VYAMA vya siasa jana vilianza kutoa maoni mbele ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku Chadema ikipendekeza umri wa kugombea urais
uwe miaka 18.
Wawakilishi
wa vyama hivyo vya siasa ambavyo ni pamoja na CCM, CUF, UDP na TLP walitoa
maoni yao bila waandishi wa habari kuhudhuria katika kile kilichoelezwa ni
kutaka watoa maoni wawe katika uhalisia wao.
Mikutano
hiyo ya jana iliendeshwa kwa siri kati ya wajumbe wa Tume na wa vyama hivyo
hali ambayo ilifanya wanahabari kusubiri nje huruma ya vyama ambavyo vilikuwa
tayari kueleza walichopendekeza ndani.
CCM
ambayo ujumbe wake uliongozwa na Mwanasheria mkongwe Andrew Chenge hawakuwa
tayari kueleza kilichomo ndani ya waraka wa chama hicho badala yake Mwenyekiti
wa ujumbe huo alijibu swali moja la waandishi wa habari juu ya mgombea binafsi.
Na
hata hivyo kuhusu mgombea binafsi Chenge hakutaka kuzungumzia mapendekezo yao
kwa kina ila alisema chama chake
kinaliunga mkono kwa hadhari.
Alisema
kama wananchi watapendelea mgombea binafsi awepo, basi awekewe mipaka kama
ilivyo kwa wagombea wa vyama vya siasa ambao wanabanwa na katiba za vyama vyao
ili watende kwa maslahi ya chama na wananchi.
"Na
huyu mgombea binafsi kama ataruhusiwa, sisi tunataka awekewe mipaka ndani ya
Katiba mpya, kwani kwenye vyama watu wanateuliwa baada ya mchakato mrefu,"
alisema Chenge ambaye hata hivyo hakutaka kuzungumza kwa kina juu ya
mapendekezo ya chama hicho.
Kwa
muda mrefu Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa inapinga kuwepo kwa mgombea
binafsi kwa madai kuwa muda wa kufanya hivyo bado.
Serikali
imebadilisha sheria ya uchaguzi mara kadhaa kuhakikisha suala la mgombea
binafsi halipewi nafasi, licha ya ushauri wa Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere
ambaye alitamani kuwepo na mgombea huyo.
Katika
kesi ambazo zilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila kupinga sheria ya
uchaguzi, Serikali licha ya kubwagwa
mara kadhaa; lakini ilikata rufaa kwa jopo la majaji wa Mahakama ya
Rufani ambao walitamka kuwa suala hilo ni la kisiasa na Mahakama haina mamlaka
ya kutamka kama mgombea binafsi awepo ama la bali ikaamuru suala hilo
lirudishwe bungeni kwani chombo hicho ndicho chenye mamlaka ya kutunga sheria.
Chenge
alipoombwa waraka wa CCM wenye mapendekezo ya chama alijibu, "Haya ni
mapendekezo ya chama siwezi kuwapa ila wanachama wetu wanafahamu tunachohitaji
kiwemo kwenye Katiba mpya," alisema Chenge baada ya kuombwa waraka wa
chama hicho ambao wameuwasilisha kwenye Tume.
Ujumbe
wa CCM licha ya Chenge, mjumbe mwingine alikuwa Kingunge Ngombale-Mwiru, Kidawa
Salehe na Othman Machano.
Maoni
ya Chadema
Chadema
kwa upande wake imependekeza umri wa kugombea urais ushushwe hadi miaka 18 ili
kutoa fursa ya mtu yeyote kuwa na haki ya kupiga kura na kupigiwa kura.
"Haiwezekani
awe na haki ya kupiga kura lakini asiwe na busara ya kuwa Rais wa nchi hii,
tunapendekeza mpiga kura awe na haki za kisheria za kugombea urais, ubunge na
udiwani," alisema Tundu Lissu ambaye alikuwa Katibu wa Ujumbe wa Chadema.
Ujumbe
wa Chadema katika mkutano huo na Tume uliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Kabwe Zitto
na Mkurugenzi wa Vijana John Mnyika.
Chama
hicho pia kilipendekeza mfumo wa elimu nchini utolewe kwa lugha ya Kiswahili
kuanzia shule za msingi hadi vyuoni na Kiingereza liwe somo linalojitegemea.
Pia walipendekeza Katiba itamke kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa ya Tanzania
hivyo shughuli zote za kiserikali, bungeni na mahakamani itumike lugha hiyo.
"Wabunge
wengi hawajui Kiingereza, lakini wanatunga sheria kwa Kiingereza. Mahakamani
majaji hawajui Kiingereza lakini wanalazimishwa waandike Kiingereza, umefika
wakati Katiba iseme Kiswahili kitumike katika vyombo hivi," alisema Lissu.
Kwa
upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, chama hicho kilipendekeza iwe na wajumbe
25 kati yao 15 watokane na vyama vyenye uwakilishi bungeni na wateuliwe kwa
uwiano wa wabunge walioko bungeni.
Lakini
wajumbe wengine 10 watokane na asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma, jumuiya za
kidini na vyama vingine vya siasa ambavyo havina uwakilishi bungeni.
"Tunapendekeza
Mwenyekiti na Makamu wa Tume hiyo wachaguliwe na wajumbe wenyewe, ila
wasitokane na wajumbe kutoka vyama vya siasa kuepuka kuingiza ushabiki kwenye
utendaji wao," alisema Lissu.
Alisema
wajumbe hao wakishapendekezwa na makundi hayo, majina hayo yapelekwe bungeni
kwa ajili ya kuthibitishwa.
"Hapa
hakuna sehemu ambayo Rais anateua wajumbe, hivyo Tume hii haitaogopa kutangaza
matokeo ya Rais…sisi tunatamani kuwa na Tume huru badala ya hii ya sasa hivi
ambayo ni mali ya Rais."
Kuhusu
Muungano, chama hicho kilipendekeza ili kuepusha kuvunjika kuwe na Serikali ya
Tanganyika na Zanzibar zote ziongozwe na Rais, Bunge na Serikali yake na pia
kuwe na Serikali ndogo ya Muungano itakayoshughulikia mambo saba tu.
Baadhi
ya mambo hayo ni Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje upande wa diplomasia. Pia Rais
wa Muungano achaguliwe na mamlaka mbalimbali kama wabunge, mameya na magavana
wa majimbo.
"Huyu
anaongoza mambo machache, haina haja ya kuchaguliwa na wananchi wote, badala yake
achaguliwe na viongozi wa mamlaka zitakazopendekezwa kwenye Katiba,"
alisema.
Aliongeza
kuwa kwa upande wa serikali za Tanganyika na Zanzibar kuwe na serikali yenye
wizara zisizozidi 18.
Pia
Bunge la Tanganyika liwe na mfumo wa mabunge mawili moja la wananchi ambalo
litakuwa na wabunge 250 na lingine la majimbo ambalo litakuwa na wabunge 50.
Walipendekeza
kila nchi iwe huru kujitoa kwenye muungano iwapo itaona haifadiki ila wananchi
wa upande wa nchi husika inayotaka kujiondoa wapige kura ya maoni na uamuzi huo
ufikiwe baada ya kupatikana kwa theluthi mbili ya wapiga kura wote.
Mfumo
wa Serikali uwe wa majimbo ili kuondoa ukabila ambao umepangwa kimkoa na
kiwilaya. Walisema mfumo wa mikoa na wilaya ambao ulianza mwaka 1962 ulifanywa
kikabila.
Alisema
chama chake kinapendekeza Tanganyika iwe na majimbo yasiyozidi 10 na kwa kuanza
na majimbo tisa ambayo ni Nyanza Magharibi ambalo litakuwa na mikoa ya Kagera,
Geita na Shinyanga na Nyanza Mashariki lenye mikoa ya Mara, Mwanza na Simiyu.
Jimbo
la Ziwa Tanganyika litakuwa na mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Jimbo la Kati
litakuwa na mikoa ya Tabora, Dodoma,
Singida na Iringa. Jimbo la Kaskazini litakuwa na mikoa ya Kilimanjaro, Arusha
na Manyara.
Pwani
Kaskazini iwe na mikoa ya Tanga, sehemu ya Mkoa wa Pwani na sehemu ya Mkoa wa
Morogoro huku jimbo la Pwani ya Kusini likiwa na mikoa ya Mtwara, Lindi na
wilaya za Mafia, Rufiji na Ulanga.
Lissu
alisema jimbo lingine ni la Mji Mkuu la Dar es Salaam ambalo litakuwa na
manispaa tatu za mkoa huo na Nyanda za Juu Kusini lenye mikoa ya Njombe, Mbeya
na Ruvuma.
Katika
mapendekezo yao walisema majimbo yatasaidia kuwa na rasilimali mbalimbali
mchanganyiko na pia majimbo hayo yataongozwa na magavana ambao watachaguliwa.
"Hapo hakuna kuchagua mtu kwa misingi ya kabila, kwani jimbo moja litakuwa
na makabila zaidi ya mawili."
Maoni
ya CUF
CUF,
kwa upande wake ilipendekeza kuwapo Katiba tatu zitakazoongoza serikali za
Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.
Akizungumza
baada ya kutoa maoni yao katika Tume ya
Katiba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, kila nchi inapaswa iwe na
Katiba ambayo itawawezesha wananchi husika kuendesha mambo yao.
Alisema
pia kuwapo Katiba mama ambayo ni Hati ya Muungano ikizungumzia na kusimamia
mambo ya Muungano ambayo pande mbili zitakuwa zimekubaliana.
Lipumba
alisema kuwapo serikali tatu, kutatoa nafasi kwa Serikali ya Tanganyika
kusimamia mambo yake ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Serikali ya Muungano na
Zanzibar kutoona kuwa wanaonewa.
“Tukisema
iwe serikali moja hilo kwa Zanzibar halikubaliki, tukiendeleza mfumo uliopo,
bado una matatizo, hivyo ni heri kukawa na serikali tatu; ya Muungano itakuwa
ikisimamia masuala ya Muungano.
“Kwa
mfano tunataka masuala ya ulinzi na Jeshi la Polisi yawe ya Muungano, na pia
Mambo ya Nje isipokuwa ushirikiano wa kiuchumi ni lazima kila nchi isimamie
kivyake. Mambo ya kilimo, michezo na mengine kila serikali isimamie kivyake,”
alisema.
Akizungumzia
uchaguzi, Lipumba alisema wamependekeza kuwapo kwa mgombea binafsi katika urais
na rais apatikane kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa,
ikiwa ni tofauti na utaratibu wa sasa ambapo mshindi anapatikana kwa idadi
kubwa ya kura.
Alisema
katika ubunge na udiwani utumike mfumo wa kura za uwiano ambako kura zinapigwa
kwa chama na chama kitatoa uwakilishi kulingana na asilimia ya kura ambazo
kimepata na kuwa utaratibu huo utafanya kuwepo uwiano sawa wa kijinsia.
“Hatutaki
viti maalumu, mfumo wa kura za uwiano zitafanya kuwapo na uwakilishi sawa
bungeni na kwenye nafasi za madiwani. Kinachotakiwa kutoa orodha ya wagombea
wake katika mkoa na wananchi watapigia kura chama na kitakachopata kura nyingi
kitatoa wabunge zaidi. Hapa kura itakuwa na thamani.”
Lipumba
aliongeza: ‘Endapo mbunge au diwani ametangulia mbele za haki, chama
kilichokuwa kinashikilia jimbo hilo kichague mwingine ili kupunguza gharama za
uchaguzi mdogo.”
Aidha,
kuhusu uteuzi wa Tume ya Uchaguzi, Lipumba alisema wajumbe wateuliwe kutokana
na mapendekezo ya vyama vya siasa vyenye wabunge, asasi za kiraia
zinazoshughulika na uongozi na jamii, Msajili wa Vyama, uwakilishi wa wanawake,
wazee, vijana, walemavu, mwakilishi mmoja wa dini ya Kiislamu na mmoja wa
Kikristo ambao ndio watachagua mwenyekiti na makamu wao.
Akizungumzia
mfumo wa serikali, Lipumba alisema madaraka ya rais ni lazima yadhibitiwe na
Bunge ambapo uteuzi wowote wa rais ukiwamo wa mawaziri ni lazima uthibitishwe
na Bunge.
“Rais
anapoteua mwanasheria wa serikali, mkaguzi wa fedha za serikali, jaji mkuu,
mkuu wa majeshi au mawaziri uteuzi wao lazima uthibitishwe na Bunge. Hii
itasaidia watu kuacha kugombea ubunge ili waje kuwa mawaziri, bali wagombee ili
wawatumikie wananchi,” alisema.
Lipumba
alisema pia wametaka Katiba itaje idadi kamili za wizara ambazo zinatakiwa kuwa
kati ya 15 hadi 20 na kama kunahaja ya kubadili basi Bunge lihusishwe. “ Hii
itapunguza mzigo kwa Serikali.”
Tume
yajitetea
Naibu
Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Casmir Kyuki alipoulizwa sababu ya
kufanya mikutano hiyo kwa siri bila wanahabari, alisema uongozi wa Tume hiyo
umeamua kwa nia nzuri kuwa mikutano yake na makundi mbalimbali iwe ya ndani.
"Hii
ni kwa sababu Tume inataka kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo kutoka wa
viongozi wa makundi hayo, ndio maana utaona kuwa hata utaratibu wa kukaa nao ni
tofauti na ule tuliokuwa tunautumia mbele ya wananchi," alisema Kyuki.
Alisema
miongoni mwa mambo ambayo wajumbe wanawauliza viongozi wa makundi hayo ni
misimamo ya vyama vya siasa pamoja na baadhi ya maoni ambayo tulipata kutoka
kwa wananchi ambayo tunaamini kuwa yametokana na misimamo ya vyama vya siasa.
Alisema
licha ya vyama vya siasa makundi mengine ambayo yataitwa na Tume ni jumuiya za
kidini, asasi za kiraia, viongozi wa kiserikali, vyama vya kitaaluma, sekta
binafsi, vyama vya wafanyakazi, wamiliki na waandishi wa habari.
"Hatuamini
kuwa kufanya mikutano hii kwa siri tunawanyima wananchi uhuru wa kupata habari,
ila kwa kuwa wananchi walishatoa, Tume inahitaji ufafanuzi wa baadhi ya mambo
kutoka kwa viongozi wa makundi haya," alisema.
Kuhusu
vyama vitakavyoitwa, Kyuki alisema ni 20 vyenye usajili wa kudumu na kuwa CCM
ambayo jana wajumbe wake walifika mbele ya Tume, ilishatuma maoni yake mwaka
jana, lakini jana waliuondoa waraka wa kwanza na kuwasilisha mpya.
0 comments:
Post a Comment