STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema upanuzi na uimarishaji wa miundombinu
ya usafari wa anga unaofanyika hivi sasa umelenga kuhakikisha kuwa
huduma za usafiri zinazotolewa Zanzibar zinakidhi viwango vya ubora wa
huduma hizo kimataifa pamoja kuzingatia viwango vya usalama
vinavyotakiwa.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema hayo leo wakati akizungumza na ujumbe wa Shirika la Kimataifa la
Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ulioongozwa na Katibu Mkuu wake Bwana Benjamin Raymond.
Aliuambia
ujumbe huo kuwa huduma za viwanja vya ndege na usafiri wa anga kwa
ujumla, kama ilivyo kwa nchi nyingine ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar
na ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua hatua
mbalimbali kwa nyakati tofauti kuimarisha sekta hiyo.
Alifafanua
kuwa mwenendo wa usafiri wa anga nchini unaonesha kuongezeka kwa abiria
mwaka hadi mwaka ndio maana Serikali imeamua kufanya upanuzi mkubwa wa
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na kwamba imo mbioni kuanza
upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ili nao uweze kutoa huduma wakati
wote.
“hivi
sasa tunapokea watalii wapatao 200,000 kwa mwaka lakini matarajio yetu
ni kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2015 lakini hata hivyo baada ya
upanuzi wa uwanja tunatarajia abiria kuongezeka kufikia kati ya milioni
1.5 na milioni 2”Dk. Shein alifafanua.
Kwa
hiyo alieleza kuwa ziara ya ujumbe huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa
utapata fursa kuona jitihada za Serikali katika kuimairsha sekta ya
usafiri wa anga Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuongeza ushirikiano
kati ya ICAO na nchi yetu.
“Ziara
yenu imekuja wakati huu muhimu tunapopanua miundombinu ya uwanja wetu
wa ndege wa Zanzibar na tungependa kuona ICAO inasaidia kwa namna
mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa viwanja vyetu ikiwemo kuijengea
uwezo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na kutupatia vifaa vya kutolea
huduma katika viwanja hivyo kwa manufaa ya watumiaji wote wa usafiri wa
anga ”Dk. Shein alisisitiza.
Dk.
Shein aliuhakikishia ujumbe huo ambao ulijumuisha pia Mkurugenzi wa
ICAO Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bwana Mashesha Belayneh
kuwa Zanzibar imejidhatiti kuhakikisha kuwa usafiri wa anga unakuwa
salama na wa raha wa watumiaji wake na ili kufikia lengo hilo ipo haja
kwa ICAO kuzidisha ushirikiano na Zanzibar.
Wakati huo huo Katibu
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) Bwana Benjamin
Raymond ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa shirika
lake litaendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha kuwa hali ya
usalama wa anga nchini unazidi kuimarika.
Amesema
ujumbe wake umefika Zanzibar kuangalia jinsi shirika hilo linavyoweza
kushirikiana na Zanzibar kukabiliana na changamoto zinaoendana na
kupanuka kwa haraka kwa sekta ya usafiri wa anga ikiwemo suala la
usalama wa usafiri huo.
Alieleza
kuwa kuna kila dalili za usafiri wa anga kupanuka kwa haraka Zanzibar
kutokana na kupanuka kwa sekta ya utalii pamoja na uwekezaji unaovutia
watu kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Kwa
hiyo alieleza kuwa anaichukulia kwa uzito mkubwa rai aliyotoa
Mheshimiwa Rais ya kutaka shirika hilo kufanyakazi kwa karibu na
Serikali ya Zanzibar katika kusaidia kuimarisha usalama wa usafiri wa
anga nchini.
Mazungumzo
hayo yalihudhuriwa pia na viongozi wa Wizara ya Miundombinu na
Mawasiliano wakiongozwa na Waziri wake Mhe Rashid Seif Suleiman,viongozi
wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na viongozi wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Zanzibar(ZAA).
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822







0 comments:
Post a Comment