Na Ohman Ame OMPR.
Mfuko
wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD }umeombwa kuendelea kuunga
mkono Sekta ya Kilimo Zanzibar katika njia ya kuwajengea uwezo
wazalishaji wa Sekta hiyo mama ya uchumi kupitia mfumo wa Teknolojia ya
kisasa.
Ombi
hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi hapo Serena Hoteli Shangani Mjini Zanzibar wakati wa dhifa maalum
iliyoandaliwa kwa ajili ya Ujumbe wa Bodi ya Utendaji ya Mfuko huo
uliofanya ziara maalum kukagua miradi mbali mbali inayofadhiliwa na
Taasisi hiyo ya Kimataifa.
Balozi
Seif alisema Sekta ya Kilimo Zanzibar bado inaendelea kukabiliwa na
changa moto kadhaa ambazo zinaweza kupunguwa iwapo msukumo wa Mfuko wa
IFADI utaongeza kasi ya kitaalamu katika kusaidia sekta ya Kilimo
Nchini.
Alielezea
matumaini yake kwamba juhudi zinazochukuliwa na Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Kilimo zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
umaskini, njaa na kuongeza mara dufu uzalishaji wa chakula.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba Serikali kwa kushirikiana na Taasisi tofauti
za ndani na nje ya Nchi imekusudia kuimarisha uzalishaji wa mazao ya
chakula na matunda ili kuwapunguzia mzigo wananchi hasa wanaoishi sehemu
za Vijiji.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wajumbe wa Bodi hiyo Tendaji
ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo kwa uamuzi wao wa
kutembelea miradi inayoifadhili hapa Tanzania kitendo ambacho kitaongeza
upeo wa ushirikiano kati ya Uongozi huo na Serikali zote mbili.
Mapema Mkuu wa Bodi hiyo yenye Makao
Makuu yake Nchini Italy Dr.Yaya Olaniran alisema ujumbe huo ulipata
fursa ya kuona hali halisi ya miradi mbali mbali inayofadhiliwa na mfuko
huo pamoja na kukutana na wakulima ambao ndio wahusika wakuu wa miradi
ya Mfuko huo.
Dr. Yaya alisema Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Kilimo { IFAD } utaendelea kuunga mkono Serikali zote mbili
Nchini Tanzania katika sekta ya Kilimo ikijikita zaidi katika
kuwajengea uwezo wakulima pamoja na jumuiya za Kilimo ili zifikie hatua
ya kujitegemea kiuzalishaji badala ya kusibiri misaada.
“ Ushirikiano wetu uliopo kati ya IFAD
pamoja na SMT NA SMZ ndio sababu ya msingi iliyochangia Mfuko huo
kuchangia harakati za maendeleo ya wakulima katika maeneo mbali mbali
Nchini Tanzania “. Alisema Dr. Yaya Olaniran.
Naye
Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } Kanda
ya Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika Bwana Perin Saint Ange akitoa
shukrani kwa niaba ya Ujumbe huo alisema Visiwa vya Zanzibar vina
rasilmali nyingi ambazo iwapo zitajengewa miundo mbinu imara zinaweza
kunyanyua maisha ya Wananchi pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Bwana
Perin alizitolea mfano rasilmali zilizomo ndani ya Bahari ya Tanzania
kwamba zinafursa ya kukomboa maisha ya wavuvi wengi waliomo pembezini
mwa bahari hiyo ambapo wengi kati yao hujishughulisha na kazi hiyo
wakitumia vifaa duni visivyohimili masafa ya bahari kuu.
Dhifa
hiyo fupi kwa Wajumbe wa Bodi Tendaji ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo
ya Kilimo { IFAD } ilijumuisha pia baadhi ya Maafisa na watendaji wa
Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar.







0 comments:
Post a Comment