
Kijana huyo ambaye hajafahamika ni mkazi wa wapi amekutwa
na kete 65 za dawa zinazosadikiwa kuwa za kulevya na alikuwa akitokea Dar es
salaam kwenda Lilongwe nchini Malawi kwa basi mali ya kampuni ya Taqwa lenye namba T 319 BLZ aina ya Nissan.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani
alisema kwa mujibu wa hati ya kusafiria kijana huyo amefahamika kwa jina la
Kassim Said Mboya(36), lakini jina lililokuwa kwenye tiketi yake ya basi hilo
ni Kassim Mueck Michael.
Kamanda Athuman aliwaambia waandishi wa habari
kuwa juzi(Novemba 7) majira ya asubuhi basi alilokuwa akisafiria kijana Kassim
lilifika Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi na abiria wote kutakiwa
kushuka kwa ajili ya kushughulikia taratibu za kuvuka mpaka kama ilivyozoeleka.
Tofauti na abiria wenzake, kijana huyo alibaki
ndani ya gari huku hali yake ya afya ikionekana kudhoofu na ndipo wafanyakazi
wa basi hilo walipochukua uamuzi wa kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo jirani
na kisha askari wa jeshi hilo kumchukua na kumpeleka katika hospitali ya wilaya
ya Kyela.
Alisema kutokana na kudhoofu kwake na dalili alizokuwa nazo ilibidi polisi washauriane na
maadaktari na ndipo yakachukuliwa maamuzi ya kumfanyia uchunguzi wa miale(X
Ray) na kubaini kuwa tumboni mwake kulikuwa na vitu aina ya pipi na kuwa huenda
ndivyo vilimfanya adhoofu kiasi hicho.
Alisema kwa bahati mbaya wakati huo wote hali ya kijana
Kassim iliendelea kuwa mbaya na hatimaye kufariki dunia wakati uchunguzi huo
ukiendelea na ndipo ikalazimu mwili wake kusafirishwa hadi hospitali ya Rufaa
Mbeya kwaaajili ya uchunguzi zaidi.
Kamanda huyo alisema baada ya mwili huo kufikishwa
hospitali ya rufaa ulifanyiwa uchunguzi kwa kupasuliwa na ndipo walipokuta kete
65 za dawa hizo zinazosadikiwa kuwa za kulevya huku moja kati ya hizo ikionekana
kutoboka hali iliyoleta hisia kuwa ndiyo iliyosababisha kijana huyo kupoteza
maisha.
“Kijana huyu pia alikuwa na begi dogo lenye
suruali moja aina ya jeans, fulana moja nyeusi,raba jozi moja rangi
nyekundu,mkate mmoja,mkoba mdogo wa kiunoni, kadi mbili za kinga ya ugonjwa wa manjano,randi
mbili sarafu za Afrika kusini na mifuko sita ya Rambo ya rangi nyeusi” alisema
Kamanda Athuman alisema taratibu zinafanyika ili dawa
hizo zipelekwe ofisi ya mkemia mkuu wa serikali kwa uchunguzi wa kitaalamu ikiwa
ni pamoja na kujua aina ya dawa na uzito wake.
Aliwataka wakazi mkoani hapa kufika katika chumba cha
kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa Mbeya kwaajili ya kuutambua mwili wa
kijana huyo ambaye hafahamiki ni mkazi wa wapi.








0 comments:
Post a Comment