
Imeandikwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB
Leo
nimeamka na mzuka wa kuandika. Kwanza nasukumwa na kuandika kuhusu
ukweli, zaidi kwa kuwa nafurahia kuandika maneno yanayofanana na yale
yaliyosemwa na mwandishi nguli wa Kiswahili, babu yangu Shaaban Robert,
ambaye kazi zake hazitokuja kufubaa vizazi na vizazi, nikizifananisha na
zile za William Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa mashairi na fasihi
simulizi wa Uingereza ya karne ya 16.
Lakini pia nafurahi kuandika kuhusu dhana ya ukweli ambayo mimi daima naisimamia na nitaifia itapobidi. Hayati
Shaaban Robert anaandika hivi katika kitabu chake cha Kusadikika:
‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake. Nikipatwa na ajali kama hiyo,
sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote.
Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na
furaha ya milele itakayotokea pale uongo utakaposhindwa.’
Nimeazima
hekima hizi kutoka kwa Shaaban Robert kwa lengo la kutaka kuzungumza
ukweli, maana ukweli una tabia nyingi sana na kubwa niipendayo mimi ni
ile ya kutobadilika badilika. Ukweli hubaki ukweli hata kama utaishi
miaka dahari, utabaki kuwa kweli tu.
Nimependa
leo kujadili jambo hili kwa sababu kwanza lilileta aibu kubwa kwa bunge
letu, pili mijadala iliyofuatia baada ya jambo hili ilileta taswira ya
kuonewa na kukandamizwa kwa upinzani kwa kuzibwa mdomo, na tatu kwa kuwa
iliongeza nguvu kwa wapinzani bungeni kudumu katika kususia kushiriki
mjadala wa hoja ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba iliyokuwa
ikijadiliwa. Yote haya naona yanapelekea kutuondoa kwenye mtindo wa
‘muafaka’ wa pamoja kwenye mchakato wa kuandika upya katiba yetu
tuliokuwa tukiendelea nao.
Nitaomba
nitumie kanuni za bunge kujenga hoja yangu. Nianze na ile kanuni ya 60
(1.) ambayo inatoa maelekezo ni wakati gani mbunge atapata muda wa
kusema bungeni, inasema: ‘ Mbunge akitaka kusema bungeni anaweza:- (a)
kumpelekea spika ombi la maandishi; (b) kusimama kimya mahali pake; na
(c) kutumbukiza kadi ya elektroniki.’ Mhe. Mbowe aliposimama bungeni
alitumia kanuni hii kwenye ile fasili ndogo ya (b).
Lakini
ukisoma kanuni hiyo hiyo ya 60 ile fasili ya pili inasema ‘isipokuwa
kwamba, Mbunge yeyote hataanza kuzungumza hadi aitwe na spika ama kwa
jina ama kwa wadhifa wake na kumruhusu kusema…’ Hivyo Mhe. Ndugai (NS)
alimuona Mhe. Mbowe lakini hakumruhusu kusema, na kwa mujibu wa kanuni
hii alikuwa kwenye mamlaka ya kuamua aidha kumruhusu ama kutomruhusu.
Mbowe
anataka kuzungumza baada ya hoja kuafanyiwa maamuzi, anazungumza nini
tena? Anataka kura zipigwe kwa mara nyingine ya pili tena ama anataka
kuanzisha upya mjadala wa hoja iliyofungwa? Anasimama kwa kanuni gani,
maana kanuni ambayo ingeweza kumpa fursa ya kuzungumza ilikuwa ni ile ya
‘kuhusu utaratibu’ tu, lakini kwa mujibu wa taarifa rasmi ya
majadiliano ya bunge (hansard) za siku hiyo, aliposimama Mhe. Mbowe
(KUB) hakusema ‘kuhusu utaratibu’. Kanuni ya 68 (1.) inasema hivi:
‘Mbunge anaweza kusimama wakati wowote na kusema maneno “kuhusu
utaratibu”, ambapo Mbunge yeyote ambaye wakati huo atakuwa anasema
atanyamaza na kukaa chini na Spika atamtaka Mbunge aliyedai utaratibu
ataje kanuni au sehemu ya kanuni iliyokiukwa.’ Kwa mujibu wa taarifa
rasmi za majadiliano ya bunge (hansard), Mhe. Mbowe (KUB) hakutamka neno
hili na kwa maana hiyo hakukusudia kulielekeza Bunge kuhusiana na
kanuni yoyote ya bunge iliyokiukwa. Na pia hakukuwa na Mbunge yeyote
yule aliyekuwa akisema kwa wakati ule hivyo matumizi ya kanuni hiyo
hayakuwa ‘warranted’.
Aghalabu
angeweza kutumia kanuni ya 63 (3.) inayoruhusu Mbunge yeyote yule
kusimama na kutamka maneno ‘kuhusu utaratibu’ kama angekuwepo Mbunge
anayesema kwa wakati ule, lakini bahati mbaya sana hakuwepo Mbunge
yeyote aliyekuwa akisema wakati ule. Kumbukumbu rasmi za bunge (hansard)
zinaonesha kuwa ndiyo kwanza tulikuwa tumemaliza kupiga kura na Mhe.
Ndugai (NS) ndiyo alikuwa amemuita tu Mbunge wa Vunjo, Mhe.
Augustino
Lyatonga Mrema azungumze, naye hakuwa amezungumza lolote lile.
Kipengele hiki cha kanuni hii huwa kinatumika bungeni kwa ajili ya
kumkosoa Mbunge aliyesema uongo ili kuweka kumbukumbu sawia. Kwa kuwa
hakuna aliyekuwa amesema lolote lile, maana yake hakukuwa na taarifa za
uongo zilizosemwa bungeni na yeyote, hivyo kipengele hiki hakikuwa na
nafasi. Hivyo kanuni hii pia isingeweza kutumika kumpa ulazima wa yeye
kupewa fursa ya kusema bungeni kwa wakati ule.
Kanuni
nyingine ambayo ingeweza kumpa nafasi ya kuzungumza ilipaswa kuwa ile
ya ‘taarifa’; hii ni kanuni ya 68 (8.) ambayo inasema: ‘vile vile Mbunge
yeyote anaweza kusimama mahali pake na kusema “taarifa” na kwa ruhusa
ya Spika, atatoa taarifa au ufafanuzi kwa Mbunge anayesema….’ Jambo la
kwanza Mhe. Mbowe (KUB) hakusema neno hili, kwa mujibu wa taarifa rasmi
za bunge (hansard) na la pili hakukuwa na mbunge mwingine aliyekuwa
akisema wakati ule hivyo hakukuwa na mtu yeyote ambaye alihitaji taarifa
ya Mhe. Mbowe.
Kilichokuwepo
bungeni kwa wakati ule ni kuwa, bunge lilikuwa limemaliza tu kuifanyia
kazi na hatimaye kuifanyia uamuzi hoja ya Mhe. John Mnyika (Mb.)
iliyotaka kura zihesabiwe na ikapita na hivyo kura zilihesabiwa.
Nimeitazama
kanuni ya 68 (7.) labda kama ilitumika, lakini wapi! Kanuni hii
inasema: ‘hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo
hakuna Mbunge mwingine anayesema na kuomba “mwongozo wa Spika” kuhusu
jambo ambalo limetokea bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama
jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa kanuni na taratibu
za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye, kadri
atakavyoona inafaa.’ Kwa bahati mbaya sana Mhe. Mbowe (KUB) pia
hakutumia kanuni hii, kwa kutotamka maneno haya kama ambavyo taarifa
rasmi za majadiliano bungeni (hansard) za siku hiyo zinavyosema.
Kumpa
nafasi ya kusema Mhe. Mbowe ingekuwa ni sawa na kudharau Bunge zima
ambalo lilikwishafanya maamuzi kwa njia ya kura kuhusiana na hoja ya
kutaka uamuzi wa kukataa hoja ya Mhe. Mnyika ufanywe kwa njia ya kura.
Wakati naandika hapa nimefanya utafiti wa kutosha kwa upeo wa macho
yangu na uwezo wangu na nimejiridhisha kabisa, bila shaka yoyote ile
kuwa, hakukuwa na nafasi yoyote ile ya kikanuni ya kutoa fursa ya Mbunge
yeyote yule kulijadili jambo ambalo lilikwishafanyiwa uamuzi na bunge
zima.
Na
kama Mhe. Mbowe (KUB) alikuwa anataka kuleta mezani hoja mpya hakukuwa
na sababu ya kuwa na wasiwasi maana tayari Mhe. Ndugai (NS)
alikwishaingiza kwenye kumbukumbu kuwa alikwishamuona, na kwa mujibu wa
kanuni za bunge angempa nafasi ya kusema baadaye. Katika hali ya
kawaida, Mhe. Mbowe (KUB) alipaswa kukaa chini na kusubiri ni wakati
gani angeitwa apewe fursa yake ya kusema. Hakuna kumbukumbu yoyote ile
inayosema kwamba Mhe. Mbowe (KUB) alikuwa na hoja ya dharura na hata
baada ya bunge hatujashuhudia jambo lolote lile la dharura
lililotokea.
Kanuni
ya 5 ya bunge inampa Spika mamlaka ya kuwa na maamuzi ya mwisho kwenye
jambo lolote kwenye mijadala ya Bungeni, na hii ni kwa mujibu wa ibara
ya 84 ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Pia kanuni hiyo hiyo
ya 5, ile fasili ya (4) mpaka ya (6), inatoa fursa kwa Mbunge yeyote
ambaye hakuridhika na uamuzi wa kiti (NS kwa niaba ya Spika) kukata
rufaa dhidi ya uamuzi huo. Hivyo, badala ya Mhe. Mbowe (KUB) kulazimika
kung’ang’aniza kiti kimpe nafasi ya kusema bungeni angeweza kukaa
akasubiria kufuata utaratibu wa kukata rufaa unaowekwa na kanuni hii.
Kwa
heshima ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni na kwa kuzingatia ukweli kwamba
katika mfumo wa demokrasia yoyote ile iliyokomaa, sauti ya wachache ni
lazima ipewe fursa ya kusikika zaidi kuliko hata ya wengi. Pengine ni
dhana hii iliyopelekea Spika kuamua kumpa haki ya kwanza ya kusema
Kiongozi wa Upinzani Bungeni kila mara anapokuwa ameonesha nia ya
kufanya hivyo kwenye hoja yoyote ile bungeni. Pia pengine ndiyo maana
KUB amekuwa akipewa kipaumbele cha kuuliza swali la kwanza kwenye
kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Pengine. Lakini
kwa mujibu wa kanuni za Bunge zinazotumika sasa, sijaona mahali popote
pale kwenye kanuni hizi ambapo KUB anapaswa kupewa nafasi ya upendeleo
kwenye kusema bungeni. Sijaona. Napata hisia kwamba pengine KUB alitaka
kujifananisha na KUB wa Bunge la Uingereza, ambaye ana mamlaka tofauti
na KUB wa bunge letu.
Rai
yangu kwa watanzania wenzangu wote ni kuwa, tuepuke tabia ya kupuuza
ukweli na kuatamia uongo. Ama kushabikia uongo. Kufanya hivyo ni
kuchukua hatua za haraka kuelekea kuondoa mtangamano wa kitaifa na
kuvuruga amani, upendo na mshikamano wetu. Watanzania tuwe makini
tuepuke vitendo vyote vinavyotishia kulegalega kwa tunu hizi. Tusikubali
kuacha mbachao kwa msala upitao. Tutakuja kujuta tukiendelea
kuushadadia uongo na kufurahia matunda ya zao la uongo la muda mfupi ,
kisha siku kweli ikidhihiri tutaambulia aibu na majuto na masikitiko ya
milele.
Ukweli
una hii tabia nyingine ambayo mimi naihusudu sana; hii ni ile tabia ya
kuwa ukweli haupendi kupuuzwa puuzwa. Ukweli unapenda usemwe na utatoa
faida yake, na ukipuuzwa tu siku moja utadhihiri na itakuwa tumechelewa.
Huu ni ushauri wangu wa wazi kwa watanzania wenzangu wote kuwa tudumu
kwenye ukweli bila kutazama itikadi zetu na tusiupuuze ukweli kwa
kuchelea aibu ya muda tukajinyima faida ya kudumu itokanayo na kweli.
Yeyote
atakayeamua kufuatilia kanuni zetu za bunge na akasoma kumbukumbu za
taarifa rasmi za majadiliano ya bunge, naamini, atakubaliana na mimi
kuwa hakuna uonevu uliokuwepo, wala hakuna mabavu yaliyotumika katika
kumnyima nafasi ya kusema bungeni Mhe. Mbowe (KUB). Tunatofautiana hisia
lakini ukweli kwa faida ya ukweli utabaki pale pale.








0 comments:
Post a Comment