Friday, March 29, 2013

Muuaji wa Padri Mushi Adakwa

JESHI la Polisi limesema anayedaiwa kuwa muuaji wa Padri Evarest Mushi amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo.
Kauli hiyo ya Polisi inakuja siku moja baada ya Askofu Mkuu wa kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kulilaumu Jeshi la Polisi kwa kuzembea kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya padri huyo.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kardinali Pengo alisema mauaji hayo yamefedhehesha si tu wakatoliki bali pia wakristo wote nchini na kusema kuwa pamoja na kuwa vitendo hivyo ni vya kinyama lakini kamwe kanisa halitalipiza visasi.
Alisema kufuata mauaji hayo kanisa limeandaa misa maalum ya kumuombea marehemu Mushi inayotarajiwa kufanyika Aprili 20,  mwaka huu Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa alisema upelelezi wa  kesi hiyo ya mauaji ya Padri Mushi umefikia mahali pazuri.
“Napenda kuwapa taarifa ya maendeleo ya kesi ya mauaji ya Padri Evarest Mushi. Najua si ninyi tu waandishi wa habari lakini Watanzania wote wanataka kujua maendeleo ya upelelezi wa tukio hili.
“Jeshi la Polisi liliwaahidi litawajulisha kila hatua iliyofikiwa juu ya upelelezi wa shauri hili. Mpaka hapa tunapozungumza upelelezi wa shauri hili umefikia pahala pazuri na jalada la shauri hili limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria.
“Muhusika wa mauaji haya tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo, “ alisema Kamishna Mussa.
Alisema Jeshi la Polisi lilichukua hatua kadhaa za kiupelelezi  ikiwa  ni pamoja na kuchora michoro ya sura ya mtu kwa kutumia watu walioshuhudia tukio hilo na kwamba baada ya kuitoa picha hiyo katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii muhalifu huyo ametambulika.
“Jeshi la Polisi liliahidi kutoa milioni kumi kwa watu watakaosaidia kupatikana kwa muhalifu huyu. Ahadi ile ipo pale pale na mwananchi aliyesaidia kutoa utambuzi Jeshi la Polisi litamzawadia kiwango hicho cha fedha, lakini kwa usalama wa shahidi huyo na kwa sababu za kiupelelezi tukio la kumkabidhi fedha hizo hatutaliweka bayana katika vyombo vya habari.
“Mwisho kabisa, naomba niwashukuru tena wananchi wote wa Zanzibar kwa kuwa karibu na ofisi yangu na Jeshi la Polisi kwa ujumla katika mapambano ya vitendo vya kihalifu,” alisema Kamishna Mussa.
Katika hatua nyingine Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar amewahakikishia amani na utulivu wananchi wa Zanzibara wakati wa Sikukuu ya Pasaka.
“Napenda kuendelea kuwahakikishia uwepo wa usalama na amani kwa muda wote wa mapumziko na Ibada za Pasaka.
“Jeshi la Polisi linawahakikishia kuendelea kudumisha doria za mjini na vijijini kwa kutumia gari, askari wa miguu, pikipiki na mbwa ili kuhakikisha usalama unadumu visiwani hapa.
“Tutaendelea kutoa ushauri wa kiusalama na kushirikiana kwa karibu zaidi na wananchi wote kuona maisha na mali zao zinakuwa salama. Tunawaomba wenye mahoteli ya kitalii na nyumba za starehe kuwa karibu na Jeshi lao la Polisi pamoja na kufuata ushauri wote wa kiusalama wanaopewa kila wakati.”

0 comments:

Post a Comment