TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
22/06/2013
MAANDAMANO
YA AMANI YA CHAMA CHA WANANCHI CUF,
TAREHE 29
JUNI 2013.
Waheshimiwa waandishi wa habari, kwa
niaba yangu binafsi na kwa niaba ya uongozi wote wa kitaifa wa Chama chetu,
naomba kuchukua fursa hii kuwakaribisha Ofisi Kuu ya chama ili tupate fursa ya
kuzungumza nanyi na kwa maana hiyo kuzungumza na watanzania kupia kwenu ili
ujumbe uliokusudiwa na chama uweze kuwafikia wananchi popote pale walipo.
Tumewaita leo tarehe 22 Juni 2013
tukiwa na agenda moja kuu nayo ni kuwaeleza kwamba Chama cha Wananchi CUF
kimeandaa Maandamano ya Amani siku ya tarehe 29 Juni 2013 maandamano ambayo
yataanzia eneo la Buguruni kituo cha Mafuta saa nne kamili asubuhi, kupitia
barabara ya Uhuru, Mnazimmoja, Bibi Titi, Posta mpya , Aridhi hadi Ikulu.
Maandamano hayo ambayo yataongozwa na
Mwenyekiti wa Chama taifa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, yanatarajiwa kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania au mwakilishi wake, na kwamba yanalengo la kufikisha
malalamiko ya wananchi kutokana na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na jeshi
la polisi na jeshi la wananchi ambalo kimsingi taifa letu linaelekea mahali
pabaya.
Waheshimiwa waandishi wabari,
mtakumbuka tarehe 15 Juni 2013 wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema
wakihitimisha mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata nne
za Arusha, palitokea mlipuko wa bomu uliopoteza maisha ya wananchi wane kwa
mujibu wa taarifa za polisi na wengine wengi kujeruiwa vibaya.
Kwa kuwa jambo hili lipo katika hatua
za uchunguzi, Chama cha CUF hakikusudii kuingilia uchunguzi unaoendelea lakini
tunataka kufikisha ujumbe kwa rais kwamba hii si mara ya kwanza kuundwa kwa
tume mbalimbali za uchunguzi hapa nchini. Kinachotusikitisha ni kuwa hata mara
baada ya uchunguzi huo, hakuna ripoti inayotolewa hadharani kuonyesha chanzo cha
tukio, wahusika na hatua zilizo au zinazotarajiwa kuchukuiliwa.
Tutamtaka Mheshimiwa rais kuhakikisha
ripoti ya uchunguzi itokanayo na maafa yaliyotokea Arusha iwekwe wazi na
serikali iwachukulie hatua stahiki wale wote watakaobainika kuhusika na tukio
hilo ili iwe funzo kwa wengine au wale wenye kuwa na malengo yanayofanana na
hayo kwa kuwa Tanzania ni yetu sote na haitowezekana watu wachache wayachezee
maisha ya watu kwa sababu ya kukidhi matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa
jamii.
Maandamano pia yanalenga kuishinikiza
serikali kukomesha vitendo vya kinyama, vitendo vya kijangili vinavyofanywa na
Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwakamata, kuwatesa, na
kubaka wananchi wasio na hatia wa Mkoa wa Mtwara na hasa wanaoishi katika
wilaya za Mtwara Mjini, MtwaraVijijini, na Newala huku baadhi yao wakichomewa
nyumba zao moto na wengine wakiporwa mali zao.
Waheshimiwa waandishi wa habari,
mtakumbuka hivi karibuni pamekuwa na fukuto la suala la gesi katika Mkoa wa
Mtwara ambapo baadhi ya maafisa wa Serikali wamekuwa wakipotosha madai ya
wananchi ikidaiwa kwamba wananchi wa mkoa huo wamesema hawako tayari kuona gesi
yao inatumiwa na wananchi wengine kinyume na wale wa mikoa ya Lindi na Mtwara
jambo ambalo si kweli lakini wanayafanya haya ili kuwajengea chuki dhidi ya
watanzania wengine ionekane kwamba wananchi wa Mtwara na Lindi ni wabinafsi na
wasioitakia mema nchi yetu.
Madai ya wananchi wa Mtwara
yanatokana na uzoefu waliokuwa nao katika maeneo yote ambapo pana miradi
ya kimaenedeleo itokanayo na maliasili
ya nchi, maeneo hayo yamekuwa masikini na watu wachache wamekuwa wanatajirika,
walichotaka kufahamu wananchi watanufaikaje na uwepo wa gesi katika maeneo yao
kabla ya kuinufaisha nchi mzima kwa kuwa wao ndiyo watakuwa wa kwanza
kuathirika ikiwa patatokea hitilafu yoyote itokanayo na uchimbwaji wa gesi
hiyo.
Leo tunaweza kujifunza kutokana na
uchimbaji wa Dhahabu Geita (GGM), uchimbaji wa Almasi Mwadui Shinyanga, Mgodi
wa Dhahabu wa North Mara, Nyamongo na maeneo mengine mengi, nini hali ya maisha
ya wananchi wa maeneo hayo.
Pamoja na upotoshwaji wa makusudi
uliofanywa na unaoendelea kufanywa na watendaji wa serikali juu ya suala la
gesi ya Mtwara, inashangaza hata Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambalo
lilionekana awali kutenda haki kwa wananchi wa Mtwara baada ya wananchi kukosa
imani dhidi ya Polisi kutokana na wizi
na uporaji wa mali za wananchi huku wakichoma moto baadhi ya maduka kwa lengo
la kuhalalisha vitendo vya hujuma pamoja na kuchoma moto soko la Nkana Read,
Jeshi lililojijengea heshima kwa jamii nalo limeanza kuingia mkumbo wa kuwatesa
raia bila makosa.
Mwanzoni mwa wiki hii Mkurugenzi wetu
wa siasa wa wilaya ya Mtwara Mjini Mhe. Saibogi ambaye pia ni mwenyekiti wetu
wa serikali ya Mtaa alitekwa na wanajeshi na kumpeleka katika Kambi yao iliyopo
barabara ya kwenda Nanyamba ambapo walimvua nguo na kumpiga mijeredi usiku
kucha bila hatia na kumuachia asubuhi yake huku wakiahidi kuwakamata viongozi
wengine wa CUF ili kutoa funzo kwa wale wanaopigania haki za wananchi.
Matukio ya namna hii si ya kuyafumbia
macho na yanatengeneza serikali yenye kiburi isiyotokana na maamuzi ya raia.
Maisha ya namna hii hayawezi kuendeshwa katika nchi inayojiita huru kama yakwetu na badala yake mambo haya
yanatukumbusha enzi za utawala wa kikoloni ambpo CUF kamwe hatupo tayari
kuruhusu vitendo vya kishenzi kuona vinafanyika nchini petu.
Tulikianzisha Chama hiki kwa
madhumuni ya kuwaunganisha watanzania wote popote walipo, bila kujali itikadi
zao, waweze kukataa aina yoyote ya uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji, ubaguzi
na udhalilishaji wa kisiasa au kiuchumi.
Aidha tuna dhamira ya kulinda,
kutekeleza na kuzienzi haki za Binadamu pamoja na kuinua uchumi wa nchi kwa
siasa zitumikie uchumi badala ya uchumi kutumikia siasa kama inavyofanyika hivi
sasa. CUF tunaamini katika siasa za ustaharabu ambazo zitatuwezesha kuwa na
jamii salama yenye mshikamano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu, lakini
wenzetu wanatumia upole wetu na ustaharabu wetu kutufanyia vitendo vinavyokiuka
utu wa mtu na hatimaye kila aliyepewa mamlaka ya kuongoza sehemu ya nchi yetu
anageuka kuwa mfalme na kuamrisha kamata Yule, mpe kesi Yule na mwache Yule.
Uvumilivu wetu usiwe mtaji kwa CCM na serikali yake kutufanya watakalo, nasi ni
binadamu.
Waheshimiwa waandishi wa habari,
maandamano yetu yanalenga pia kuitaka serikali kuwasikiliza wananchi wa Mtwara
kwa kukaa nao chini, kujua hoja zao na kutoa ufafanuzi pale patakapobidi, sisi
tunaamini wanazo hoja za msingi na wakisikilizwa serikali itaona namna ya
kuzifanyia kazi hoja hizo badala ya kukurupuka na kutoa kauli za kibabe eti
hawa wanachochewa na vyama vya siasa au pana watu wasioitakia mema nchi ndiyo
wanachochea, kauli hizi zinajenga chuki na zanakosa uzalendo wa taifa.
Haiwezekani hao wanaojiita ndiyo wazalendo halisi wawe wanaifidi nchi alafu
tuendelee kukaa kimya kama vile wananchi wa kusini ni watu wasioweza kufikiri
na kupambanua baya na zuri.
Wakati wananchi hawa walipopeleka
maombi yao kupitia kwa Mhe. Mohamedi Habibu Mnyaa Mbunge wa Mkanyageni, ilikuwa
nafasi nzuri kwa serikali kuweza kusikiliza maombi yao na kutoa maamuzi, badala
yake siasa zikatumika, maombi yakakataliwa leo Bunge linaunda kamati ya
uchunguzi iende mtwara wakachunguze nini ikiwa tayari hoja zao zilikataliwa?
Ieleweke kuwa nchi yetu itajengwa na
watanzania wenyewe kwa kushirikiana na kusikilizana. Amani ya kweli itapatikana
ikiwa haki itaonekana kutendeka kwa jamii yote. Waheshimiwa waandishi wa
habari, haya ni sehemu tu ya mambo ambayo tunakusidia kumfikishia rais wetu ili
aweze kuyafanyia kazi.
Mungu Ibariki CUF, Mungu ibarika
Tanzania.
Imetolewa na
Shaweji Mketo,
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi
na Siasa,
tarehe 22 Juni 2013.
0 comments:
Post a Comment