Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MSIBA wa msanii nyota wa uchekeshaji
hapa nchini, Hussein Mkiety, maarufu kama 'Sharomilionea' umegusa hisia za
wengi, huku King Majuto akikimbizwa Hospitali baada ya kushikwa na presha,
hivyo kutishia usalama wake.
Mtoto wa King Majuto, Hamza Majuto,
aliimbia HANDENI KWETU kuwa hali ya baba yake inaendelea vizuri kutokana na
kuumizwa zaidi na msiba wa Sharomlionea anayetamba katika ulingo wa filamu na
muziki hapa nchini.
Msanii huyo alikufa
jana saa mbili za usiku Maguzoni, kilimita chache na kijijini kwao Lusanga,
wilayani Muheza mkoani Tanga, baada ya gari lake alilokuwa akisafiria lenye
namba za usajili T478 BVR Toyota Harrier kupinduka na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga,
Constantine Masawe, alikiri kutokea kwa msiba huo na kusema kuwa mwili wake
umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, Muheza, mkoani Tanga kwa taratibu za
mazishi zinazopangwa na familia yake.
![]() |
| Hili ndilo gari alilopatanalo ajali Sharomilionea |
“Marehemu alikufa majira ya saa mbili
za usiku kwenye barabara ya Segera alipokuwa anatoka Dar es Salaam kwenda
Muheza, hivyo mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, huku gari lake
likihifadhiwa pia kwasababu haliwezi kutembea,” alisema Masawe.
Taarifa za kifo cha msanii huyo
aliyeibukia hivi karibuni na kufanya vema katika ulingo huo zilianza kuzagaa
saa tatu za usiku, ikiwa ni dakika chache baada ya kufariki katika ajali hiyo
ya kusikitisha kwa nyota huyo.
Katika mitandao yote ya kijamii kuanzia
saa tatu za usiku zilizagaa habari zake, huku kila mmoja kiwa na hisia tofauti
zilizotokana na madai ya kifo cha msanii huyo, ambaye baadaye jeshi la Polisi
lilithibitisha kwa kupitia Kamanda wake, Masawe.
Sharomilionea ameshacheza filamu nyingi
za uchekeshaji na kujipatia sifa kubwa, ikiwamo ile ya Sharo Millionea, Imekula
Kwako, Jini Mahaba, Porojo na nyinginezo zinazofanya vyema katika tasnia ya
filamu nchini.
Katika filamu ya Jini Mahaba,
Sharomillionea anayetamba pia kwa msemo wake wa ‘Umebug Men’, anacheza kama mtu
maarufu anayekwenda kujitambulisha kwa wake zake (Kingwendu) na kushangazwa na
hali zao za maisha.
Sharomillionea anamshangaa mama yake
mkwe anavyochambua mboga za majani wakati yeye sio utaratibu katika maisha
yake. “Huyu ndio mama yako Men? Mbona anachambua majani,” aliuliza huku
anakunja mdomo wake na kujifuta uso.
Maneno hayo yanamuumiza mama yake mkwe
na kuamua kumuita mume wake (Kingwendu) na kuja kushangaa Sharobalo alivyokuwa
katika mueneko wa super Star na kujikuta akipagawa alipoanza kukejeliwa na mkwe
wake.
Mbali na filamu hiyo ya Jini Mahaba,
mkali huyo pia ametamba katika filamu nyingi pamoja na nyimbo mbili alizorekodi,
huku pia akililiwa na wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake, mara baada
ya kuibuka kisanii.
Wasanii wengi waliozungumzia kifo cha
Sharomillionea wakiongozwa na Steve Nyerere, walionyeshwa kuchanganyikiwa kwa
msiba wa msanii aliyeanza kutokea peupe na kutamba mno katika sanaa ya
uchekeshaji.
Sharomillionea aliyetokea katika ubavu
wa nguli wa vichekesho nchini, King Majuto, anazikwa kesho Jumatano, kijijini
kwao Lusanga, huku wasanii wengi wakitarajia kuhudhuria msiba na mazishi ya nyota
huyo aliyeipenda pia nyumbani kwao Muheza.








0 comments:
Post a Comment