Polisi
nchini Tanzania wamewakamata waganga wawili wa kienyeji baada ya mwanamke mmoja
mwenye ulemavu wa ngozi au Abino kuuwawa kwa kuchinjwa.
Moja
ya miguu yake pamoja na vidole vilinyofolewa baada ya shambulizi hilo la hapo
jana Jumanne katika mkoa wa Simiyu Kaskazini Mashariki mwa Tanzania. Kumekuwa
na visa vingi vya mauaji ya albino katika eneo hilo hapo awali.
Shirika
la kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi Albino la 'Under the Same Su'n
limeiomba serikali ya nchi hiyo kufuta vibali na shughuli zote za waganga wa
jadi kwa madai kuwa wao ndiyo chanzo cha kuuawa kwao.
Kuuawa
kwa mwanamke Munghu Lugata mlemavu wa ngozi toka kijiji cha Gasuma mkoani
Simiyu Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo kumeacha hisia na uchungu kwa walemavu
wengine waliopata mikasa hiyo.
Akizungumza
na mwandishi wa BBC Leonrad Mubali kwa uchungu na kilio, Mariamu Staford
mlemavu wa ngozi Albino amesema kwamba tukio la kuuawa kwa Munghu Lugata
mwanamke mwenye umri wa miaka 40 juzi linamkumbusha mkasa wake uliomkuta wa
kukatwa mikono yake yote, zaidi ya miaka mitano iliyopita na sasa anatumia
mikono ya bandia ya vyuma huku akisema malengo yake mengi yamekwama.
Albino
wamekuwa wakihangaishwa sana nchini Tanzania ambako baadhi ya watu wanaamini
kuwa dawa za miujiza zinazotengezwa kutokana na viungo vya miili yao zinaleta
bahati nzuri.
Mashambulizi
yamepungua katika siku za hivi karibuni lakini mauaji ya hivi punde yamepelekea
shirika moja la kutetea haki za Albino kutoa wito kwa serikali kupiga marufuku
waganga wote wa kienyeji.
Matukio
mengi ya maujia ya walemavu nchini Tanzania yamekuwa yakihusishwa na imani za
kishirikina huku waganga wa jadi wakihusishwa.
Mkoa
wa Simiyu ni moja katika maeneo kaskazini magharibi mwa Tanzania yenye matukio mengi
ya mauaji hayo.
Hivi
karibuni nchini Tanzania umezinduliwa mnara maalumu unaoitwa NITHAMINI, mnara
pekee duniani unaowakilisha kupinga mauaji ya albino huku Tanzania ikiwa ni
moja ya nchi yenye matukio mengi ya ukatili dhidi ya walemavu hao







0 comments:
Post a Comment