MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto,
ameendelea kusisitiza kuwa hadi sasa hakuna chama chochote cha siasa
kilichowasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake kwa Msajili wa Vyama
vya Siasa na kuvitaka vyama hivyo kuacha propaganda na kulichukulia
suala hilo kisiasa.
Amesema hazungumzi suala hilo kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, bali
anasimamia Sheria na kama hawataki, wamshauri Spika wa Bunge, Anne
Makinda, avunje kamati yake.
“Napenda niwaambie nazungumzia suala hili si kama Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema bali Mwenyekiti wa PAC na ninasimamia sheria,” alisema.
Akizungumza jana katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam,
Zitto alisema tangu atoe tamko la kutaka vyama hivyo vijiandae kujieleza
kwanini havijawasilisha ripoti hizo za ukaguzi, amekuwa akisikia kelele
tu na hakuna chama chochote kilichotekeleza kisheria jukumu hilo la
kuwasilisha taarifa zake kwa Msajili tangu 2009 kama vinavyodai.
“Najua kuna vyama vinajitetea kuwa tayari vimefanya ukaguzi wa hesabu
zake, sasa kama kweli ziko wapi hizo ripoti, Sheria iko wazi, ukaguzi
ukikamilika ripoti inatakiwa kuwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti
wa Hesabu za Serikali (CAG), na Msajili na si kuzifungia kabatini,”
alisisitiza Zitto.
Alisema amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
kuwaandikia barua ya kisheria viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku
ya Serikali, ya kuwaita mbele ya kamati hiyo, Oktoba 25, mwaka huu ili
kujieleza kwanini hawajawasilisha ripoti hizo kwa Msajili kwa kipindi
cha miaka minne iliyopita.
Vyama hivyo ambayo vimeshakula Sh bilioni 67.7 bila kutoa ripoti ya
matumizi yake ni CCM Sh bilioni 50.9, Chadema Sh bilioni 9.2, CUF
bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi Sh milioni 677, TLP Sh milioni 217, UDP Sh
milioni 333, DP Sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo Sh milioni 11 na Chausta
Sh milioni 2.4.
SOMA ZAIDI: HABARILEO ONLINE
0 comments:
Post a Comment