Na Veronica Mheta, Arusha
NDEGE ya Shirika la Ndege la Ethiopia, imetua kwa dharura katika uwanja mdogo wa
Arusha baada ya kushindwa kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA) kutokana na ndege nyingine ya TFC kukwama kwenye njia ya
kurukia.
Aidha, ndege hiyo ya Ethiopia aina ya Boeing 767 namba ET- AQW
iliyokuwa ikitoka Ethiopia ili kutua KIA na iliwasiliana na waongoza ndege wa
KIA waliotoa maelekezo ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo
Kenyatta, lakini rubani huyo alishindwa kufika Nairobi na kulazimika kutafuta
uwanja mwingine wa karibu ndipo alipotua uwanja mdogo wa Arusha.
Hata hivyo, ndege hiyo iliyotua saa 6 mchana uwanjani hapo,
ilititia kwenye tope wakati rubani akijaribu kukata kona katika uwanja huo
mdogo ambao hauruhusu kutua ndege kubwa.
Hali hiyo ilizua taharuki kwa wafanyakazi wa kiwanja hicho na
abiria waliokuwa wakisubiri ndege zingine
kwenda sehemu mbalimbali za
utalii na safari za kawaida.
Baada ya kutua salama, abiria wa ndege hiyo zaidi ya 213 na
wafanyakazi 23 waligoma kushuka kwa
kutumia ngazi za kiwanjani hapo na kukaa ndani ya ndege kwa karibu saa tano
wakisubiri ngazi kubwa kutoka KIA.
Kugoma kushuka kwenye ndege hiyo kulisababisha baadhi ya
wafanyakazi wa ndege hiyo kufungua milango ya dharura ili abiria wapate hewa.
Kwa mujibu wa wafanyakazi
wa uwanja huo wa Arusha, ndege hiyo ililazimika kutua hapo kutokana na kuishiwa
mafuta.
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka jina lake liandike
gazetini kwa madai ya kuwa si msemaji, alisema haijawahi kutokea ndege kubwa
kama hiyo kutua uwanjani hapo salama, lakini kwa kuwa ni kubwa ilikwama kwenye
tope na kusababisha hofu kubwa ila vyombo vya usalama vilikuwapo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ambaye alifika eneo la
tukio alisema tukio hilo halijapata kutokea lakini akasisitiza kuwa kuna haja
ya kuboresha uwanja huo ili hata
zinapotokea dharura zishughulikiwe kwa wakati.
SOMA ZAIDI: HABARILEO ONLINE














0 comments:
Post a Comment