Sunday, June 23, 2013

TABOA WALIA NA WAMILIKI WA NOAH



Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimewashukia baadhi ya viongozi wa serikali hasa ngazi za mikoa kuwa ni miongoni mwa wamiki wa magari aina ya Noah, ambayo hayana uwezo wa kubeba abiria kwa mujibu wa sheria.

Mbali na hatua hiyo TABOA imemuomba Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, kufanya ukaguzi maalum ili kuweza kubaini hali ambayo imekuwa ikihujumiwa na viongozi hao kwa kupinga agizo la Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu, ilieleza kuwa hatua ya viongozi wa serikali katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ya kuungana na wamiliki wa magari ya Noah inatia mashaka ikiwemo ya kutaka wabebe abiria zaidi ya saba kinyume cha sheria.

Mrutu, alisema sheria ya usafirisha iliyowekwa na SUMATRA imeweka wazi namna ya ubebaji wa abiri kwa magari hayo ya abiria lakini baadhi ya viongozi wamekuwa wakiunga mkono hoja ya kutaka gari hizo zitembe kilometa zaidi ya 50.

“TABOA inasikitishwa sana na hatua ya hatua ya baadhi ya viongozi wa serikali ambao wameonekana wazi kutaka kupinga sheria halali ya
SUMATRA ya namna ya kubeba abiria. Haiwezekani katika hili wao wawe mstari wa mbele katika hili la uvunjaji wa sheria hii halali.

“Ni wazi Noah hazina leseni ya biashara lakini kwa Mkoa wa Arusha Mkuu wa Mkoa Magesa Mulongo ametoa agizo magari haya yaruhusiwe kufanya safari zake sehemu zozote ile bila kujali  ya umbali na idadi ya abiria.

“Hata huko zilipotengenezwa Japan mwisho wa kubeba ni watu saba iweje hapa Tanzania. Kuna picha inayojengeka hapa kwani hata katika kikao kilichofanyika Juni 19, mwaka huu mkoani Kilimanjaro wenye magari haya wamekuwa na jeuri kuliko SUMATRA kuna nini hapa,” alisema na kuhoji Mrutu.

Katibu Mkuu huyo wa TABOA alisema kuwa ruhusa iliyotolewa na Waziri Mwakyembe kuna baadhi ya viongozi wa ngazi ya mikoa wanataka kuitumia vibaya huku wenye mabasi yanayobeba abiria kuanzia 10 hadi 65 wao wakiendelea kubanwa pekee.

Alisema vitendo vya wabunge na baadhi ya wakuu wa mikoa kuunga mkono jambo hilo huku wakiwa na shinikizo kubwa la kutaka watu hao kutokata leseni ni kwenda kinyume na sheria za nchi.

“Ikiwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro hawa wenye Noah wanataka kuvunja sheria hali ya kuwa wamiliki wa mabasi hatutakubaliana na hali hii hata
kidogo. Hivyo  tunamtaka Waziri Mwakyembe aingilie jambo hili la
uvunjivu wa sheria kwa makusudi,” alisema.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment