HALI ya mtawanyiko wa nchi kavu na maeneo
ya maji ni moja ya alama kuu za utambulisho kijiografia.
Ni kwa hali hiyo watu huweza kutofautisha
bara la Afrika, kwa mfano, na lile la Asia; la Ulaya na la Amerika Kusini au
Amerika Kaskazini na mengineyo.
Kadhalika sura ya nchi hutumika kueleza mazingira
ya maeneo tofauti, kuhusu mwinuko wake kutoka usawa wa bahari, pepo, jotoridi
na hali ya mvua au ukame.
Mabara yaliyopo sasa duniani
yametenganishwa kwa maji, eneo la maji likiwa
ni kubwa, tofauti na visiwa vikubwa na
vidogo visivyoweza kurejewa kama
mabara.
Haya ni Afrika, Amerika, Antarctica, Asia,
Australia ikiunganishwa na Oceania
na Ulaya ikiwa peke yake. Inatambulika kwamba
theluthi mbili ya dunia imefunikwa na maji, na pia theluthi mbili ya maeneo ya
nchi kavu yapo upande wa kaskazini mwa ulimwengu.
Lakini, wakati kadiri miaka inavyokwenda vitu
vingi vikitarajiwa kuongezeka,
mabara yanatabiriwa kupungua.
Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Yale, nchini
Marekani, wamekuwa akifanya utafiti wao
kwa muda mrefu kuhusu hali ya sura ya nchi, na sasa wanasema mabara yataungana,
kutokana na maeneo ya ardhi kuhama. Wanasema kwamba, kitakachotokea ni ardhi
inayounda bara la Amerika kusogea hadi kukutana na ile ya bara la Asia, ambayo
pia itakuwa ikihama
kwenye eneo lake la awali.
Kwa hiyo katika hali hiyo, mabara hayo
mawili yatagongana katika ncha ya
kaskazini ya dunia katika kipindi cha
kati ya miaka milioni 20 hadi milioni 200 ijayo.
Wanatabiri pia kwamba huenda Afrika na
Australia nazo zikaungana katika
bara kubwa kabisa, wanalolipa jina la ‘supercontinent’,
itakayokuwa alama ya
kuungana kwa maeneo husika ya ardhi ya
dunia. Mabara hayo yanadhaniwa
kwamba yalipata kuwa katika upamoja, yaani
kuwa bara moja siku zilizopita,
yapata miaka milioni 300 hivi iliyopita, ambapo
bara hilo kubwa liliitwa Pangea.
Maelezo ya kina kuhusu kuhama kwa ardhi
kulivyotokea na kutakavyotokea na maeneo yatakayohusishwa yameandikwa kwa kina
kwenye jarida mahsusi la kitaaluma la wasomi hao liitwalo ‘Nature’.
Wanasayansi hao wanasema kwamba, japokuwa
ni kitu kisichoweza kuonekana kwa macho,
kila siku inayokuja na kwenda, maeneo ya ardhi, kwa maana ya mabara, huwa
yanasogea kutoka eneo moja hadi jingine kwa kadiri ‘visahani’ vinavyoshikilia
mabara vinavyovunjika.
Wanasema kwamba mwendelezo huo wa kuhama
kwa ardhi ndiko umesababisha kuwapo maeneo yenye maumbo kama ya katikati ya
Atlantiki (Mid-Atlantic Ridge), ambapo paliundwa Iceland. Pia linatajwa eneo la
pwani ya Japan, ambapo kisahani kimoja kimekipandia kingine.
Wataalamu wa miamba wanaamini kisayansi kwamba,
katika kipindi cha miaka zaidi ya bilioni moja, visahani hivyo vinavyohama
vimepata kuyaleta pamoja mabara hayo kwa muda.
Yalipotokea hayo, ndipo yakandwa mabara
makubwa (super continents)
yanayofikirika, kama Nuna, miaka bilioni 1.8
iliyopita; Rodinia miaka bilioni moja iliyopita, kisha Pangaea lililotokea
miaka milioni 300 nyuma.
Tayari bara kubwa lijalo limeshapewa jina
lake la kufanyia kazi, nalo ni Amasia, kwa sababu wataalamu hao wanadhani Amerika
itaungana na Asia, kwa hiyo wakachukua herufi mbili za mwanzo kwenye ‘Amerika’
na tatu za mwisho kwenye ‘Asia’ kupata ‘Amasia’.
Walichofanya watafiti hawa wanaoendelea kuumiza
vichwa usiku na mchana
ili kuweka sawa haya, ni kupima lini mambo
haya yatatokea kwa kufanya
marejeo ya siku zilizopita, kuangalia watangulizi
wao (wa mabara) aliunganikia wapi.
“Sote tunaielewa vyema dhana ya Pangea,
lakini hapajapata kuwapo
takwimu nyingi toshelezi za kushawishi jinsi
mabara hayo makubwa yalivyounganika,” anasema Ross Mitchel wa Chuo
Kikuu cha Yale. “Katika mfano wetu, ni kwamba
kweli kuwa tunaona Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini zitaungana kwa
kufunga Bahari ya Caribbean na ya Arctic na kuunganisha Amerika na Asia,”
anasema msomi huyo.
Mfano huu wa hali itakavyokuwa, unaeleza
kwamba Amerika (yote ya
Kaskazini na Kusini) itahama na kujikita katika
eneo la Pasifiki linaloitwa ‘mzingo wa moto’. Maono mengine ya kisayansi kwa
kusomea, yanaonesha kwamba bara la Ulaya na sehemu ya lile la Asia linalokaribiana
na Ulaya (Eurasia), Afrika na Australia nayo yanaweza kusogea kuungana hapo,
yakiiacha Antarctika nje.
Utabiri huu una misingi yake katika uchambuzi
wa takwimu za kisumaku
zilizo kwenye miamba kote duniani, ambazo
husaliti mazoea ya kisumaku ya
miamba yake baada ya miaka mingi.
“Miamba inapojengeka, iwe ni kwa kupoa
kwa lava au kuimarika kisedimentari, lazima mwelekeo wa kisumaku utafungiwa
ndani mwake.
“Japokuwa hii inaonesha latitudo kwa usahihi
kabisa, kihistoria bado hatujaweza kuona viashiria vya longitudo.
“Tumeweza kuona kwamba kila baada ya
kuundwa kihistoria kwa mabara hayo makubwa (supercontinents) mabara haya yanapitia
mzunguko wa mbele na nyuma katika mhimili mara kwenye ikweta,” anasema Mitchel.
Akizungumzia utafiti na mada husika, mtaalamu
wa miamba wa Chuo Kikuu Huria nchini Uingereza, Dk David Rothery anasema kwamba
utafiti huo umewafunua watu macho, na kuwafanya kuijua vyema zaidi historia ya
sayari yao.
“Tunaweza kuyaelewa mazingira vyema zaidi
ikiwa tutajua ni wapi hasa yalikuwa.
“Nikiwa Mzungu, sioni kwamba nitajali
sana kwamba mabara yatakuja kuungana kwenye ncha ya kaskazini au kwamba
Uingereza ktakuja kugongana na Amerika katika siku za mbali sana mbeleni.
Makala haya yameandaliwa na Mwandishi
Wetu kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari, kwa kiasi kikubwa
0 comments:
Post a Comment