
Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imewataka
wafanyabiashara, wanasiasa na watumishi wa umma wanaojihusisha na ujangili,
kujisalimisha haraka.
Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema hayo jana Dar es Salaam mara baada ya
kupokea ujumbe wa matembezi ya hiari yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi
Wanyamapori (AWT).
Amesema pia Serikali
inakusudia kuwafikisha katika vyombo vya Dola watuhumiwa na kuwatangaza kwenye
vyombo vya habari ili umma na dunia
ifahamu wahujumu rasilimali hiyo.
Nyalandu alisema Serikali
inajenga uwezo wa kukabiliana na majangili porini na matajiri wanaofadhili
ujangili ambao wako Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Nairobi (Kenya) na hata
Beijing nchini China.
“Dawa ya majangili
imekwishachemka na inapelekwa mezani wakati wowote...ole wake
atakayenyweshwa dawa hiyo,” alisema
Nyalandu huku akitoa onyo kwa wanaojihusisha kuacha kabisa uovu huo, vinginevyo
watajikuta wamenaswa na vyombo vya Dola.
Alisema ujangili
umechangia kupungua idadi ya tembo nchini kutoka 350,000 miaka ya 1960, hadi
110,000 mwaka 2009, huku idadi ya tembo wanaouawa na majangili ikizidi
kuongezeka kila mwaka.
Alitoa mfano wa mwaka
2010 ambao tembo waliouawa walikuwa 259, mwaka 2011 tembo waliouawa walikuwa
276 na mwaka 2012 walikuwa tembo 473 huku kati ya Januari hadi Julai mwaka huu,
tembo 378 wakiuawa.
Hata hivyo alisema
Serikali imekuwa ikipambana na majangili hao ndani na nje ya hifadhi za taifa,
na katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia (2010 – 2012), majangili 4,066 walikamatwa na bunduki 1,899
kukamatwa na kutaifishwa.
Kuhusu matembezi
yaliyoanzia jijini Arusha Agosti 24,2013, aliwapa pole wananchi 18 waliotembea
kwa hiyari kutoka Arusha hadi hapa Dar es Salaam na kuongeza kuwa ubunifu huo
umebeba ujumbe mkubwa kuhusu kupiga vita ujangili nchini.
Kwa upande wake
muanzilishi wa matembezi hayo, Pratik Patel
amewataka Watanzania kuamka na kuhakikisha wanatokomeza ujangili kwani ni
rasilimali inayopotea pasipokuwa na manufaa.
Alisema ametumia siku 19 kutembea bila kulipwa
chochote ambapo vuguvugu hilo halitoishia katika matembezi hayo na kwamba
atakwenda kuhamasisha wananchi nyumba
kwa nyumba namna ya kuwa walinzi wazuri wa rasilimali zao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge Ardhi Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema endapo wimbi la
ujangili litaachwa liendelee bila ya hatua stahiki kuchukuliwa katika miaka 10
ijayo Tanzania haitokuwa na tembo.
Alisema hata kitendo cha
matembezi hayo kimeionesha Serikali kuchukua hatua za haraka kwani tembo
wamekuwa wakiingiza mabilioni ya fedha.
Alisema kila mwezi tembo
800 huuawa huku kwa mwaka ikifikia tembo 10,000 jambo ambalo hivi sasa hakuna
anayeweza kutoa idadi ya tembo waliobaki.
“Serikali inatakiwa
kuchukua hatua za haraka, kwani kipindi cha nyuma lipo gari la Wizara ya Elimu
lilikamatwa likiwa na meno ya tembo na mhusika alikamatwa kwa siku tano tuu
baada ya hapo akaachiwa huru jambo ambalo linatakiwa kutazamwa upya,” alisema
Lembeli.
Mbali na matembezi hayo,
Mfuko wa uhifadhi wanyamapori Fredkin Conservation Fund umekabidhi hundi ya dola za kimarekani
milioni 2.25 kwa ajili ya kupambana na ujangili nchini.








0 comments:
Post a Comment