Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba huo jijini Dar es Salaam jana,
Kiongozi wa Orijino Komedi, Seki David alisema mkataba huo umewapa maslahi
mazuri wasanii wa kikundi hicho na kuwawezesha kufanya kazi zao kitaalamu.
Hata hivyo, alikataa kutaja kiasi cha fedha walichopata kwa kuingia
mkataba huo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwakilishi wa Rockstar 4000, Christine
Mosha alisema Kampuni ya Nexus imenunua haki zote za usimamizi wa biashara na
uongozi wa kundi hilo, lengo likiwa ni kuboresha kazi zao na kuwatafutia masoko
nje ya nchi.
Mosha alisema wanakusudia kuzifanya kazi za kundi hilo ambalo linaonesha
vichekesho vyake kupitia televisheni ya TBC1 kuonekana katika nchi nyingine za
Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Aliainisha majukumu yake kuwa ni pamoja na uboreshaji na uandaaji wa
vipindi vya Orijino Komedi pamoja na kukuza vipaji vya wasanii hao kupitia kazi
zao nyingine wanazozifanya.
Alisema wanakusudia kurusha vipindi hivyo katika televisheni mbalimbali
barani Afrika, na kwa kuanzia wataweka vichwa vidogo vya habari vya lugha za
Kiingereza na Kifaransa na hatimaye kuwawezesha kutengeneza programu zao kwa
Kiingereza.
Aidha, alisema ndani ya mkataba huo, wasanii wa Orijino Komedi watapata
nafasi ya kufanya kazi na wasanii wakubwa Afrika na nje ya Bara la Afrika ambao
wana mikataba ya kazi na Rockstar 4000.
Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mkataba huo, wasanii wa
Orijino Komedi wameelezea kuridhishwa na mkataba huo ambao pamoja na mambo
mengine, unalenga kuendeleza vipaji vya wasanii hao ili vifikie kiwango cha juu
cha ufanisi ndani ya Afrika na kimataifa kwa jumla.
0 comments:
Post a Comment