyo, Springboks, Francois Pienaar.
Soma Zaidi

Monday, December 9, 2013

Picha ya mwisho ya Mandela yaoneshwa

PICHA ya mwisho ya Kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela akiwa hai imetolewa akionekana mwenye tabasamu huku ameshika mkono wa kitukuu chake.

Picha hiyo ilipigwa Mei nyumbani kwake Houghton jijini Johannesburg akiwa amekaa kwenye kiti alichokipenda sana –mwezi mmoja kabla hajalazwa hospitalini jijini humo.

Kwa familia ya Mandela picha hiyo inabaki kuwa kumbukumbu nzuri za nyakati za furaha. Na kwa mtoto wa miaka mitatu, Lewanika, ambaye anaonekana kwenye picha hiyo, itakuwa ni kumbukumbu ya aina yake, anasema baba yake, aliyeipiga, akiongeza kuwa kitakuwa ni kitu ambacho ni hazina kwake atakapokuwa amekua kiasi cha kuweza kuelewa mambo.
Ni taswira ya mwisho ya mtu wa kihistoria ambaye Waafrika Kusini na walimwengu duniani wanamwomboleza-huku pia wakisherehekea urithi aliowaachia wa amani, mtu mashuhuri ambaye karama zake zitahisiwa na kila mtu duniani hata katika miaka ijayo.
Picha hiyo inamwonesha Lewanika akiwa amekaa kwenye mkono wa kiti, huku akimwangalia kwa udadisi mkubwa babu yake, mtu ambaye amekuja kuwa alama ya nchi yake, katika mapambano dhidi ya maovu, lakini ambaye pia mtoto huyo alizoea kumwita ‘baba’.
Akihojiwa jana na The Mail on Sunday la Uingereza, baba yake Lewanika, Ndaba Mandela-ambaye ni mjukuu wa Mandela-alisema alipiga picha hiyo akiamini kuwa huenda ikawa ni fursa yake ya mwisho kuwapiga picha wawili hao wakiwa pamoja.
“Ilikuwa Mei, Jumamosi moja mchana. Tulikuwa tumekuja kumjulia hali mzee huyo na tukamkuta akiangalia kipindi cha National Geographic kwenye televisheni, “Ndaba (30) alisema.
“Alimwangalia Lewanika na kumwita, “njoo, njoo.” Uso wa mzee ulijawa nuru alipomwona-kama ujuavyo alipenda sana watoto. Walikumbatiana na mwanangu akamwita “baba”. Ilinigusa sana kuwaona wawili hao wakiwa pamoja.”
Ndaba ambaye ni Mwenyekiti wa Wakfu wa Africa Rising ambayo inashughulikia maendeleo ya uchumi wa vijana wa Afrika Kusini, anaishi katika nyumba ya Mandela ya Houghton, ambako ndiko mzee huyo alifia Alhamisi.
Ndaba alisema: “Tunajivuna kwamba tumeweza kutunza kumbukumbu hii maalumu na kupata heshima ya kuionesha dunia.”
Alipenda watoto
Binti wa Mandela, Zindzi (53) naye aliiambia The Mail on Sunday mapema mwaka huu jinsi baba yake alivyopenda kuwa na watoto na vijana karibu naye. Anakumbuka simulizi ya jinsi alivyotoka gerezani, alipomwomba aache kumnyonyesha mwanawe wa kiume ili akae na mtoto huyo chumbani kwake, amlishe na kumlea kila usiku.
Zindzi alisema wakati fulani:”Baba hufurahi sana anapoona watoto wamemzunguka. Anawapenda na hufurahi wakimpandapanda.”
Picha hii ilitoka wakati Mandela akisumbuliwa na maambukizi sugu ya mapafu yaliyogundulika akiwa gerezani alipotengwa na kuwekwa kwa miezi kadhaa akiwa ndani ya rumande yenye giza.
Hali yake ilibadilika ghafla mapema wiki jana, wakati binti yake mkubwa Makaziwe, aliyezaliwa katika ndoa yake ya kwanza, aliposimulia uchungu wake alipomwona baba yake akiwa “katika kitanda chake cha mauti.”
Jana Ndaba, akiwa mwana familia wa kwanza kuzungumza tangu Mandela afariki dunia, alielezea masikitiko yake makubwa, lakini akaongeza:”Kuna hisia za faraja pia, kwamba hatimaye yuko mahali pema zaidi. Ni faraja kutambua kuwa mamilioni kwa mamilioni ya watu duniani wako nasi katika majonzi haya. Nimeona maua yote nje ya nyumba, haiaminiki.”
Kuhusu picha hiyo, Ndaba aliongeza: “Siku moja nitamwambia mwanangu Lewanika juu ya babu yake huyu alivyokuwa maarufu na picha hii itakuwa maalumu kwake.”
Alikumbuka, kwamba Mandela alikuwa amekaa kwenye kiti chake katika chumba cha kupumzika nyumbani kwake, huku amezingirwa na vitabu na picha alizopewa kama zawadi, alipompeleka mwanawe huyo. 
Kuna wakati madaktari walikuwa na wasiwasi na afya yake hasa kutokana na moyo wake kuzidi kudhoofu; mikono yake iliyovimba kutokana na tatizo hilo, vyote vinaonekana kwenye picha hiyo.
Baada ya wiki kadhaa alizidiwa usiku wa manane na kukimbizwa katika hospitali ya moyo jijini Pretoria ambako alilazwa kwa miezi mitatu. Katika picha hiyo Mandela anaonekana mwenye furaha kwa kuwa na kitukuu chake.
“Alipozaliwa nilimwuliza mzee tumwite jina gani,” Ndaba anakumbuka. “Na babu yangu akapendekeza jina la Ngubencuka ambalo ni la mmoja wa wahenga wetu. Nalazimika kusema nilikuwa tayari nina jina la Lewanika lakini tukampa jina la katikati la Ngubencuka.”
Ndaba alikuwa Brazil akiwakilisha nchi yake katika kura za ratiba ya fainali za soka Kombe la Dunia aliposikia taarifa za kifo cha babu yake. “Ndio nilikuwa nimewasili katika eneo la shughuli mara nikapigiwa simu na shangazi. Tulirudi nyumbani mara moja.”
Alisema takribani asilimia 90 ya familia tulikusanyika nyumbani kwa Mandela katika barabara inayopambwa na miti ya mijakaranda katika kitongoji cha watu matajiri.
“Ni majonzi lakini kila mmoja alikuwa akijishughulisha kulisha ndugu na kuandaa mambo mbalimbali. Tulikuwa na chakula cha pamoja leo (jana) jambo ambalo ni jema.”
Miongoni mwa watu walioshinda nyumbani hapo ni mke wa pili wa Mandela, Winnie. Mke wa tatu Graca Machel alikuwa pembeni mwa kitanda wakati anakata roho Alhamisi, pamoja na wajukuu wake kadhaa na wazee wa kimila wa jamii ya Waxhosa. Walijumuika pia na Mchungaji ambaye alifanya maombi ya mwisho kwa mzee.
Mandela alikuwa na watoto sita, watatu walishatangulia mbele za haki. Mmoja alikuwa ni wa kiume Makgatho Lewanika Mandela, ambaye alifariki dunia kwa Ukimwi mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 55. Mjukuu wa Makgatho-aliye na Mandela kwenye picha hiyo- alipewa jina la kati la babu yake huyo.
Kwa jumla kuna wajukuu 17 na vitukuu 13. Zenani ambaye ni binti wa mjukuu wa Mandela, Zoleka, alifariki dunia katika ajali ya gari siku ya mkesha wa uzinduzi wa sherehe za fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini. Alikuwa na umri wa miaka 13.
Ndaba alisema: “Sisi ni familia kubwa na tutakuwa hapa kwa siku chache zijazo. Tukio kubwa litakuwa ni sherehe za kumbukumbu ya Mandela Jumanne. Kwa maziko ya Jumapili, nina uhakika kutakuwa na wakuu kadhaa wa serikali za dunia.
“Najua Obama (Barack-Rais wa Marekani) alisema anataka kuja na Rais wa Ufaransa anataka kuja pia, na viongozi mbalimbali wa Afrika. Sijasikia ni nani anakuja kutoka Uingereza”.
Hata hivyo, habari kutoka Uingereza zilisema Malkia Elizabeth II hatahudhuria maziko ya Mandela kutokana na ushauri wa madaktari apunguze safari ndefu kutokana na afya yake. Mwanawe, Prince Charles atamwakilisha.
Malkia badala yake anatarajiwa kutoa heshima zake katika Misa maalumu itakayofanyika kwenye Kanisa la Westminster Abbey, London, Uingereza.

Soma hapa jinsi Nelson Mandela alivyosahau viatu vyake alipokuja Tanzania

 
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watanzania kuacha tabia ya kuwa na roho ya kulipiza visasi badala yake wawe watu wa kusamehe na kusahau kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuenzi moja kwa moja Rais mstaafu wa Afrika Kusini Marehemu Nelson Mandela.
Rais Kikwete amesema mara baada ya Rais Mandela kutolewa gerezani  hofu ilitawala Afrika ya Kusini, watu wengi wakitambua kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais badala ya kuijenga nchi ataanza kulipiza visasi kwa wale wote waliotumika kwa namna moja ama nyingine kumtesa yeye na watu wa nchi yake.
“Badala yake Mzee Mandela alitoa tamko la kuwasamehe wote waliohusika kuwabagua watu wa Afrika ya Kusini, na kisha aliunda tume maalumu ya maridhiano ili kujenga umoja kati ya watu wenye ngozi nyeupe na wenye ngozi nyeusi, jambo hili ni la ajabu sana” amesema Kikwete.
“Hiki ni kipimo kikubwa cha ukomavu wa kisiasa, yatupasa watanzania na viongozi mbalimbali kuenzi jambo hili la kusameheana na kutokuwa walipiza visasi, hapa tulipo wengine wanasema kabisa nikichaguliwa watanikoma….. lakini nawasihi tumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga mambo mema aliyoyafanya ambayo hadi hivi leo yamechangia kukuza uchumi wa Afrika ya Kusini, “amesema Kikwete.
Amesema tokea enzi za TANU Tanzania imekuwa karibu sana na vyama vya ukombozi wa mataifa mengi Afrika, kikiwemo chama cha ANC ambacho kilikuwa kikiongozwa na Marehemu Mzee Mandela, hivyo aliwasihi watanzania waendeleze umoja huo .
“Kuna jambo moja ambalo hamlijui mwaka wa 1964 Mzee Mandela alikuja nchini na kufikia kwa mweka hazina wa TANU, Siro Swai, alikuwa akielekea kwenye mafunzo ya kijeshi Algeria, aliacha viatu vyake ‘pea moja’ akieleza kuwa atakaporudi atakuja kuvichukua lakini haikuwa hivyo, nilipokuwa waziri wa mambo ya nje, mke wa Swai alinifuata na kunieleza, nasi tulilazimika kuzirudisha kipindi hicho ambacho Mzee Mandela alikuwa Rais wa nchi hiyo tayari,” Anaeleza Kikwete.
Amesema haya yote yanatafsiri ukaribu na undugu wa hali ya juu kati ya nchi zetu mbili na ndiyo maana katika kumuenzi leo hii kwenye shughuli za kutimiza miaka 52 ya uhuru hatutakuwa na vikundi vya kutumbuiza.

Saturday, December 7, 2013

RAIS BARACK OBAMA KUONGOZA MAZISHI YA MZEE NELSON MADIBA MANDELA...

 
Gari maalumu liliondoa mwili wa Mzee Nelson Mandela kutoka nyumbani kwake alipofariki dunia usiku wa kuamkia jana.

 Kama haamini kilichotokea. Mtu huyu akishika picha ya Mzee Mandela mara baada ya kutangazwa kufariki dunia.

Karama aliyokuwa nayo Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ya kuunganisha watu, itadhihirika kutokana na orodha ya wageni wanaotarajiwa kushiriki mazishi yake, wakiwamo viongozi wa kimataifa weupe na weusi, nyota mashuhuri wa filamu na wanamuziki.
Rais Barack Obama wa Marekani, mkewe Michelle na mabinti zao wawili Sasha na Malia, wataungana na marais wastaafu wa Marekani akiwamo Bill Clinton, ambaye alimfahamu vilivyo Mandela.
Maarufu wengi ambao walikuwa na uhusiano wa binafsi na Mandela, kama vile Oprah Winfrey na kiongozi wa kikundi cha U2 Bono, nao wanatarajiwa kushiriki mazishi ya kitaifa yatakayofanyika keshokutwa katika uwanja wa michezo wa FNB jijini Johannesburg wenye uwezo wa kuchukua watu 90,000.
Askofu Mkuu mstaafu Desmond Tutu wa Cape Town, anatarajiwa kuongoza Ibada maalumu ya mazishi hayo.
Hadi  jana vitabu vya rambirambi vilikuwa vimefunguliwa katika majengo ya Serikali nchini kote na katika ofisi za ubalozi wa Afrika Kusini duniani kwa waombolezaji kusaini.
Maandalizi ya maziko ambayo yanatarajiwa kuchukua kama wiki mbili yanatarajiwa ‘kuisimamisha’ nchi hiyo yenye watu milioni 53.
Makadirio ya haraka haraka ya wageni watakaohudhuria mazishi wakiwamo wakuu kadhaa wa serikali, yanaashiria kuongeza mzigo katika sekta ya usafiri na huduma kwa Serikali ya Afrika Kusini, ambayo sasa italazimika kuimarisha ulinzi wa anga wakati wote wa kipindi hicho.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, vinavyoshiriki maandalizi ya mazishi, tukio hilo la siku kama 10 litachanganya mila za kimagharibi na za jadi za ukoo wa Mandela wa kabila la Wathembu.
Katika hatua fulani kuanzia siku ya kwanza hadi ya nne, CNN iliripoti kuwa wazee wa Kithembu watakusanyika kwa ajili ya sherehe ya kwanza inayoitwa ‘kufunga macho’ ama nyumbani kwa marehemu au ndani ya mochari ulimohifadhiwa mwili.
Baada ya sherehe hiyo, inaaminika mwili utatiwa dawa kuzuia kuharibika ndani ya mochari, katika hospitali ya kijeshi jijini Pretoria.
Hakuna tukio lolote rasmi linalotarajiwa kufanyika hadi siku tano ziishe pale ambapo waombolezaji watapata fursa ya kumuaga baba yao kipenzi wakati wa Ibada maalumu itakayofanyika katika uwanja huo ambao ulitumika kwa fainali za soka Kombe la Dunia mwaka 2010.
Kwa siku tatu baadaye, mwili wa shujaa huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi unatarajiwa kuwekwa katika majengo ya Serikali ya Union jijini Pretoria, ambako aliapishwa kushika urais Mei 10, 1994.
Kwa mujibu wa mila za Wathembu, atatakiwa kuzikwa mchana siku ya Jumamosi-kuna uwezekano maziko yakafanyika Jumamosi ya Desemba 14. 
Rais Obama alitangaza rasmi kuhudhuria mazishi ya Mandela aliyefariki dunia juzi usiku nyumbani kwake Johannesburg.
Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Washington, DC, ofisi ya Rais ilitangaza kuwa Obama atasafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria maziko hayo.
Akimzungumzia Mandela, Rais Obama alisema: “Alipata mafanikio makubwa zaidi ya ilivyotarajiwa kwa mtu yeyote na leo amerudi nyumbani. Madiba aliibadilisha Afrika Kusini na alituvutia sote-safari yake kutoka jela hadi urais inajumuisha juhudi za binadamu kubadilisha maisha yakawa bora zaidi.”
Obama alizuru Afrika Kusini Juni na kukutana na familia ya Mandela na kushindwa kuonana na kiongozi huyo aliyekuwa mahututi hospitalini. Akiwa Seneta, Obama mara nyingi alikuwa akiwasiliana na Mandela.
“Hatutaweza kuyaona tena ya mfano wa Mandela, hivyo tunapaswa kuishi kwa mfano wake na kufanya uamuzi bila chuki ila upendo,” alisema Obama.  Alisema mawazo na maombi ya familia yake na watu wa Marekani yako na familia ya Mandela.
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma na kupitia kwake, kwa mkewe  Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wa Afrika Kusini.
"Afrika Kusini, Afrika na dunia wamepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa karne ya 20 na 21. Tunaelewa uchungu walionao wananchi wa Afrika Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwanamapinduzi, mvumilivu na mstahimilivu," aliongeza Rais Kikwete.
Alimwelezea Mandela kuwa kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, kuhurumia na upendo uliomwezesha kuunganisha wananchi wa Afrika Kusini kuwa Taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu mwungwana anavyopaswa kuwa. Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake. Tuzidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi".
Kutokana na kifo hicho Rais alitangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana Desemba 6 hadi keshokutwa na aliagiza bendera zote zipepee nusu mlingoti kwa siku hizo tatu.
“Mungu alikuwa mwema kwetu sisi Waafrika Kusini kwa kutupa Nelson Mandela  kuwa Rais wetu katika kipindi kigumu sana katika historia,” alisema mshirika wake wa siku nyingi, Askofu Mkuu mstaafu Tutu.
Bibi wa miaka 70 aliwatia faraja waombolezaji nyumbani kwa zamani kwa Mandela katika barabara ya Vilakazi mjini Soweto jana.

Ernestina Matshaka alionekana akicheza kama kijana akifuatisha wimbo wa uhuru ukimhusu Mandela. “Sisi Waafrika tunapofurahi, tunaposononeka au kuomboleza huimba. Kuimba kunatufariji,” alisema.

“Nimepunguziwa mzigo kwamba Madiba amefariki dunia. Haikuwa haki kumtarajia aruke kutoka kwenye kitanda cha ugonjwa na kukimbia huku na huko kama mtoto wa kiume.”

Matshaka alisema atakuwa na furaha sana kama Waafrika Kusini watatulia wakati huu na kuheshimu mema aliyoyaacha Mandela. Kundi la vijana na wazee lilitiwa nguvu na Matshaka, likicheza na kuimba.

Maofisa wa Polisi wakiwa katika magari yapatayo 10 walikuwapo wakifuatilia huku mishumaa ikiwa imewashwa mbele ya nyumba yake hiyo na barabara zikifungwa..

Walinzi wanaolinda nyumba hiyo walisimika ubao mkubwa mweupe kwa ajili ya watu kuandika ujumbe wao.  Hata hivyo, ghafla nyimbo zilikatizwa na gari lililopita karibu likipiga wimbo wa Johnny Clegg wa ‘Asimbonanga isiZulu’ wenye maana ya “hatujamwona”.

Ingawa alidhoofu, Mandela alikuwa akikimbizwa na kutoka hospitalini katika miaka zaidi ya mitano, mara ya mwisho akipelekwa Juni 8. Awali alitibiwa tatizo la mapafu, lakini baada ya wiki tatu ilitangazwa hali yake kubadilika na kuwa mahututi.

Ingawa Serikali ya Afrika Kusini haikutangaza ukubwa wa tatizo lake kiafya, lakini vyanzo vya kuaminika vya habari vilisema ini na figo vilikuwa vikifanya kazi kwa asilimia 50 tu.

Vyombo vya habari Afrika Kusini viliripoti kwamba alikuwa akipumua kwa mashine huku figo zake zikisafishwa kila mara.

Baada ya kutangaziwa kifo hicho, wananchi waliingia mitaani huku wengine wakionesha wazi sura za majonzi huku wengine wakisherehekea wakiimba nyimbo kuonesha uzalendo.

Watu wa kada, rangi na dini tofauti waliimba kwa sauti kubwa pamoja, wakicheza na kupunga mishumaa karibu na nyumbani kwake alikofia.
Wengi waliimba: “Iko mikononi mwetu sasa,” wakimaanisha urithi aliouacha Mandela huku wengine wakijihisi kuwa sasa ni wajibu wao kuuendeleza.
Mamia wengine walipeperusha bendera za Afrika Kusini, wakipiga makofi na kutaja jina la Mandela kumkumbuka Rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia.

Wakati wa kesi yake mwaka 1964 Mandela alikamilisha utetezi wake akiwa kizimbani akisema: “Nimepambana dhidi ya utawala wa weupe, nimepigana dhidi ya utawala wa weusi.

Ninavutiwa na wazo la jamii iliyo huru na ya kidemokrasia ambamo watu wote wanaishi pamoja kwa amani na fursa sawa. Ni wazo ambalo natumaini kulitetea na kulifanikisha. Lakini kama itawezekana, ni wazo ambalo niko tayari kulifia.”

Hakika Mandela aliishi kwa wazo hilo na kulifanikisha. Alifanikiwa zaidi ya matarajio ya mtu yeyote. Leo, amekwenda nyumbani. Na tumepoteza mmoja wa watu wenye ushawishi, jasiri na hakika binadamu wema ambao kila mmoja wetu atapenda kuwa nao duniani hapa. Si wetu tena – ni wa zama.
“Waafrika Kusini wenzangu, mpendwa wetu Nelson Rolihlahla Mandela, Baba wa Taifa letu la kidemokrasia, ameondoka. Alifariki dunia kwa amani akiwa na familia yake saa 2.50 (saa 3.50 saa za Afrika Mashariki) usiku wa Desemba 5 nyumbani kwake Houghton,” alitangaza Rais Zuma na kuongeza: “Hivi sasa amepumzika. Amepumzika kwa amani.”

Jijini London, Uingereza, familia ya kifalme, watu mashuhuri na wanafamilia ya Mandela –wakiwamo mabinti zake wawili-walikuwa wakihudhuria maonesho ya filamu ya maisha ya Mandela ndipo walipopokea taarifa hizo za kusikitisha. Akizungumza kutoka ukumbi wa sinema wa Odeon, mtoto wa Malkia Prince William alisema: “Nilitaka kusema kwa kweli ni habari za kusikitisha na kuhuzunisha. Tumekumbushwa kile mtu asiye wa kawaida Nelson Mandela alichokuwa. Tuko pamoja kwa mawazo na maombi na familia yake.”

Haikuweza kueleweka mara moja kilichompata binti wa Mandela, Zindzi, ambaye alionekana mwenye furaha na aliyetulia akiingia katika ukumbi wa sinema na akaonekana kuzidiwa alipoingia ndani.

“Ni kitu kinachonifanya nijisikie furaha kwamba kile familia yangu ilichopitia na mchango wa baba yangu vimetambuliwa,” alisema Zindzi kuhusu filamu hiyo na kukutana kwake na familia ya kifalme. 

Mandela ameacha mjane Graca Machel, binti yake Makaziwe kwa mkewe wa kwanza na mabinti wawili Zindzi na Zenani.

Mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 pale mkewe alipomsaidia kuinua mkono wake kupungia umati wa watu.

Pamoja na kupata  matibabu ya saratani ya kibofu, maumivu ya tumbo na matatizo ya macho, tatizo kubwa la Mandela lilikuwa ni kupumua.
Aliharibika mapafu na kuugua kifua kikuu wakati akichimba chokaa akitumikia kifungo cha miaka 18 katika gereza la mateso la kisiwa cha Robben, nje ya Cape Town.

 Hali hiyo ilimfanya alazwe mara nyingi hospitalini katika muongo uliopita-na mara tano tangu Desemba mwaka jana.
Alipata matibabu ya matatizo ya kupumua, maumivu ya tumbo, mawe kwenye figo na Aprili aliondolewa maji kwenye mapafu.

Alizaliwa katika familia ya kifalme, katika ufalme wa Wathembu, mjini Transkeiin mwaka 1918.  Baba yake alikuwa na wake wanne, mama yake akiwa ni wa tatu. Alikuwa mtoto wa kwanza kwenye familia yao kwenda shule na alikuwa ni mwalimu wake aliyempa jina la Kiingereza la Nelson badala ya jina lake la awali la Rolihlahla.

Akiwa na miaka 19, alijiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare, ambako mara moja alianza kujihusisha na masuala ya siasa – au kuandaa migomo dhidi ya siasa.

Baada ya kukataa kufunga ndoa ambayo iliandaliwa kwa ajili yake na wazee wa kikabila, kwa kipindi kifupi alifanya kazi ya ulinzi mgodini na baadaye akajiunga na kampuni ya sheria ya Johannesburg.

Alianza kuishi katika mji wa weusi wa Alexandra na kuanza masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, ambako alikutana na wanafunzi wenzake ambao walikuja kuwa wanaharakati wa kisiasa baadaye; Ruth First, Joe Slovo na Harry Schwarz.

Katika miaka ya awali ya hamsini, Mandela alijiingiza zaidi katika upinzani wa ubaguzi wa rangi, yeye na mwanaharakati mwenzake Oliver Tambo walianzisha kampuni ya uwakili, wakitoa ushauri wa bei nafuu kwa wakazi wa Alexandra.

Mandela alivutiwa sana na Mahatma Ghandhi wa India, kwa kujihusisha na upinzani usiotumia nguvu. Lakini mwaka 1956, akiwa na wenzake 150 walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhaini.

Katika hukumu dhidi yao, walinusurika adhabu ya kunyongwa lakini wakakumbwa na kifungo cha  maisha jela. Alitumikia kifungo cha miaka 27, huku miaka 18 akitumika katika kisiwa cha Robben.

Ndoa yake na Winnie ilisambaratika baada ya kutoka jela na kuamua kumwoa Graca Machel, aliyekuwa mjane wa rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel.

HUYU NDIYE MTANGAZAJI WA BBC ALIYEMWAGA MACHOZI WAKATI AKITANGAZA TAARIFA ZA KIFO CHA MANDELA

BBC newsreader Huw Edwards fought back the tears as he broke the news of Nelson Mandela 039 s death
Mtangazaji wa BBC  Huw Edwards ametoa machozi wakati alipokuwa akitangaza taarifa za mapema kabisa (BREAKING NEWS) kuhusiana na  kifo cha Nelson Mandela. 
Sauti ya mtangazaji huyo mzoefu ilikuwa na mawimbi wakati akiwa
anatangaza matangazo ya moja kwa moja(LIVE) ndani ya  BBC News baada ya rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kutangaza kifo cha Mr Mandela.  

Mr Edwards alionekana na uso wa huzuni baada ya kutangaza habari  za kifo cha Mr Mandela ambaye amefariki akiwa na  umri wa miaka 95 baada ya kuungua kwa muda mrefu kwa sababu  ya matatizo ya mapafu.
Watu katika mtandao wa kijamii wa Twitter,walitoa maoni ya kumpongeza Mr Edwards kwa "kipaji" kwani alikuwa akifanya kazi licha ya kuangalia kama yeye alikuwa "anaumia ndani na kutoa machozi". 
Mtumiaji mmoja wa Twitter anaitwa Geraint Lloyd aliandika: "Huw Edwards unafanya kazi ngumu usiku wa leo,licha kwa kiasi gani ni wazi unamaanisha unachokifanya."  
Mwingine anayeitwa Glyn Morgan aliongeza: "Huw Edwards ni wazi umenigusa # bbcnews channel,wote tunatokwa na machozi."
   
Na Nicola Bitton pia aliandika: "matangazo ni mazuri,kwa kiasi kikubwa yamebebwa na muonekano wa kusikitishwa wa Huw Edwards ndani ya BBC News usiku wa leo, kwa dhati atasonga sana." 
Mtandao wa kijamii wa Twitter ulitawaliwa na maombolezo ya Mr Mandela, kwa kutawaliwa na #RIPNelsonMandela zilizovuma juu ya mitandao huo wa kijamii . 
  
Watu maarufu na wanamichezo kutoka duniani kote walitumia Twitter na mitandao mingine kama Facebook kutoa rambirambi zao baada ya kifo cha Mr Mandela.