KATIKA hali inayoashiria ukubwa wa tatizo la ajira
katika sekta rasmi nchini, juzi wasomi wa ngazi ya Chuo Kikuu 10,500
walijitokeza jana kwenye usaili wa Idara ya Uhamiaji nchini inayohitaji kuajiri
watu 70 tu.
Wengi wakiwa ni vijana wasomi wa fani mbalimbali wenye
umri wa kati ya miaka 22 na 30, walifurika kwenye uwanja huo uliopo Kurasini,
katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam kuanzia saa 12 asubuhi.
Idadi hiyo inahusisha waombaji wa ajira walioitwa na
idara hiyo kutoka kundi la waombaji 20,000.
Idadi ya waombaji hao walijiotokeza katika usaili huo
ilithibitishwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Namtanga,
aliyekiri ni usaili wa kihistoria kutokana na kuhusisha waombaji wengi kwa
wakati mmoja.
“Kwa kweli huu ni usaili wa kihistoria, hatujawahi
kupata maombi mengi kama haya, wote waliotuma ni wale wenye sifa kielimu ambayo
ni kuwa na shahada ya kwanza ya fani tulizozitaja hapo awali,” alisema.
Alifafanua kuwa, Wizara kupitia matangazo ya nafasi
hizo za ajira katika vyombo vya habari yaliyotolewa mapema mwanzoni wa mwaka
huu, yaliainisha nafasi zinazohitaji watu na sifa zake ambapo katika nafasi ya
kwanza ni ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji iliyohitaji watu
70.
Sifa za nafasi hiyo ni pamoja na waombaji kuwa na
elimu ya Shahada ya Kwanza katika fani za Uchumi, Biashara, Utawala, Uandishi
wa Habari, Ualimu, Usafirishaji, Rasilimali Watu na Sayansi ya Kompyuta.
Nyingine ni Habari na Mawasiliano, Takwimu, Uchapaji,
Uhandisi Majengo na Uhandisi Mitambo.
“Na masharti yalitaka waombaji hao wawe na umri
usiozidi miaka 35, jambo ambalo waombaji wote 20,000 waliotuma maombi yao
walikuwa na sifa hizo hivyo ikabidi wachujwe ili kupata waombaji watakaoitwa
kwenye usaili.
“Hii inaonesha kuna uhaba mkubwa wa ajira, na waombaji
wote wana sifa hiyo ya shahada na umri, sasa tulifanya usaili kwa makini
tukapata hao zaidi ya 15,000 tumejitahidi na tumewaita wengi ili waje wachuane
kwenye usaili tupate hao 70,” alisema Namtanga.
Akizungumzia jinsi watakavyopata waombaji wenye sifa
ikiwa wote waliotuma maombi wanasifa tajwa, Namtanga alisema pamoja na
kuangalia sifa ya elimu, lakini pia wataangalia na ufahamu wa mambo mengine ya
kijamii.
Alisema hiyo ni
ili kupata waombaji wenye upeo mkubwa hasa kwa kuwa wengi wao wana sifa
kielimu, hivyo kuitwa kwao kwa wingi ni kutoa mwanya kwa wao kuchuana kwa uwazi
na kupata waombaji kwa haki.
Kwa upande wa waombaji hao, baadhi ya waliozungumza na
gazeti hili baada ya kutoka kwenye usaili huo walisema, ni usaili mgumu kwani
una ushindani wa hali ya juu.
“Sijawahi kufanya usaili wa watu wengi kama huu,
nafasi zinazohitajika ni 70, ila tulikuwa zaidi ya 10,000 sasa unaona wazi
kwamba ni lazima ufanya kwa makini ili kushindania nafasi hizo”, alisema mmoja
wa waombaji hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Aliongeza, hali hiyo inaonesha jinsi gani vijana wengi
wana uhaba wa ajira, kwani kwa nafasi hizo 70, maombi ni mengi na yanavunja
historia ya usaili wa nafasi nyingine mbalimbali zilizowahi kutangazwa.
Alisema katika usaili huo, waliufanya kwa kugawanywa
kwenye makundi mawili, ambapo walitumia Uwanja wa Taifa kufanyia kwa kuketi
kwenye viti vya watazamaji mithili ya waliokuwa wanaangalia pambano la soka
kwenye uwanja huo wa kisasa wa michezo nchini.
Kuhusu usimamizi na ulinzi wakati wa usaili, mmoja wa
wasaili hao alisema wasimamizi walikuwa wa kutosha wakiongozwa na Maofisa
kutoka Uhamiaji, Magereza na baadhi ya maofisa kutoka Utumishi.
“Usimamizi ulikuwa mzuri na walikuwepo wasimamizi wa
kutosha, tulifanya kwa makundi mawili moja lilikuwa chini uwanjani na wengine
walipanda juu kwenye jukwaa la watazamaji, tulifanya mtihani wa kuandika,
ulikuwa mzuri tu, ndio tusubiri tuone majibu,” alisema mmoja wa waombaji hao
aliyeshukuru magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla kwa mchango wao mkubwa
katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwa pamoja na nafasi za
ajira zinazotangazwa.
Hata hivyo Namtanga alisema , baada ya usaili huo
kukamilika, watafanya uchambuzi na watachagua watu waliofanya vizuri kwa ajili
ya usaili wa pili wa kuzungumza.
“Tumejipanga vizuri, tunategemea kazi hii itafanyika
kwa utulivu na tutapata watu wenye sifa na ufahamu wa mambo ya kijamii kwani ni
moja ya sifa ya ziada,” alisema Namtanga.
Alisema watakaopata nafasi hizo watakuwa na majukumu
mbalimbali yakiwemo kusimamia doria sehemu za mipakani, bandarini vituo vya
mabasi, kusimamia shughuli za upelelezi, kuandaa hati za mashtaka, kukagua na
kusimamia hati za safari na majukumu mengineyo.
Wakati wasomi hao wakionesha kiu ya ajira katika sekta
rasmi, katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikisisitizwa umuhimu wa wasomi
kujiajiri kutokana na ajira rasmi kuwa na nafasi chache, si kwa Serikali ya
Tanzania pekee, bali kote duniani.
Ends
Halmashauri 80 kuvuna
bil. 40/- nyumba za walimu - THIRD
Na Nelson Goima, Dodoma
SERIKALI inatarajiwa kutoa Sh bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba za walimu katika halmashauri 80 nchini, sawa na Sh Sh milioni 500 kwa
kila halmashauri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya aliposoma Hotuba ya Serikali kwa
mwaka wa fedha wa 2014/15.
Alisema hayo mjini hapa juzi, wakati akielezea matumizi ya fedha kwa
makundi maalumu, hasa kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu.
Waziri huyo alisema serikali inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa
nyumba za walimu kwa awamu.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14, halmashauri 40 zilipewa kila moja
Sh milioni 500 ili zianze ujenzi wa nyumba za
walimu. Kiasi kama hicho, kitatolewa katika halmashauri hizo kwa mwaka 2014/15.
“Aidha, Sh milioni 500 zitatolewa kwa halmashauri 80 zaidi, hivyo
kufanya jumla ya halmashauri 120 kunufaika na utaratibu huo, lengo likiwa ni
kuzifikia halmashauri zote mwaka 2015/16”, alisema.
Aliwahimiza viongozi wa Serikali katika ngazi za mikoa, wilaya na
kata, kusimamia kikamilifu fedha hizo ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu malipo ya madai ya walimu, alisema serikali inaendelea kulipa
madai ya walimu yaliyohakikiwa, ambapo katika mwaka 2014/15 kiasi cha Sh
bilioni 5.6 kimelipwa.
“Aidha, kwa mwaka 2014/15 madai ya walimu ambayo yatakuwa
yamehakikiwa, yataendelea kulipwa.
Aidha, Waziri huyo alisema uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule ya msingi, umeimarishwa kutoka 1:47 mwaka 2012 na
kufikia 1:43 mwaka 2013, ikilinganishwa na lengo la uwiano wa 1:40. Katika
elimu ya sekondari, uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi ulifikia lengo la MKUKUTA
II la 1:28 mwaka 2013.
CHANZO: HABARILEO







0 comments:
Post a Comment