Rais Jakaya Mrisho Kikwete akinyanyua juu kitabu baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa
na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)
iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.Picha na IKULU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na vijana baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)
iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.

Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na msanii wa vichekesho ambaye pia ni
mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili Emmanuel Mgaya maarufu kama
Masanja Mkandamizaji baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa
na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014
KUSOMA HOTUBA YA RAIS BOFYA HAPO CHINI
============= ==========
HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
WAKATI WA UZINDUZI WA SERA YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA MAADILI NA UCHUMI TANZANIA
(MVIMAUTA), KWENYE UKUMBI WA BCIC, MBEZI BEACH, TAREHE 15 FEBRUARI, 2014
Baba
Askofu
Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission
International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa
Kizazi Kipya;
Mheshimiwa
Sadiq Meck Sadiq, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Askofu
Michael Peter Imani, Mwangalizi wa Makanisa ya WAPO Mission International,
Kanda ya Dar es Salaam na Pwani;
Maaskofu
Waangalizi wa Wapo Mission;
Ndugu
Waumini;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani
kwa Mwaliko
Nakushukuru
sana Baba Askofu Mkuu Sylverster Gamanywa na viongozi wenzako wa Wapo Mission
International kwa kunialika na kunishirikisha
katika tukio hili la kihistoria la kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya
Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA). Nakushukuru
kwa Risala ambayo imeelezea kwa ufasaha malengo na madhumuni ya MVIMAUTA na
jinsi mlivyojipanga kuyatekeleza na nini mnachotegemea Serikali ifanye kusaidia
utekelezaji wake. Napenda kuchukua
nafasi hii kukupongeza kwa dhati kwa ubunifu wako na kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya
wewe na Kanisa lako la kulea vijana wawe raia wema na wenye manufaa kwa familia
zao, jamii na taifa kwa jumla.
Hii
ni mara ya pili kwangu kushuhudia matunda ya ubunifu wako na kazi njema
inayofanywa na WAPO Mission International.
Mara ya kwanza ni mwaka 2010 mliponishirikisha katika uzinduzi wa Mpango
wa Kizazi Kipya Tanzania. Matokeo ya
Mpango ule ni kuanzishwa kwa Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania
ambao sera yake ndiyo hii tunayoizindua leo.
Nasema hongera sana Baba Askofu Mkuu na hongereni sana viongozi na
waumini wa WAPO Mission International.
Sera
ya MVIMAUTA
Ndugu
Baba Askofu Mkuu;
Napata
faraja ya pekee kuona kuwa mpango huu sasa umewekewa mkakati madhubuti wa
utekelezaji ili malengo yake yaweze kufikiwa.
Sote tumekusikia ukieleza kwa ufasaha maudhui ya sera na mikakati ya utekelezaji
wake. Ni ukweli ulio wazi kuwa ni Sera
nzuri na hakuna mpenda maendeleo wa kweli anayeweza kubeza au kukataa kuwaunga
mkono. Jambo mnalokusudia kufanya ni
jema kwa nchi yetu na la manufaa kwa vijana ambao ndiyo taifa la leo na
kesho. Mnalenga kusaidia kundi muhimu
linategemewa sana na familia zao, jamii na nchi yetu kwa jumla. Kundi ambalo bahati mbaya linakabiliwa na changamoto
nyingi za kimaadili na kimaisha. Lakini
changamoto ni fursa za aina yake pia kwani changamoto hupanua mawazo ya watu. Changamoto huwafanya watu kuwa wabunifu
katika kutafuta majawabu. Baba Askofu na
viongozi wenzako mmefanya kile kinachostahili kufanywa. Hongereni sana.
Mmelitimiza vyema jukumu la
wazazi, familia, jamii na viongozi wa dini kuwapatia watoto na vijana malezi
mema ili waweze kuzikabili na kushinda changamoto za kimaadili. Najua ni kazi ngumu hasa katika dunia ya leo
ya utandawazi inayoongozwa na teknolojia za kisasa za habari na mawasiliano. Hatuna budi kuifanya kazi hiyo, tena tufanye kwa
umahiri na kushinda. Tukishindwa
tutakuwa tumepata hasara kubwa kwani tutakuwa na vijana wasiokuwa waadilifu
jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo na ustawi wa familia, jamii na taifa. Na sisi lazima tuwe wabunifu tutumie
utandawazi huo huo na teknolojia hizo hizo kuwajenga vijana wetu wawe na
maadili mema. Natoa pongezi nyingi kwa
WAPO Mission International kwa jitihada mzifanyazo kufanikisha jambo hili
muhimu na la msingi sana. Siyo kazi
rahisi lakini ni jambo linalowezekana.
Penye nia pana njia. Dumisheni msimamo
wenu na endelezeni juhudi mzifanyazo mtafanikiwa. Mungu ni mwema atawabariki na kuwashindia kwa
kazi njema muifanyayo.
Risala
Baba
Askofu Mkuu Gamanywa;
Waheshimiwa
Maaskofu na Ndugu Waumini;
Sote
tumekusikia Baba Askofu ukieleza kwa ufasaha kwenye risala shabaha za Sera ya
Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania na jinsi mnavyokusudia na mlivyojipanga
kuzitekeleza. Lazima nikiri kuwa
nimetiwa moyo na mambo mazuri mliyokusudia kufanya. Ikiwa mtandao mnaotaka kuunda utafanya kazi
kama inavyokusudiwa, nina imani baadhi ya changamoto kubwa zinazowakabili
vijana nchini zitakuwa zimepata muarobaini.
Mambo mengi yameelezwa vizuri na Baba Askofu Mkuu na mimi sina sababu ya
kuyarudia. Lakini naomba nigusie
machache ambayo nadhani yanahitaji kusemewa kidogo.
Kwanza
naomba niwapongeze kwa hatua mliyofikia ya kuanzisha mchakato wa kusajili Chuo Kikuu
cha Uongozi wa Kimaadili na Taasisi ya Kukuza Vipaji. Naomba mkamilishe mapema usajili wa taasisi
hizi za aina yake ili vijana wetu waanze kunufaika nazo. Kuhusu umilikishwaji wa ardhi, nawashauri
mpeleke maombi yenu kwa mamlaka zinazohusika bila ya shaka mtafanikiwa. Nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kuwawezesha
kujenga taasisi hizo. Lakini ardhi hiyo
ina wenyewe wanaoimiliki. Ama ni wananchi mmoja mmoja au familia zao au Serikali
za Vijiji au Halmashauri za Wilaya na Miji.
Ni kweli Katiba inasema ardhi yote ya nchi hii ni mali ya Rais. Lakini Rais ni mdhamini tu wa ardhi ya nchi
yetu kwa niaba ya wananchi wote. Inampa
fursa ya kutwaa ardhi ya mtu ye yote kwa manufaa ya taifa. Hapo tunazungumzia mambo ya kitaifa ya
kunufaisha wengi. Wenye ardhi hasa ni
hao niliowataja hapo juu, hivyo anaetaka
ardhi hana budi kuwaona. Mnachotakiwa ni
kutambua ardhi mnayoitaka kisha mumjue mwenyewe nani muonane nae na kuzungumza
nae. Naamini mtaelewana na wala
hakapakuwa na lazima ya Rais kusema neno.
Baba
Askofu;
Nimefurahi
kusikia
kuwa kilimo ni miongoni mwa shughuli za vikundi vitakavyoundwa katika
utekelezaji wa sera hii. Mmefikiria
jambo la maana sana. Ni ukweli ulio wazi
kamba kilimo kinatoa fursa kubwa za ajira kuliko sekta nyingine yo
yote. Kilimo hakivutii watu wengi hasa vijana kwa
sababu ya matumizi madogo ya teknolojia za kisasa. Kilimo ni kazi ya
shuruba kwa sababu ya
kutegemea jembe la mkono na plau ya kukokotwa na ng’ombe badala ya
trekta. Inakimbiza vijana wasomi. Kilimo kina tija ndogo kwa sababu ya
kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu na matumizi madogo ya pembejeo za
kisasa kama
vile mbegu bora, mbolea, dawa za kuua wadudu na za kukinga na kutibu
magonjwa
ya mimea. Hali kadhalika kutokutumia
maarifa ya kisasa katika utayarishaji wa mashamba, upandaji na
mengineyo. Juhudi tulizozianza mwaka 2006 chini ya ASDP
zina lengo la kukitoa kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa. Tuna program
za kutoa ruzuku ya pembejeo kwa
wakulima na tayari wengi wananufaika.
Tunao mpango wa kuingiza matrekta na kukopesha wakulima katika vikundi
vyao. Naamini vikundi hivi navyo
vinaweza kunufaika. Pia tunao mpango wa
kuanzisha Benki ya Wakulima kutoa mikopo kwa wakulima waweze kupata zana
na
pembejeo za kilimo. Vikundi hivi
vitanufaika pia. Ninawatia moyo
likazanieni hili la vikundi vya kilimo kwani ni jambo lenye matumaini
makubwa. Sisi Serikalini tutaendelea
kushirikiana nanyi kufanikisha malengo yenu.
Tutasaidia
upande wa mafunzo kwa vijana wetu.
Maafisa ugani watawaelimisha masuala ya kilimo. Kwa wale watakaojihusisha na viwanda ni vyema
mkashirikiana kwa karibu na SIDO kwani wao wanao utaalamu wa kutosha katika
shughuli za namna hiyo. Kwa suala la
mitaji siwezi kusema kwamba Serikali inaweza kuwa na fedha zote
zitakazohitajika. Lakini, jungu kuu
halikosi ukoko. Tutasaidiana pale tutakapoweza. Hivi sasa upo Mfuko wa kusaidia
wajasiriamali na hasa kupitia vikundi vya uzalishaji mali na huduma. Bahati mbaya mahitaji ni makubwa kuliko uwezo
wa Mfuko, hivyo wanaopata si wengi.
Katika hao wanaopata baadhi ya vikundi hivi vinaweza kuwa miongoni mwa
hao.
Napenda
kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na
sekta binafsi, kuangalia namna ya kuchangia katika juhudi hizi za
Serikali. Siyo lazima watoe fedha,
lakini wanaweza kufungua fursa za kuwasaidia vijana katika vikundi vyao kama
hivi vilivyoanzishwa na WAPO Mission International. Wanaweza kufanya kama wanavyofanya Shirika la
Nyumba la Taifa na VETA. Imani yangu ni
kuwa hivi vikundi vikisaidiwa vitakua na kuwezesha vijana wengi zaidi
kujitegemea badala ya kusubiri kuajiriwa Serikalini au kwenye makampuni binafsi.
Mwisho
Kabla
ya
kumaliza narudia kuwapongeza kwa jambo hili jema mlifanyalo leo.
Lakini ni sifa yenu ya miaka mingi. Napenda kuwaahidi kuwa Serikali
itajitahidi
kufanya yale inayotakiwa kufanya ili sera hii tunayoizindua leo ifikie
malengo
yake. We will play our part. Mwisho
nawashukuru tena kwa kunialika, nawapongeza wale wote alioshiriki kuandaa na
kufanikisha shughuli hii ya leo. Wamefanya
kazi nzuri iliyotukuka. Nawapongeza waumini
na hasa vijana kwa kufika kwa wingi. Ninyi
ndiyo walengwa. Bila ya nyie hakuna
MVIMAUTA. Naomba sote tuendelee kumuunga
mkono Baba Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa na kumtia moyo azidi kufanya mambo
mengi mengine mazuri katika kuwatumikia ninyi waumini wa Kanisa lake na
Watanzania kwa jumla. Tunakupenda
sana. Tunatambua na kuthamini sana kazi
njema uifanyayo. Nawaomba muendelee pia
kuliombea taifa letu, liendelee kuwa na amani na utulivu na tupate mafanikio
zaidi.
Baada
ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania, imezinduliwa rasmi.
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.










0 comments:
Post a Comment