MTANDAO
wa Wanafunzi nchini(TSNP) na Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya Chuo Kikuu
cha Dar es salaam(UDHRA) wamemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuweka hadharani
ripoti ya Tume ya kuchunguza matokeo ya kidato cha nne mwaka jana ndani ya wiki
moja.
Mkurugenzi
wa TSNP, Alphonce Lusako alisema jana kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na
serikali katika kuimarisha elimu lakini bado kuna changamoto kubwa katika
ukuaji wa sekta ya elimu.
“Kwa
niaba ya watanzania na wadau wa elimu waliowengi tunasikitishwa na usiri wa
tume ya kuchunguza matokeo ya kidato cha nne iliyoundwa na waziri Mkuu mwaka
huu” alisema.
Alisema
“tunamtaka waziri mkuu ndani ya wiki moja atoe ripoti ya Tume hadharani juu ya
madhaifu yaliyopatikana, wakina nani wamehusika na madhaifu husika, mapendekezo
ya tume husika ili yasijirudie tena kwa wadogo zetu wa kidato cha nne,
wanaofanya mtihani sasa”.
Lusako
alisema “ikumbukwe kwamba kwa sasa kidato cha nne wapo kwenye miihani yao ya
mwisho lakini bado tume iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza madhaifu ya mitihani
ya kidato cha nne mwaka uliopita bado imekuwa ni siri ya tume na waziri mkuu”.
Alisema
endapo waziri mkuu hatatoa ripoti yake ndani ya wiki moja watachukua jukumu la
kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, wanafunzi wa sekondari na shule
za msingi nchini, asasi zisizo za serikali, wadau mbalimbali wa elimu, vyama
vya siasa, wazazi na watanzania kwa ujumla wake ambao wameunga mkono umahututi
wa mfumo wa elimu kufanya maamuzi ili kunusuu elimu nchini.
Aliwaomba
watanzania wote kushirikiana kwa suala hilo kwa kuwa suala la elimu ni la
watanzania wote na si la serikali pekee na kusisitiza kamba elimu itabadilishwa
na watanzania na itauawa na watanzania.
Mwisho








0 comments:
Post a Comment