KESI ya mauaji ya
kutokukusudia inayomkabili msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael “Lulu”
imepokelewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam na kusajiliwa kwa namba
125 ya mwaka 2012.
Kwa mujibu wa habari
zilizopatikana mahakamani hapo, kesi hiyo imepokelewa kutoka Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu nainasubiri kupangiwa Jaji na tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali Lulu alikuwa
akikabiliwa na mashitaka ya kumuua msanii mwenzake Steven Kanumba kwa kukusudia
lakini baada ya upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi alibadilishiwa
mashitaka na kuwa kuua bila kukusudia.
Kesi hiyo
ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Augustina Mmbando, katika hatua za awali na
Lulu hakuruhusiwa kujibu mashitaka yanayomkabili kwa kuwa Mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria,
kutokana na Lulu kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata
dhamana.
Desemba 21 mwaka huu,
Lulu alisomewa maelezo ya kesi na ushahidi utakaotumika na upande wa mashitaka
katika kesi hiyo, ambapo Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro alidai kuwa
watakuwa na mashahidi tisa, ushahidi wa nyaraka, ripoti ya uchunguzi wa
hospitali na ramani ya eneo la tukio.
Baadhi ya mashahidi
watakaotoa ushahidi ni pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, Sofia Kassim,
Daktari wa marehemu aitwaye Pancras Kageigwa, Morris Semkwao na Esther Zephania
ambaye ni askari Polisi wa kituo cha Oysterbay, Kinondoni.
Katika kesi hiyo,
inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwa Steven Kanumba, Sinza Vatican,
jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua bila kukusudia msanii huyo nyota wa filamu
nchini.








0 comments:
Post a Comment