JUU: Dk Conrad Murray. CHINI: Catherine Jackson. KATIKATI:
Michael Jackson. KULIA: Dk Charles Czeisler.
Imeelezwa hayati mfalme wa Pop duniani Michael Jackson alifikisha siku 60
bila kulala, na kumfanya awe mtu pekee kuwahi kufanya hivyo, mtaalamu wa
usingizi amedai.
Charles Czeisler, mtaalamu wa usingizi kutoka Chuo cha Tiba cha Havard, alisema
hajawahi kusikia mtu yeyote ambaye amefikisha siku 60 huku akilala macho wakati
akitoa ushahidi kwenye kesi ya kifo batili ya promota wa tamasha AEG Live.
Mama wa Michael Jackson, Catherine anaishitaki AEG Live, akidai ilishindwa
kumchunguza ipasavyo daktari binafsi wa mtoto wake, Conrad Murray na kushindwa
kugundua ishara za tahadhari kuhusu kudorora kwa afya yake.
Murray alitiwa hatiani kwa mauaji bila kukusudia mwaka 2011 baada ya kumpatia
Michael Jackson dozi ya nusukaputi.
Mama wa Jackson anaasa AEG Live ilimshinikiza Dk Murray kumpeleka mtoto wake
kwenye mazoezi lakini ilipuuza ishara za tahadhari na kushindwa kumpatia
msaada.
Lakini wanasheria wa AEG Live wanasema Jackson alimchagua na kumkodisha Murray
hivyo wakuu wao hawakuwa na jinsi ya kufahamu kuhusu matibabu hayo ya
nusukaputi yaliyokuwa yakiendelea nyumbani kwake.
Kama ilivyoripotiwa, mahakama hiyo ilielezwa na Dk Czeisler kwamba siku 60 za
unyweshwaji nusukaputi ambao Dk Murray anasema alimpatia Jackson ili kumtibu
kukosa usingizi hazikuwahi kutumiwa hapo kabla.
Dk Czeisler, daktari wa usingizi wa NASA na CIA, aliieleza mahakama hiyo kwamba
dawa hizo hazitibu kukosa usingizi na kuvuruga mzunguko wa kawaida wa usingizi.
Lakini zinawafanya wote wanaotumia kujisikia safi na kujihisi kama walipata usingizi
wa kawaida usiku.
Mahakama hiyo ilielezwa kwamba panya waliojaribiwa na wanasayansi walikufa
baada ya wiki tano za kukosa usingizi.
Watu ambao wanasumbuliwa na kukosa usingizi kwa vipindi virefu hudhoofika,
kupata wazimu na kuwa wenye wasiwasi.
Pia hupoteza uwiano na hamu ya kula, na wanaweza kuwa na madhara ya taratibu ya
kimwili na kisaikolojia.
Hizi ni dalili ambazo Jackson alisemekana kusumbuliwa nazo katika wiki zake za
mwisho. Maprodyuza wa onesho lake waliripoti kwamba alikondeana, mwenye wasiwasi
na msahaulifu mno, na alikuwa akisikika akiongea mwenyewe.
Kesi hiyo, ambayo imekuwa ikinguruma kwa wiki nane, inaendelea. Inatarajiwa
kuhitimishwa mwezi Agosti.
Jackson alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 50 Juni 25, 2009 baada ya
kutumia dozi ya nusukaputi aliyoagizwa na Dk Murray na kushindwa kupumua.
Murray alitiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia katika kifo cha Jackson na sasa
anatumikia kifungo cha miaka minne jela katika gereza la Los Angeles County kwa
kosa la kutoa dozi iliyosababisha mauti.
Anapinga hukumu hiyo, akidai kuwa Jackson ndiye anayehusika kwa kujizidishia
dozi yake mwenyewe.