Sehemu ya waandishi wa habari walioshiriki mkutano huo katika Idara ya Habari (Maelezo).
Picha ya pamoja, kutoka kulia ni Balozi wa China, Mhe. Lu Youqing; Katibu Mkuu, Bw. John M. Haule; Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Nathaniel
D. Kaaya; Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya
Mambo ya Nje, Bibi Mindi Kasiga na Afisa kutoka Ubalozi wa China
HOTUBA
YA BW. JOHN HAULE, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
KIMATAIFA WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI JUU YA MAFANIKIO YA ZIARA YA
MHE. XI JINPING, RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, NCHINI TANZANIA, UKUMBI WA
HABARI MAELEZO, DAR ES SALAAM, TAREHE 25 MACHI, 2014
Mheshimiwa
Balozi Lu Youqing, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania,
Wakurugenzi
wa Idara na Wakuu wa Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa,
Ndugu
waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya umma na binafsi,
Mabibi
na Mabwana,
Ni
heshima kubwa na furaha kwangu kujumuika na wenzetu wa Ubalozi wa China
katika siku hii ya leo, kwa ajili ya kuelezea mafanikio ambayo Tanzania na
China zimepata kutokana na mahusiano ya muda mrefu na ya kidugu katika nyanja
za kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kijamii. Mwaka huu, Tanzania na China
zinajivunia kuadhimisha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia ambayo yamekuwa
na mafanikio makubwa kwa nchi hizi mbili. Ikumbukwe kwamba, moja ya vielelezo
vikubwa kabisa vya ushirikiano wa nchi hizi mbili ni Reli ya TAZARA, Kiwanda
cha Nguo cha Urafiki na kwa wale wapenzi wa Soka, ni Uwanja wa Kisasa wa Mpira
wenye Uwezo wa Kuchukua Watu elfu sitini (60,000) wakiwa wamekaa.
Kama mnavyofahamu, katika kipindi cha mwaka
2013, Tanzania ilipata bahati ya kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika
kutembelewa na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China tangu
ateuliwe kuwa Rais wa nchi hiyo. Vilevile, kupitia ziara hiyo, Mheshimiwa Rais
Xi Jinping alipata fursa ya kutangaza Sera ya Mambo ya Nje ya China kwa bara la
Afrika, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere. Hii inaonesha
si tu historia ya uhusiano mzuri na madhubuti uliopo baina ya Tanzania na
China, bali pia utayari wa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali za kimaendeleo zinazotokea hivi sasa duniani kote.
Ziara ya Rais Xi Jinping nchini Tanzania,
iliyofanyika mwaka mmoja uliopita ilikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa
kidiplomasia na kidugu ulioanza tangu mwaka elfu moja mia tisa sitini na nne
(1964) pamoja na kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili. Ziara
hiyo ilishuhudia kusainiwa kwa Mikataba mbalimbali katika nyanja za kilimo,
miundombinu, afya, nishati, utamaduni pamoja na teknolojia ya habari na
mawasiliano.
MAFANIKIO
YA ZIARA YA MHESHIMIWA RAIS XI JINPING NCHINI TANZANIA
Mahusiano ya watu-kwa-watu kati ya Tanzania
na China
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Mahusiano ya watu-na-watu kati ya Tanzania
na China ni mazuri na yanazidi kukua siku hadi siku. Tangu kufanyika kwa ziara
ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini, takwimu ya idadi ya wageni wenye uraia kutoka
China waliotembelea Tanzania kwasababu mbalimbali zikiwemo utalii na biashara inakadiriwa
kuongezeka kutoka 10,790 mwaka 2013 hadi kufikia takribani 11,555 mwaka 2014.
Wakati huohuo, idadi ya Watanzania waliotembelea China inakadiriwa kuongezeka
kutoka 7,657 mwaka 2013 hadi kufikia takribani 8,114 mwaka 2014.
Kwa upande mwingine, ziara ya Mhe. Rais Xi
Jinping nchini imekuwa chachu kwa viongozi wa ngazi za juu kutoka Serikali ya
Tanzania na China kutembeleana kwa nyakati tofauti. Ziara hizo zimeendelea kuwa
ishara ya mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo baina ya nchi hizi mbili.
Kwa mfano; kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ujio wa Mhe. Rais Xi Jinping
nchini, viongozi mbalimbali wa Kitaifa na wa ngazi za juu wa Tanzania
walitembelea China. Viongozi hao ni pamoja na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye alifanya ziara ya
kikazi nchini China kuanzia tarehe 27 Mei hadi 02 Juni, 2013. Wakati wa ziara
yake, jumla ya Mikataba minne (4) ya maendeleo katika nyanja za Afya, Bahari,
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Mafunzo, iliwekwa saini
kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China.
Vilevile, Mhe. Mizengo Pinda (Mb.), Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizuru nchini China Mwezi Oktoba,
2013. Kupitia ziara ya Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya China ilitoa ahadi ya
kuipatia Tanzania msaada wa fedha kiasi cha Yuan million 200 (sawa na dola za
Kimarekani milioni 33) na mkopo wa masharti nafuu wa Yuan milioni 100 (sawa na
dola za kimarekani milioni 16). Vilevile, Serikali ya China imekubali kuendelea
kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo katika
mpango wa “Matokeo Makubwa Sasa- (BRN)” ambayo Serikali ya Tanzania tayari
imekwisha iwasilisha kwa Serikali ya China.
Kufuatia ziara hiyo ya Mhe. Waziri Mkuu
nchini China, Mikataba na Makubaliano mbalimbali takriban kumi na miwili (12)
iliwekwa saini. Mikataba hiyo inahusu sekta ya nishati na uzalishaji umeme,
kuanzisha ukanda maalum wa viwanda kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa za
Tanzania nje, uendelezaji wa sekta ya nyumba na makazi pamoja na ushirikiano wa
kitaalamu katika sekta ya sayansi na teknolojia.
Kwa
upande wa Serikali ya China, Mhe. Yang Huanning, Naibu Waziri wa Usalama wa
Umma wa China alitembelea Tanzania mwezi Mei, 2013. Vyombo vya Usalama vya
Tanzania na China vimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha usalama wa nchi
hizi mbili hususan kupambana na uhalifu wa kimataifa kama vile biashara za
pembe za ndovu, meno ya tembo na madawa ya kulevya.
Madhumuni ya ziara hizo za viongozi hao wa
ngazi za juu kutoka Serikali za Tanzania na China yalikuwa ni kuimarisha
ushirikiano wa kidugu uliopo na wa muda mrefu na kuimarisha mahusiano yaliyopo
katika nyanja mbalimbali hususan za kiuchumi na biashara.
Mikataba
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Wakati wa ziara ya kihistoria ya Rais Xi
Jinping jumla ya Makubaliano na Mikataba kumi na sita (16) kati ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China iliwekwa saini pamoja na
misaada mbalimbali kutolewa. Baadhi ya Mikataba na Makubaliano hayo yameanza
kutekelezwa; na mingine kufikia hatua nzuri za utekelezaji.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda na
wingi wa Makubaliano ambayo nchi hizi mbili ziliafikiana wakati wa ziara ya
Rais Xi Jinping, nitatumia sehemu ya muda niliopewa kutoa mifano michache ya
mafanikio na matarajio ya utekelezaji wa baadhi ya miradi hiyo ya maendeleo kwa
kipindi cha mwaka mmoja tangu kuwekwa saini kwa Makubaliano hayo.
Kilimo
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kwa upande wa
kilimo, Serikali ya China imefungua milango kwa zao la tumbaku ya Tanzania
kuuzwa nchini humo kutokana na utekelezaji wa Mkataba unaohusu Masharti ya Afya ya Mimea kwa majani ya Tumabaku
inayotoka Tanzania. Mkataba huo ambao uliwekwa saini wakati wa ziara ya
Mhe. Rais Xi nchini unatoa fursa ya soko la Tumbaku ya Tanzania nchini China na
hivyo kuchangia katika kuleta urari wa biashara. Hivi sasa, bidhaa za tumbaku
zaa Tanzania zinaruhusiwa kuuzwa katika soko la China.
Uwekezaji
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Tanzania na China
zimeingia Mikataba mbalimbali kwa lengo la kukuza biashara na kuongeza
uwekezaji. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba
unaohusu Msaada wa Fedha za Miradi ya Maendeleo nchini Tanzania na ule wa
Uimarishaji na Kulinda Uwekezaji.
Utekelezaji wa
Mikataba hiyo utasaidia kufikia Malengo yetu ya Dira 2025 kupitia utekelezaji
wa Miradi mbalimbali iliyopo chini ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011-2016) na Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now). Vilevile,
Mkataba wa Kuimarisha na Kulinda Uwekezaji ni mmoja ya Mikataba muhimu ya
kiuchumi ambayo inalenga kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini hivyo,
hutoa nafasi nzuri ya kukuza na kuvutia uwekezaji kutoka kwa makampuni makubwa
ya China.
Ndugu Waandishi
wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Tayari Makampuni ya
China yameonyesha nia ya kuwekeza katika Sekta ya Nishati nchini. Kampuni ya
Nishati ya China {China Power Investment
(CPI)} inatarajia kuwekeza katika Mradi wa Kuzalisha MegaWatts 300 za Umeme
(300MW) ujulikanao kama Kinyerezi III. Kadhalika, Kampuni nyingine ya Kichina
ya Poly Technologies nayo inahusika
katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Kinyerezi IV wa 330MW ambazo zinategemea
kuongezeka hadi 450MW. Miradi hii ya Kinyerezi kwa kiasi kikubwa itaondoa
tatizo la upatikanaji wa Nishati hiyo hapa nchini na hivyo kuwahakikishia
wananchi, pamoja na wawekezaji, upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wakati wote
na kwa kiwango cha kutosha.
Kampuni ya Poly Technologies pia imeingia
Makubaliano na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yenye thamani ya Dola za
Kimarekani milioni 200 (USD 200 Million) kwa ajili ya uendelezaji wa sekta ya
makazi nchini (real estate development).
Miradi ya Mikopo
Nafuu na Misaada
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Katika juhudi za
Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, Tanzania na China
zinashirikiana kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji wa nishati ya umeme
kupitia gesi; mfano ukiwa ni mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara
kuja Dar es Salaam kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya umeme. Mradi huo
unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, si tu utaiwezesha Tanzania
kuzalisha nishati ya umeme ya kutosha kwa matumizi ya ndani pamoja na kuuza nje
ya nchi, lakini pia umekuwa ukitoa ajira kwa Watanzania wengi. Mradi huu
unatekelezwa sanjari na miradi mingine ya uzalishaji umeme kama ule wa
usafirishaji kupitia korido la Kaskazini na Kusini {North East Power Transmission Line (400kV) Dar-Chalinze-Arusha and
North West Power Transmission Line (220kV) Nyakanazi-Kigoma-Mpanda-Rukwa-Mbeya}
na ya Kinyerezi.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama mtakavyoona,
miradi ambayo Tanzania na China inaitekeleza ina umuhimu mkubwa katika
kuchangia maendeleo ya Taifa letu na hivyo kusaidia katika juhudi za Serikali
ya Tanzania za kupambana na umasikini. Kwa mfano, Kampuni ya Sichuan Hongda
Group ya China inashirikiana na Shirika la Maendelo la Taifa (NDC) kutekeleza
Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. Miradi hiyo yenye
thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni Tatu (USD 3 billion), inatarajiwa si tu
itachangia katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, bali pia,
inatarajiwa kutoa ajira zisizopungua elfu thelathini na tatu (33,000), kuongeza
pato la Taifa la fedha za kigeni la Shilingi bilioni 1.73 kwa mwaka pamoja na
kusaidia uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya chuma nchini.
Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Utekelezaji
wa Mradi wa Taifa wa Miundombinu ya TEHAMA Awamu ya III umeanza kutekelezwa. Mradi huu wa Taifa
unalenga kusambaza miundombinu na kuiunganisha mikoa yote nchini kwa lengo
la kuwawezesha wananchi wa ngazi zote
kupata habari za uhakika, za kuaminika na kwa wakati na pia, kupata huduma za
TEHAMA kwa gharama nafuu na ufanisi.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kadhalika, katika
kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata habari za uhakika na kwa wakati,
Serikali ya Tanzania na China zilibadilishana Hati kuhusu kulipatia Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) Gari
Maalumu la Matangazo ya Runinga (TV
Broadcast Truck). Makabidhiano ya gari hilo maalumu yatakayofanyika
mwezi ujao (Aprili, 2014), pia yanajumuisha ujio wa timu ya wataalamu kutoka
China kwa ajili ya kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya gari hilo la kisasa.
Ni dhahri kuwa,
upatikanaji wa habari na huduma za mawasiliano na teknolojia unachangia kujenga
jamii yenye maarifa na ufahamu, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na
kiuchumi.
Uchukuzi
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kwa upande wa sekta
ya uchukuzi, Tanzania na China ziliingia Mkataba
wa Ubia kuhusu kuendeleza Bandari na Eneo la Viwanda la Bandari kwenye eneo
Maalumu la Uwekezaji la Bagamoyo. Hadi hivi sasa, hatua zilizofikiwa za
utekelezaji wa Mradi wa Bandari ya
Bagamoyo ni za kuridhisha. Ni mategemeo yetu kwamba kukamilika kwa miradi
hiyo kutakuza uchumi wa nchi kwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa Watanzania
katika viwanda hivyo vya uzalishaji na miradi hiyo pia itaimarisha sekta ya
viwanda vya uzalishaji wa bidhaa zenye thamani za Tanzania na kuwezesha bidhaa
hizo kuingia katika soko la ushindani la biashara nje ya nchi.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kadhalika, katika
kukuza ushirikiano wa karibu wa kuimarisha usalama, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imepokea vifaa vya kisasa vya kukagua makontena katika bandari ya
Zanzibar. Vifaa hivi vinavyotumia teknolojia ya kisasa vimefika kwa wakati
kwani vitasaidia katika kuimarisha usalama wa shughuli za bandari ikiwemo
ukaguzi wa mizigo na bidhaa zinazoingia na kutoa kupitia Bandari hiyo.
Afya
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Katika sekta ya
Afya, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya China zimekubaliana
kutekeleza mradi wa ukarabati wa hospitali ya Abdullah Mzee ya mjini Pemba.
Katika kufanikisha
utekelezaji wa Mradi huo, hatua mbalimbali zimekwisha chukuliwa zikiwa ni
pamoja na; mchakato wa kulipa fidia kwa wakazi wanaoizunguka hospitali hiyo kwa
ajili ya kupisha ujenzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Utalii
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Itakumbukwa kuwa,
mwezi Machi, 2013, wakati wa ziara ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini, alimkabidhi
rasmi Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China.
Kituo hicho cha
Mikutano ambacho ni kikubwa kuliko vyote jijini Dar es Salaam,
kimekuwa chachu ya
kukuza na kutangaza Utalii wa Mikutano (Conference
Tourism) kutokana na uwezo wa kuhudumia Mikutano ya watu zaidi ya elfu moja
na mia nane (1,800) kwa wakati mmoja. Kadhalika, kituo hiki kina manufaa ya
kiuchumi kutokana na kutoa nafasi za ajira kwa wananchi na kukuza mapato ya
mara kwa mara kwa wakazi wa Dar es Salaam kutokana na biashara ya huduma
hususan wakati wa Mikutano mikubwa ya kimataifa.
Utamaduni
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama mnavyofahamu
‘Utamaduni ni Kioo cha Taifa’. Kwa kulitambua hilo, Serikali ya China iko mbioni kujenga kituo cha utamaduni cha Jamhuri ya
Watu wa China nchini (Chinese Cultural
Centre).
Lengo la kituo
hicho ni kukuza utamaduni wa China kwa kujifunza lugha, michezo na sanaa
mbalimbali za Kichina. Kadhalika, tayari Serikali ya China imeweza kufungua
Taasisi ya Kujifunza lugha ya Kichina (Confucius
Institute) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma. Taasisi hizi hudhamini masomo ya lugha
ya kichina nchini China na pia, kuhitimu lugha hiyo, huchukuliwa kama kigezo
kwa nafasi za ajira katika makampuni ya Kichina yaliyopo Tanzania.
Mahusiano ya
kijamii
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama nilivyokwisha
eleza awali, mahusiano kati yetu na China ni ya kidugu. Hili linadhihirishwa na
msaada wa vitu mbalimbali wenye thamani
ya Shilingi milioni 30 uliotolewa na Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya
Wafanyabiashara ya Wachina kwa
waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro mwezi Janauri, 2014.
Hii ni ishara tosha
ya kuonyesha kuwa, ushirikiano uliopo na China, haujaishia tu katika ngazi za
juu za Serikali, lakini pia katika ngazi za wananchi wa kawaida.
HITIMISHO
Ndugu
Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Ujio wa Rais Xi
Jinping nchini, mwaka jana umeimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China
hususan katika kipindi hiki tunachoelekea katika kilele cha kusherehekea
maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya
nchi hizi mbili. Maadhimisho haya ni ishara ya mshikamano wa kirafiki na udugu
ulipo kati ya nchi hizi.
Hivyo,
napenda kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania kwa ujumla, kutumia vyema fursa
za kibiashara na kiuchumi zinazotokana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu
kati ya nchi zetu.
Tanzania
na China zimeazimia kuendelea kufanya juhudi za pamoja kuimarisha ushirikiano
wa kirafiki, katika sekta mbalimbali na kuhimiza uhusiano na ushirikiano wa
kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.







0 comments:
Post a Comment