Imeelezwa kuwa Zanzibar inaweza kukumbwa
na Janga la uhaba wa Maji ifikapo mwaka 2015 kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo watu kuharibu Vyanzo vya Maji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Mohammed Aboud ameeleza hayo alipokuwa akizindua Kongamano la Kitaifa
la kukabiliana na Maafa lililofanyika Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kuna Tafiti
zimefanywa na kuonesha hatari inayoikabili Zanzibar katika
upatikanaji wa Maji na kwamba juhudi binafsi zinahitajika ili kukabiliana na
hali hiyo.
Aboud amesema Wasomi na Wataalam kwa
ujumla wanapaswa kufahamu hali hiyo na kuisaidia Serikali katika kukabiliana na
Upungufu huo badala ya kukaa kimya na kulaumu.
“Wasomi wamekaa kimya sana hawatoi
ushauri wa kitaalamu kwa Serikali juu ya nini kifanyike ili kuijengea uwezo
Serikali na Jamii kwa ujumla kukabiliana na Majanga ” Alifafanua Aboud.
Ametolea Mfano wa Zao la Nazi
linavyoendelea kupotea katika Visiwa vya Zanzibar na kusema kuwa Wataalamu
wameshindwa kuja na namna bora ya kupata Minazi bora inayozalisha
zaidi na kuchukua eneo dogo kuliko Minazi iliyopo.
Aidha Waziri Aboud
amesisitiza Idara ya Maafa kwa kushirikiana na wadau
wengine kuendelea kutoa Elimu ya kukabilaiana na
Majanga kwa jamii ili kupata jamii salama.
“Ndugu wadau Elimu ni Muhimu kwa
wananchi kuanzia ngazi ya chini hadi juu,kwa kukosekana Elimu ya Majanga baadhi
ya wakati hata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanakuwa wagumu kupitisha Vifungu
vya Bajeti za Idara,yote ni kiashirio cha uelewa mdogo juu ya Majanga”
Aliongezea Aboud.
Awali akimkaribisha Waziri Aboud,
Mkurugenzi wa Idara ya Maafa alisema licha ya kukabiliwa na Changamoto
mbalimbali Idara yake imejipanga vyema kuhakikisha inafanya majukumu yake
ya msingi ikiwemo kukabiliana na Maafa.
Amesema kwa Sasa Idara ya Maafa ina
mpango wa kuainisha maeneo hatarishi katika Ramani ili kusaidia
ufahamu na namna ya kuweza kukabiliana na maafa pale yanapotokea.
Kongamano hilo la kitaifa la kukabiliana
na maafa limendaliwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
Zanzibar ambapo kwa siku mbili Washiriki kutoka Taasisi mbalimbali
za Serikali na Binafsi watajadili na namna bora ya kukabiliana na Majanga
Zanzibar.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR 26/06/2013
0 comments:
Post a Comment