
Siku chache baada ya kuachia video ya wimbo wake - ‘NINGEFANYAJE’, muimbaji wa R&B kutoka Tanzania, Bernard Paul maarufu kama Ben Pol ameeleza sababu zilizopelekea muimbaji Avril kutoka Kenya aliyeshirikishwa kwenye wimbo huo, kutoonekana kwenye video hiyo anayoitaja kuwa kubwa kuliko video zote alizowahi kufanya.
Katika video hiyo
iliyoongozwa na Justin Campos wa Afrika Kusini, Ben Pol anaonekana akiimba na
Rossie M ambaye pia ameshirikishwa kwenye wimbo huo huku mashabiki
wakiisikia sauti ya Avril bila kumuona mwimbaji huyo mrembo.
Ben Pol amewaomba radhi
mashabiki wake kwa kuwapa video ambayo haijakamilisha wahusika wote hususan
kutokuonekana kwa Avril, na kwamba sababu zilizopelekea hivyo zilikuwa
nje ya uwezo wa pande zote katika utayarishaji wa video hiyo.
Ben amesema kuwa baada ya yeye na Rossie M kuwasili Afrika
Kusini ilikoshutiwa video hiyo, zilijitokeza changamoto muda mfupi kabla ya
kuanza zoezi hilo. Ben Pol ameeleza kuwa pamoja na kuwa na maandalizi
makubwa, video ya ‘Ningefanyaje’ ilikumbwa na changamoto nyingi tangu awali
zilizopelekea kuahirishwa mara tatu.
“Kwa kweli hii video tokea
mwanzo ilikuwa na changamoto, kwanza tuliisogeza mbele karibu mara tatu tena
tukiwa tayari tumeshafika Afrika Kusini mimi na Rossie,” alisema Ben Pol. “Mara
ya kwanza ni kutokana na ‘delay’ ya viza upande wa Avril. Si unajua Wakenya wao
wanaenda South kwa viza tofauti na sisi Tanzania hatuendi kwa viza so kwetu ni
rahisi zaidi muda wowote tu ukiamua fasta unaenda,” aliongeza.
Mkali huyo alieleza kuwa
baada ya terehe mpya kupangwa na muongozaji aliyeshuti video hiyo, Justin
Campos, siku moja kabla ya kushuti, AVRIL alipata tatizo lingine ambalo
lilimzuia kusafiri kwa siku iliyofata kwenda Afrika Kusini.
Wakati huo huo, Campos naye
alimueleza Ben Pol kuwa kwa jinsi ratiba yake ilivyo endapo ataahirisha
tena kushuti video hiyo, ratiba yake isingemruhusu kushuti video hiyo hadi
Januari au Februari 2016, kitu ambacho Ben Pol amesema kisingewezekana
kwasababu ingeendelea kumgharimu zaidi kifedha na kuvuruga ‘timing’ yake.
“Kutokana na hali hiyo,
sikuwa na jinsi nyingine zaidi ya kukubali matokeo kwasababu mwisho wa
siku si mimi wala Avril wala director aliyekwamisha bali ni ‘situation’ ambayo
ilikuwa nje ya uwezo wa kibinadamu.” Ben Pol anaeleza.
Ameongezea kuwa pamoja na
kwamba angeweza kuamua kushuti video kwa kutumia version nyingine ya wimbo huo
isiyokuwa na sauti ya Avril ili video isionekane na upungufu wake, lakini
hakupenda kufanya hivyo kwa kuwa lengo kuu la wimbo lilikuwa kumshirikisha
mwimbaji huyo. Pia, mashabiki wangekosa ladha nzuri na kazi nzuri aliyoifanya
Avril. Hivyo, aliamua kufanya video hiyo bila Avril na kukusudia
kuwaeleza mashabiki wake kilichosababisha hali hiyo kwa kuwa aliamini mashabiki
wataelewa magumu aliyopitia katika kuwapa video hiyo waliyokuwa wakiisubiri.
“Namshukuru sana Avril kwa
kukubali kufanya kazi na mimi kwasababu imetimiza moja kati ya malengo yangu ya
2015, ambayo ilikuwa kuanza kufanya kazi na wasanii wa nje ya Tanzania na yeye
ndiye alikuwa chaguo langu la kwanza. Ni imani yangu tutafanya tena project
nyingine ya pamoja na kuikamilisha kama tulivyoikusudia,” alimaliza Ben Pol na
kuwashukuru mashabiki wake kwa kuupokea kwa mtazamo chanya wimbo na video
yake.
ITAZAME VIDEO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment