Monday, September 9, 2013

Dk Shein aahidi neema kwa wafanyakazi



 
Na Mwandishi Maalumu, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imewahakikishia watumishi wa sekta ya afya kuwa changamoto zinazowakabili, ikiwemo maslahi yao, zinatafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua ili waweze kutoa huduma vizuri kwa wananchi.


Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana wakati akifungua  Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya kilichoko Mbweni, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.


Alisema changamoto kubwa inayoikabili Serikali katika kutekeleza azma hiyo ni ukosefu wa fedha jambo ambalo alikiri kuwa si kwa Serikali yake tu bali katika nchi nyingi duniani.  

Dk Shein alisema Serikali itajitahidi kuhakikisha ajira kwa wanafunzi wanaohitimu mafunzo katika sekta ya afya hazicheleweshwi na kwamba zitafanyika kwa kuzingatia muundo wa utumishi kwa watumishi wa sekta hiyo.
 
Rais wa Zanzibar alitangaza uamuzi wa Serikali wa kukiweka chuo hicho chini ya Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Sambamba na kutangaza uamuzi huo, Dk Shein ametoa mwito kwa Wizara na Uongozi wa Chuo cha Afya kukubali mabadiliko vinginevyo watabaki nyuma wakati wengine wakisonga mbele.

Naye Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo matatu ambayo moja ni la darasa na mawili mabweni ya wanafunzi wa kike kunadhihirisha namna hatua kwa hatua chuo hicho kinavyoimarika.

 

0 comments:

Post a Comment