Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia
ramani ya ujenzi wa miradi mitatu ya uwanja wa ndege wa Zanzibar,
alipofanya ziara ya kutembelea miradi hiyo.
Mtathmini
wa viwango vya ujenzi wa miradi hiyo Bw. Mohd Juma, akitoa maelezo
mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhusiana na ujenzi huo.
Meneja wa Mradi wa ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa kuruka Frederick Nkya akionyesha ramani ya ujenzi huo.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria bw. Ibrahim Zhang, akimueleza Maalim Seif hatua zinazoendelea za ujenzi huo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Miundo mbinu
na mawasiliano, viongozi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar pamoja na
wakandarasi wa miradi ya ujenzi katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
(picha na Salmin Said, OMKR).
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea
kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miradi mitatu
inayoendelea kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Miradi
hiyo inahusisha ukarabati na ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa
kuruka pamoja na sehemu ya maegesho ya ndege, ujenzi wa uzio wa eneo la
uwanja wa ndege, pamoja na ujenzi wa jingo jipya la abiria (Terminal 2).
Akizungumza
katika ziara ya kutembelea miradi hiyo huko uwanja wa ndege wa
Zanzibar, Maalim Seif amesema hatua iliyofikiwa inatia moyo, na kuwataka
wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa inakamilika kwa wakati.
Amesema
Serikali kwa upande wake itaweka mkakati wa makusudi ili iweze kumaliza
kuwalipa fidia wananchi ambao bado hawajalipwa, na kuruhusu ujenzi wa
uzio uweze kukamilika kwa akati.
Mapema
meneja wa mradi wa ujenzi wa uzio huo Bw. Frederick Nkya, alimueleza
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwamba hadi sasa tayari asilimia 73
ya ujenzi huo imeshakamilika.
Hata
hivyo amesema changamoto kubwa inayowakabili ni eneo la mita elfu tatu
na mia moja ambapo sehemu kubwa ya eneo hilo bado wananchi hawajalipwa
fidia.
Amefahamisha
kuwa hadi sasa eneo la mita elfu mbili na mia saba ndilo ambalo
halijafanyiwa tathmini kuweza kuwalipa wananchi walioko katika maeneo ya
mradi huo.
Miradi
ya ukarabati na ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa kuruka
(Taxiway) pamoja na sehemu ya maegesho ya ndege (Apron) katika uwanja
huo inafadhiliwa na Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, ambapo mradi wa ujenzi wa uzio wenye urefu wa mita 11,690 katika
uwanja huo, unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pekee,
ambapo zaidi ya shilingi bilioni sita zitatumika hadi kukamilika kwa
mradi huo.
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria ambao awali ulikumbwa na
changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa eneo la mradi,
meneja wa mradi huo Bw. Ibrahim Zhang, amesema kazi hiyo sasa inaendelea
vizuri.
Mradi
wa ujenzi wa jengo jipya la abiria awali ulitiwa saini mwezi wa
Septemba 2009 baina ya Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano na Kampuni
ya ujenzi ya Beijing Construction Engineering Group ya China, lakini
baadae serikali iligundua kuwa ukubwa wa jengo uliopendekezwa mwanzo
haukidhi haja.
Hivyo
Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuongezwa ukubwa wa jengo kutoka
mita 15,600 hadi mita 17,800 kwa ongezeko la fedha dola za kimarekani
milioni 11.8, na kufanya gharama za mradi huo kufikia dola la
kimarekani milioni 82.2







0 comments:
Post a Comment