MWANAMUZIKI mashuhuri wa taarab Isha Ramadhan maarufu kama
Isha Mashauzi (25) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo
akikabiliwa na mashitaka ya wizi.
Isha ambaye ni mkazi wa Kinondoni pamoja na mwenzake Halima Shabani
(26) walifikishwa mahakamani hapo jana kusomewa mashitaka yanayowakabili mbele
ya Hakimu Matrona Luanda.
Karani Blanka Shayo wa mahakama hiyo, alidai mbele ya Hakimu
Luanda kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 20, mwaka huu katika
mtaa wa Mafia na Jangwani eneo la Kariakoo.
Shayo alidai kuwa siku ya tukio, washitakiwa wote kwa pamoja
waliiba pochi moja ya mkononi iliyokuwa na Sh 758,000 kutoka dukani kwa Sara
Peter, mali ya Veronica Taki.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashitaka hayo, walikana kutenda
kosa hilo na washitakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya
kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshitakiwa aliyetakiwa kusaini hati ya dhamana
ya Sh milioni 1.5. Kesi hiyo itatajwa tena Mei 14, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment