Na Othman Ame OMPR
Kampuni ya Kimataifa
inayojishughulisha na miradi ya uwekezaji katika sekta ya Viwanda,
Bandari na Uwanja wa Ndege ya ALTEC yenye makamu Makuu yake Nchini
Ukrain imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake hapa
Zanzibar.
Ujumbe wa Kampuni hiyo
umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi ya hivi karibuni aliyoifanya katika umoja wa falme
za Kiarabu { UAE } na kuyaomba Makampuni na Taasisi mbali mbali za
uwekezaji kuja kuwekeza vitega uchumi vyao hapa Zanzibar.
Ujumbe wa Viongozi wa
ngazi ya juu wa Kampuni hiyo yenye tawi lake Umoja wa Falme za Kiarabu
kwenye Mji wa Dubai ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Dr. Ramzan
Musipov ulieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Zaidi ya Dola za
Kimarekani Bilioni kumi { U$ Dollar 10,000,000,000 } zitatengwa na
kampuni hiyo katika mpango wake wa kutaka kuwekeza katika sekta ya
Mafuta na Gesi, Bandari, pamoja na uwanja wa ndege.
Ujumbe huo ulimueleza
Balozi Seif kuridhika na mazingira mazuri yaliyopo ya uwekezaji vitega
uchumi hapa Zanzibar na uko tayari kutumia fursa hiyo katika kuona sekta
ya Viwanda inakuwa ili isaidie kuimarisha ustawi wa wananchi wa
Zanzibar.
Naye kwa upande wake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza
ujumbe wa Kampuni ya altec kwa uamuzi wake iliyouchukuwa wa kuangalia
mazingira ya uwekezaji ndani ya visiwa vya
Zanzibar katika kipindi kifupi tokea kupata fursa hiyo.
Balozi Seif alisema
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar iko katika mpango wa kupanua Bandari
yake sambamba na kuimarisha miundo mbinu katika uwanja wa ndege wa
Pemba kwa lengo la kuongeza mapato yake.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliufahamisha ujumbe huo wa Kampuni ya Altec kwamba mkazo
umeongezwa zaidi kwenye sekta ya uchumi kwa kuimarisha eneo la utalii
ambalo linaonekana kusaidia uchumi wa Zanzibar unaotegemea zaidi hivi
sasa zao la Karafuu.
Hata hivyo Balozi Seif
alisema ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ulioachwa milango wazi kwa
kushirikisha washirika wa maendeleo njeya ya nchi utaongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi pamoja na kupanua soko la ajira kwa kundi mkubwa la
vijana wanaomaliza masomo yao.







0 comments:
Post a Comment