Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RASIMU ya Tatu ya Katiba
mpya, inatarajiwa kuwekwa hadharani Jumatatu ijayo, wakati Kamati ya Uandishi
ya Bunge Maalumu la Katiba, itakapokuwa ikiwasilisha rasimu hiyo kwa wajumbe wa
bunge hilo.
Ratiba ya shughuli za
Bunge Maalumu la Katiba iliyopatikana jana bungeni hapo,
imeonesha kuwa
Sekretarieti ya Kamati ya Uandishi, ilipaswa kukamilisha kuandika Ibara za
Rasimu hiyo juzi.
Kuanzia jana, mpaka
Jumamosi ya wiki hii, ratiba hiyo inaonesha Kamati ya Uandishi
inatakiwa kufanya kazi ya
kuandika Rasimu hiyo na kuikabidhi
Kamati ya Uongozi
Jumapili wiki hii.
Baada ya kukabidhiwa kwa
Kamati ya Uongozi, Jumatatu Rasimu hiyo itawasilishwa
bungeni na baada ya
kuwasilishwa, wajumbe watapewa muda wa kutafakari Rasimu hiyo ya Katiba kuanzia
siku hiyo na kesho yake.
Jumatano na Alhamisi wiki
ijayo, mjadala wa Rasimu ya Tatu ya Katiba mpya utaanza
bungeni pamoja na uhakiki
wa Ibara zake kisha Kamati ya Uandishi itarejea kibaruani kufanya marekebisho
ya mwisho ya Ibara za Rasimu ya Mwisho ya Katiba.
Jumamosi ya wiki ijayo
Septemba 27, Kamati ya Uandishi itawasilisha Rasimu ya Mwisho ya Katiba
bungeni, ambapo Jumapili kamati za Bunge Maalumu la Katiba, zitajielimisha
kuhusu Rasimu ya Mwisho ya Katiba na taratibu za upigaji kura.
Kura ya kupata Katiba
inayopendekezwa, kwa mujibu wa ratiba hiyo, inatarajiwa kuanza kupigwa kuanzia
Jumatatu ya Septemba 29, mpaka Oktoba 2, mwaka huu.
Wakati mchakato huo ukiwa
katika hatua za mwisho, ule uoga wa kukosekana kwa
theluthi mbili za kura
kutoka Tanzania Bara za Zanzibar, uliosababishwa na kutokuwepo kwa baadhi ya
wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), umeanza
kuondoka.
Tayari Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, ameshatoa tamko kuonesha kuwa wajumbe wa Ukawa,
waliosusa wakitarajia kukwamisha kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa,
hawatakuwa na athari.
Kwa mujibu wa Dk Migiro,
idadi ya wajumbe wote walikuwa 630, na Ukawa waliosusa ni 130 tu ambao ni sawa
na asilimia 21 ya wajumbe wote. Kwa maana hiyo wajumbe waliobaki ni 500, sawa
na asilimia 79 ya wajumbe wote ambao ni zaidi ya theluthi mbili tayari.
Dk Migiro aliweka wazi
kuwa wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati yao, 125 wanatoka kundi la
201. Kwa Zanzibar, takwimu hiyo inaonesha wapo wajumbe 152 ambao kati yao 64
wanatoka kundi la 201.
Chanzo: HabariLeo







0 comments:
Post a Comment